loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Yanga Vs Kagera mechi ya kisasi

KIKOSI cha Yanga kimepania kuibuka na ushindi dhidi Kagera Sugar, kwenye mchezo wa hatua ya robo fainali katika muendelezo wa michuano ya Kombe Shirikisho (FA) utakaofanyika leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Yanga wanahitaji ushindi kwenye mchezo huo ili kukata tiketi ya kutinga hatua ya nusu fainali kwenye michuano hiyo na kuanza kujitengenezea nafasi ya kuipeperusha bendera ya nchi kwenye michuano ya kimataifa.

Mabingwa hao wa kihistoria wa Ligi Kuu Tanzania Bara, wamebaki na nafasi moja tu ya kuliwakilisha taifa kimataifa kupitia Kombe la FA baada ya kushindwa kuivua Simba ubingwa.

Mchezo huo unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa, ambapo Yanga wanahitaji zaidi ushindi ili kulipa kisasi cha kufungwa mabao 3-0 kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kuelekea kwenye mchezo huo, kocha wa Yanga Luc Eymael alisema kikosi chake kimejipanga na kuwahakikishia wapinzani wao kuwa zama za kuendelea kuwa mteja wa Kagera Sugar zimepita na sasa wanataka kuandika historia mpya.

“Tunaingia kwenye mchezo muhimu ambao unahisia nyingi kutoka kwa mashabiki, hasa wakiwa na kumbukumbu ya kutoka kutufunga mabao 3-0 tulipo kutana kwenye mchezo wa ligi, lakini niwaambie tu mashabiki watulie, kwani zama za kuendeleza uteja zimeisha tutaingia kwa lengo la kutafuta ushindi tu,” alitamba Eymael.

Alisema wamefanya maandalizi ya kutosha, ikiwemo kufanyia kazi sehemu ya ushambuliaji na ushindi walioupata kwenye mchezo uliopita dhidi ya Ndanda umewaongezea ari yaushindi katika mchezo huo.

Kocha wa Kagera, Mecky Maxime alisema kikosi chake kimeshawasili salama Dar es Salaam na wanajipanga kwa mchezo huo ili kujiweka nafasi nzuri ya kuwakilisha nchi kimataifa.

Alisema hawatishiki na kelele za kocha wa Yanga, Eymael isipokuwa wanautazama mchezo kwa kwa uzito mkubwa wakijua wanaenda kukutana na ushindani kwakuwa kila timu itakuwa imejipanga kusaka ushindi.

“Siwezi kusikiliza kelele za kocha wa Yanga, tumemsikiliza kwa muda mrefu sasa imetosha, kikosi chake kina malengo ya kupata ushindi ili kuiwakilisha nchi kimataifa,“alisema Maxime.

Kagera wanaingia kwenye mchezo huo wakiwa na kumbukumbu ya kutoka sare ya 1-1 kwenye mchezo uliopita wa Ligi Kuu dhidi ya KMC uliofanyika katika Uwanja wa Kaitaba, Bukuba.

Mchezo mwingine wa michuano hiyo leo, Namungo FC watawaalika Alliance katika mchezo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Majaliwa Lindi

MWIGIZAJI maarufu wa tamthilia ya Karma, Wema Sepetu amewaomba radhi ...

foto
Mwandishi: Tuzo Mapunda

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi