loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Hata urais ungekuwa miaka 5 JPM angeacha alama

NATAKA niwe mkweli kwa nafsi yangu kuwa, hata kama tungekuwa kama nchi kuwa na utaratibu wa kuwa na Rais wa kipindi cha miaka mitano tu, basi, huyu tuliye naye sasa, John Pombe Magufuli, angekuwa amemaliza muda wake wa miaka mitano akiwa ameacha alama kubwa nyuma yake.

Alama za kudumu daima. Ni ukweli nchi yetu imebadilika kwa kasi na fikra za watu wake pia zimeanza kubadilika.

Maana, ilifika mahali, kuna walioacha kazi kwenye mashirika yasiyo ya kiserikali na kwenda kufanya kazi serikalini, ikiwamo kwenye halmashauri zetu wakitamka wazi kuwa kwenye mashirika hayo kazi ni nyingi, wanarudi serikalini na kwenye halmashauri kupumzika na kula posho za safari na nyinginezo.

Nchi haiwezi kusonga mbele ikiwa na watu wenye mitazamo kama hiyo.

Ni lazima kuwe na nidhamu ya utendaji kazi na kuheshimu sheria, kanuni na taratibu. Na wenye kukiuka hayo ni lazima wajue kuna adhabu yenye kuendana na matendo yao maovu. Ndiyo siri kubwa ya nchi za wenzetu zilizoendelea.

Nimepata kuandika kuwa, Magufuli ana uwezo wa kumwona bata na sungura kwa wakati mmoja.

Hii ni dhana kongwe ya kimtazamo iliyojengeka kifalsafa. Ni uwezo wa mwanadamu katika taswira moja kuwaona viumbe wawili wenye kufanana.

Hivyo, inahusu uwezo wa kuliona jambo hilo hilo katika sura tofauti. Ndio, kuna kuona kikiwa na kuona kama. Kuliangalia jambo kwa mtazamo tofauti.

Mwanafalsafa Thomas Kuhn, yeye anazungumzia dhana ya’ ‘Paradigm Shift’. Ni ile hali ya uwapo wa mapinduzi ya kifikra na ya kisayansi yenye kupelekea mabadiliko ya kimsingi katika jambo lile lile tulilokuwa na mazoea nalo.

Kapteni Thomas Sankara, kiongozi mwanapinduzi aliyeuawa Burkina Faso, katika wakati wake, alizungumzia umuhimu wa kuwa na ujasiri wa kuyapa mgongo mazoea ya kale. Sankara aliacha haiba njema ya kuenziwa ndani ya nchi yake, Afrika na duniani.

Mwanamapinduzi huyu alikuja kuuawa kwa kupigwa risasi na wapinga mapinduzi na maendeleo ya Burkina Faso. Sankara alipata kukaririwa akisema: “Ningependa kuacha nyuma yangu imani ya kuwa, kama tunaimarisha kiwango fulani cha uangalifu na oganaizesheni, basi, tunastahili ushindi.”

“Kamwe huwezi kuleta mabadiliko ya kimsingi bila ya kuwa na kiwango fulani cha ‘uwendawazimu’.”

“ Hali hii inatokana na kutoshinikizwa na taratibu zilizoeleka, kuwa na ujasiri wa kuzipa mgongo kanuni za kizamani, ujasiri wa kuanzisha mustakabali.

Ni ‘wendawazimu’ wa jana waliotuwezesha kuyafanya tuyafanyao leo. Ninataka kuwa mmoja wa ‘wendawazimu’ hao.” (Hayati, Kapteni Thomas Sankara) Yumkini tunachokishuhudia kwenye nchi yetu ni Magufuli’s paradigm shift’. Hali ya kuwa na mabadiliko ya msingi.

Nimeona nini kwa Rais Magufuli baada ya miaka mitano? Kama urais ungelikuwa wa miaka mitano, basi, Rais tuliye naye, Dk John Pombe Magufuli, angeondoka akiwa ameacha alama chanya za kudumu milele.

Maana, akipewa miaka mitano mingine, ninachoona ni upepo chanya wa Magufuli wenye kuendelea kuvuma ndani na nje ya mipaka. Huo ndio ukweli mwingine ningependa kuusema. Nimepata bahati ya kusafiri sehemu mbali mbali za nchi. Nimekuwa na mazoea ya kuzungumza na wananchi kupata mitazamo yao.

Mahali pengi kabisa, John Magufuli yumo kwenye midomo ya Watanzania wa kawaida walio wengi, wakiwemo vijana ma-bayaye wanaoongezeka kwenye miji yetu. Kwanini? Naamini, John Magufuli amefaulu sio tu kubeba ajenda ya vita dhidi ya ufisadi, rushwa na uhujumu uchumi, bali anaifanyia kazi ajenda hiyo na watu wanaona ikifanyiwa kazi.

Ni kwa kiwango kile ambacho Hayati Edward Sokoine alikuwa anakwenda nacho na akawa kipenzi cha umma.

Niliandika huko nyuma kuwa, kero nambari moja kwa Watanzania kuelekea uchaguzi mkuu uliopita ilikuwa rushwa na ufisadi, kero nambari mbili ilikuwa rushwa na ufisadi na kero nambari tatu ni rushwa na ufisadi.

Hivyo, hiyo ndio ilikuwa ajenda kuu. Huko nyuma upinzani, tofauti na CCM, ndio ulibeba ajenda hiyo, wakaipoteza njiani, sasa upinzani unahangaika kutafuta ilichokuwa nacho.

Ndio maana, tofauti na huko nyuma, maeneo mengi nilimopita huwezi sasa kuona tofauti za wananchi za kiitikadi, wote wanajadili ajenda moja, ya kupiga vita ufisadi na hali zote zenye kurudisha nyuma maendeleo yao.

Wanamuunga mkono Rais John Magufuli. Hao ni Wana CCM, Wana- Chadema na wa vyama vingine. Jipya jingine ndani ya miaka mitano ni kitendo cha Rais Magufuli kuruhusu wananchi kutoa kero zao hadharani kwa kuandika kwenye mabango. Hali hii inaongeza uwajibikaji na kuwatia kiwewe viongozi warasimu na wenye kuwanyanyasa wananchi.

Hawa huko nyuma walijificha kwenye risala kwa Rais ambazo zilikuwa na maana ya kumsomea Rais taarifa ya kumfurahisha na wananchi hawakuwa na pa kumsomea Rais risala inayotokana na wao wananchi.

Siku hizi inawezekana kupitia mabango. Wananchi wanamuunga mkono pia Rais Magufuli kwa nia yake ya dhati ya kusimamia rasilimali za taifa hata kuwa tayari kugombana na matajiri wamiliki wa kampuni kubwa za uchimbaji madini.

Haijawahi kutokea wala kufikiriwa kuwa, kama nchi, tungeweza kutunisha misuli na kufanikiwa kushinda kwenye meza ya majadiliano, kwenye kudai kipande kikubwa cha keki kwa maana ya kinachopatikana kutokana na uchimbaji wa madini yetu. Vita hivi vya kupigania rasilimali zetu.

Vita hivi anavyoviongoza Rais Magufuli vimemsogeza karibu zaidi kwenye mioyo ya wananchi ambao huko nyuma walianza kukata tamaa. Kimataifa, Rais John Magufuli ametolewa mfano wa kuwa kiongozi mwenye kusimamia uwajibikaji.

Nimepata kuongea na maofisa wawili waandamizi wa Balozi za Kimagharibi walioniambia wazi kuwa, Rais Magufuli anafanya vema sana kwenye eneo la uwajibikaji na kukuza uchumi.

Mwingine akafikia kuniambia kuwa, haijawahi kutokea kwa serikali ya Tanzania kurudisha fedha za misaada ambazo hazikutumika au zimepotea kutokana na ufisadi. Ndani ya miaka miwili ya mwanzo, kwa mshangao wa ofisa yule wa ubalozi niliyeongea nae, aliniambia Balozi yao ilipokea fedha ambazo Tanzania ilikuwa inadaiwa irudishe. Nini tafsiri ya jambo hilo?

Kwa mujibu wa ofisa yule wa kibalozi, kubwa kabisa serikali inayoongozwa na Rais Magufuli sasa inaaminika na wahisani na mabenki yenye kukopesha.

Kwamba kuna usimamizi na ufuatiliaji wa fedha za miradi ya maendeleo. Kwamba sasa si rahisi fedha kuliwa na wajanja na kwamba zitafanya yale yenye kuwaletea wananchi maendeleo. Nini siri kubwa ya hatua hii mpya?

Nilimwuliza ofisa yule wa ubalozi. “Ukiwa na Rais aliye juu na anayesimamia kwa vitendo yale yanayotakiwa kufanyika, basi, huku chini watendaji hubadilika haraka na kufanya kilicho sahihi na hata kuwa na hofu ya kufanya ufisadi,” alianiambia ofisa yule wa ubalozi. Nini faida na hatari ya mafanikio haya ya Rais Magufuli?

Kwa nchi, hii ni fursa pekee ya kuungana na kumkabili adui aliye mbele yetu na aliyetufikisha hapa tulipo. Waliotufikisha mahali ambapo akina mama na watoto wetu wakakosa dawa na huduma nyingine muhimu.

Wananchi wakakosa mabomba ya maji na mengineyo, huku wachache wakichota fedha za umma kwa rushwa na ufisadi.

Baada ya miaka hii mitano, hatusomi tena habari za ufisadi mkubwa ukifanyika kwenye halmashauri na kwengineko serikalini. Hatari ninayoiona mbele yetu ni pale tunapokuwa na Rais mwenye ushawishi mkubwa wa kisiasa na kiuongozi ndani ya chama chake na serikali.

Rais anayekubalika na wananchi wengi. Kwamba akitumia vema ushawishi huo na kwa kutanguliza hekima na busara, nchi yetu itakuwa mfano katika bara hili, ikiwamo pia kuimarisha misingi ya demokrasia na utawala wa sheria.

Lakini, kama Rais mwenye haya akaja akaota mapembe, basi, hapo itabaki kuomba majaaliwa ya maanani.

UZURI wa ngozi huanzia ndani. Hivyo unavyoitunza ngozi yako kwa ...

foto
Mwandishi: Maggid Mjengwa

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi