loader
Dstv Habarileo  Mobile
Serikali yatoa bil 48/- kujenga vyuo Veta

Serikali yatoa bil 48/- kujenga vyuo Veta

SERIKALI imetangaza kutoa Sh bilioni 48 kwa ajili ya ujenzi wa vyuo vya Ufundi Stadi nchini (VETA) katika halmashauri za wilaya 29 nchini.

Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako alisema hayo akifungua chuo cha Veta cha Nyamidaho wilayani Kasulu mkoani Kigoma jana.

Alibainisha kuwa serikali ipo kwenye mpango kabambe wa kuandaa wataalamu watakaotosheleza mahitaji ya nchi katika uchumi wa viwanda.

Profesa Ndalichako alisema kuwa kumekuwa na mahitaji makubwa ya vijana wenye taaluma za ufundi kwenye kazi mbalimbali na wanafunzi wanaoenda kwenye mafunzo kwa vitendo wamekuwa waking’ang’aniwa kubaki kwenye maeneo wanayofanya mazoezi yao kwa vitendo.

“Kwa Sasa vijana wanaomaliza VETA wamekuwa na mahitaji makubwa kwenye soko la ajira na kwenye fursa za kujiajiri.

“Ni lazima kupanua wigo kuhakikisha mafunzo hayo yanawafikia Watanzania kila mahali na kwa urahisi, kuanzia mwezi ujao, Sh bilioni 48 zitaanza kupelekwa kwenye maeneo husika ili miradi ya ujenzi ya vyuo hivyo uanze,” alisema.

Mwenyekiti wa Bodi ya Veta, Peter Maduki alisema kuwa kwa sasa, Veta inafanya maboresho makubwa katika utoaji wa elimu ili taaluma inayotolewa iweze kukidhi mahitaji ya Watanzania katika ajira ikiwemo kujiajiri wenyewe.

Katika uzinduzi huo, Maduki aliahidi kutoa mafunzo ya ufundi uandishi bila malipo kwa wananchi wa Kijiji Cha Nyamidaho watakaojiunga na mafunzo hayo katika chuo cha Nyamidaho.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Veta, Pancras Bujuru akitoa taarifa ya ujenzi wa chuo cha Veta, Nyamidaho wilayani Kasulu mkoani Kigoma alisema kuwa Sh milioni 477.4 zimetumika kufanyia marekebisho chuo hicho na kufikia viwango vya utoaji elimu vinavyosimamiwa na Veta kutoka chuo cha ufundi kilichokuwa chini ya usimamizi na uendeshaji wa halmashauri ya Wilaya ya Kasulu.

Mkurugenzi huyo alisema kuwa chuo hicho kimekarabatiwa kwa majengo ambayo yalijengwa na Shirika lisilo la kiserikali la World Vision ambalo lilijenga majengo matano mwaka 1994 na mwaka 2019 chuo hicho kilikabidhiwa kwa uongozi wa halmashauri ya wilaya Kasulu.

Mkuu wa Mkoa Kigoma, Emanuel Maganga aliwataka wananchi kutovichukulia vyuo hivyo kama mahali wanaposoma walioshindwa kielimu kwani wanafunzi wanaomaliza wamekuwa na taaluma kamili na kupata soko kubwa kwenye soko la ajira.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/1d4ac76d4d93ee5966162d2a4e49be8d.jpg

ALIYEKUWA Mbunge Mteule wa Jimbo la Konde ...

foto
Mwandishi: Fadhili Abdallah, Kigoma

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi