loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wizara Kilimo yazalisha wataalamu 16, 570

WIZARA ya Kilimo imesema imepata mafanikio makubwa kwa kuzalisha wataalamu wa kilimo 16,570 nchini kupitia vyuo vyake na kuipaisha sekta ya kilimo kuchangia asilimia 28.2 ya Pato la Taifa.

Wataalamu hao walizalishwa kati ya mwaka mwaka 2009 na 2018. Kauli hiyo imetolewa jana mjini hapa na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya alipofungua kikao kazi cha siku mbili cha wakuu wa vyuo vya mafunzo ya kilimo (MATI) chini ya wizara hiyo.

Kusaya alisema anatambua vyuo vya mafunzo ya kilimo vya kati ni kiwanda cha kuzalisha wataalam wenye sifa zinazohitajika soko la ajira au ajira binafsi katika mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo.

“Vyuo vya mafunzo ya kilimo vimetoa mchango mkubwa kuhakikisha nchi ina wataalamu wa kutosha wenye weledi wa kusimamia sekta ya kilimo ambapo jumla ya wataalamu 16,570 walihitimu mafunzo yao kwenye vyuo vya mafunzo ya kilimo nchini kati ya mwaka 2009 hadi 2018,” alisema Kusaya.

Katibu Mkuu aliongeza kuwa sekta ya kilimo imeendelea kutoa ajira kwa Watanzania kwa asilimia 58, imechangia asilimia 28.2 ya Pato la Taifa ambako sekta ndogo ya mazao imechangia asilimia 16.2.

Ili kuwa na vyuo bora na vyenye tija, ameagiza wakuu wa vyuo vyote 14 chini ya wizara hiyo kuweka msisitizo kufanya mapinduzi ya kilimo kwa kufundisha wanafunzi kwa vitendo zaidi ili kujenga umahiri.

“Sisi ndio vyuo vya kilimo lazima tuoneshe kuwa tunafanya kilimo cha kisasa. Itakuwa jambo la ajabu kukuta chuo hakina shamba darasa bora la kufundishia wanafunzi,” alisisitiza Kusaya.

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu huyo amevipongeza vyuo vya kilimo nchini kwa kazi nzuri wanayoifanya kufundisha wanafunzi na wakulima mbinu bora na za kisasa za kukuza sekta ya kilimo.

“Nawapongeza na ningependa kuona mnaongeza kasi na kuwajengea uwezo wanafunzi katika maarifa na ujuzi wa kilimo biashara kwa vitendo ili kufikia lengo la kuongeza uzalishaji na kuiwezesha Tanzania kupata malighafi kwa urahisi zaidi kwa ajili ya viwanda vinavyozunguka maeneo yenu,” alieleza.

Kikao kazi hicho cha siku mbili kimelenga kuweka mipango imara ya kuhakikisha mafunzo yanayotolewa yanakidhi viwango vinavyohitajika kwenye soko la ajira na kujiajiri. Hivyo wakuu wa vyuo hivyo watajadili changamoto na mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amezipa ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu, Morogoro

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi