loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Biashara magendo Sirari inavyonyonya mapato ya Serikali

“PENYE msafara wa mamba, kenge hawakosekani.”

Ndiyo unavyoweza kusema kwani wakati Watanzania chini ya Uongozi wa Serikali ya Rais John Magufuli wakiwa katika msafara wa kuelekea kwenye uchumi wa kati unaochochewa na viwanda, wapo kenge waliojitokeza kunyonya uchumi wa nchi kupitia biashara ya magendo.

Hao ni baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu wanaoshirikiana na wenzao kutoka nchi jirani huku wengine wakiwa na uraia wa nchi mbili wanaotorosha na kusafirisha kinyemela bidhaa mbalimbali za Tanzania yakiwamo madini ya dhahabu, kemikali, mifugo na nafaka kinyume cha taratibu na sheria na hivyo, kukosesha nchi mapato yake.

Katika kipindi cha Machi 2019 hadi Juni 2020, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Tarime mkoani Mara kwa kushirikiana na baadhi ya maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Kituo cha Sirari na raia wema kwa kutoa taarifa, imefanikiwa kukamata mali mbalimbali za magendo yakiwemo madini ya dhahabu yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 3 na bidhaa mbalimbali zinazotoka ndani ya nchi na kuingizwa nchini kinyume cha utaratibu na kuikosesha serikali mapato.

Uchunguzi wa mwandishi wa makala haya katika maeneo mbalimbali ya mpaka wa Kenya na Tanzania likiwamo eneo la Sirari, bidhaa nyingine inayotoroshwa kwenda nje ya nchi aukuingizwa nchini kinyemela, ni pamoja na kemikali kama spiriti zinazotengeneza pombe kali zaidi ya mapipa 500, sigara zinazotoka nchini Burundi, mifugo na nafaka mbalimbali kama mchele na mahindi.

Imebainika kuwa, bidhaa hizo zimekuwa zikisafirishwa bila kufanyiwa ukaguzi wa ubora wala wamiliki kuwa na leseni au vibali husika vya kusafirisha bidhaa hiyo kwenda nje ya nchi.

Hali hii inaikosesha mapato serikali na kuhamisha ajira kwani bidhaa yakiwamo mazao hayo kama yangechakatwa nchini na kuongeza thamani, yangezalisha ajira japo za muda mfupi, serikali ingepata ushuru, mazao au bidhaa hizo zingeongezwa thamani na kuwa na tija zaidi na pia, wanunuzi wangekuja kununulia nchini.

“Wakati wanakuja na kununua, wanunuzi hao wangefanya manunuzi mbalimbali nchini, ikiwa ni pamoja na kulala na kula, hivyo kuchochea mzunguko wa pesa nchini,” anasema mchumi mmoja wilayani Tarime anayekataa kutajwa.

Wakazi wa Wilaya ya Tarime wakiwemo wafanyabiashara waliojitambulisha kwa majina ya John Marwa, Mwikwabe Manko, Mang’era Boroye, Elizabeth Samwel, Bhoke Chacha, Alois Johanes na Wambura Nyamhanga, wanasema biashara za magendo zinazorotesha maendeleo ya nchi na kufifisha juhudi za serikali kutoa na kuboresha huduma za kijamii zikiwamo za afya, elimu na miundombinu.

“Kwa mfano, wafanya magendo wanaoingiza dawa, wengine wanaleta dawa feki na zilizoisha muda wa matumizi,” anasema Marwa. Naye Elizabeth anasema:

“Hao, wanaziuza kwa bei rahisi na kuua biashara za wauza dawa halisi na halali, lakini wakati huo huo hao wafanya magendo wanahatarisha afya za watu maana dawa zilizoisha muda ni sumu na hatari kubwa.” Mkuu wa Wilaya Tarime Mtemi Msafiri katika kikao na Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), Biswalo Mganga anasema:

“Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Tarime imejipanga kukabiliana na wafanyabiashara wa magendo katika maeneo yote yakiwamo ya vijiji vya mipakani.

Anaongeza: “Wafanyabiashara wote wanatakiwa kufuata taratibu na sheria za nchi kwa kufanya biashara halali na kulipa kodi kulingana na bidhaa wanazosafirisha kwenda au kutoka nje nchi kwa kufuata taratibu maana serikali haitakuwa na msamaha na mkwepa kodi, au mfanya magendo yeyote.”

Hata hivyo, serikali na vyombo vyake haina budi kupongezwa kwani mara kadhaa mwandishi wa makala haya ameshuhudia baadhi ya wafanyabiashara wa magendo wakikamatwa wanapojaribu ‘kuvusha’ mali hizo.

Imeshuhudiwa pia baadhi ya mali yakiwamo magari yaliyotumiwa kusafirisha mali za watuhumiwa kutaifishwa na watuhumiwa wenyewe kupigwa faini na kutakiwa kulipa fidia kwa serikali ama kuhukumiwa kwenda jela kutumikia kifungo.

Kuhusu juhudi za serikali kukabili biashara ya magendo na uhujumu uchumi kwa jumla, hivi karibuni DPP Mganga, alifika wilayani Tarime katika kesi dhidi ya mfanyabiashara mwenye asili ya Kiasia mkazi wa jijini Mwanza katika Mtaa wa Nkrumah, Bhawesh Cha ndulal Gandecha (50).

Mfanyabiashara huyo alikuwa amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Tarime akituhumiwa kupatikana na dhahabu bila kibali na pia, kusafirisha madini hayo kwenda nje ya nchi bila leseni huku akidanganya katika nyaraka zake zilizoonesha uhalali wa madini hayo.

Mahakama ilimtia hatiani na kumtoza faini ya Sh 115,000,000 na kulipa fidia ya serikali ya Sh 20,000,000 ama kutumikia kifungo cha miaka saba jela.

Gari lililotumiwa kusafirisha madini hayo lenye namba T 366 DKY aina Toyota Land Cruser lilitaifishwa.

Akiwamo mkoani hapa hivi karibuni, DPP Mganga alifanya kikao na Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Mara na Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Tarime kukiwa na Mkuu wa Mkoa wa Mara Adam Malima na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Mtemi Msafiri na kamati za ulinzi na usalama.

Katika kikao hicho, Mganga anasema: “Serikali iko macho dhidi ya wafanya magendo na wote siku zao zinahesabika…

Anayekamatwa na mali za magendo, kwanza mali hiyo inataifishwa, chombo kilichobeba mali hiyo kinataifishwa na mhusika mwenyewe anafikishwa mahakamani kupigwa faini na kulipa fidia ya serikali, ama kwenda jela.”

Anasema: “Katika miaka 5, serikali imekamata kilo 425 za dhahabu yenye thamani ya mabilioni ya fedha ikisafirishwa kinyume cha sheria kwenda nje ya nchi…. Serikali inawaomba wananchi waendelee kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa sahihi za uhalifu ukiwemo huo wa biashara za magendo mipakani unaoikosesha serikali mapato.”

Anaongeza: “Serikali itaendelea kuwalinda wafanyabiashara halali kwani hao ni kama mayai meupe na wale wanaofanya biashara haramu ya magendo ni kama mayai meusi fedha zao za utakatishaji ni haramu na mkono wa sheria utawakumba.”

Matukio mengine ya kusafirisha mali za magendo yaliyokamatwa ni pamoja la Wachina wanne waliokamatwa katika Mpaka wa Sirari wakisafirisha dhahabu kg 300.75 wakitumia gari aina ya Toyota Land Cruiser lenye namba KBW 515 Y.

Wachina wengine walikamatwa wakisafirisha dhahabu kwenda nchini Kenya na kukamatwa wakiwa wameweka dhahabu ndani ya ndoo katika gari lao lenye namba T 994 DHC aina Toyota.Mahakama ya Wilaya ya Tarime iliwatia hatiani watuhumiwa hao na kuwatozwa faini na fidia ya ya Sh 300,000,000 ama kwenda jela miaka 5 huku magari yao yakitaifishwa.

Magendo mengine yaliyokamatwa ni madini aina ya mbalimbali yakiwemo ya dhahabu yenye uzito kg 28.116. Wahusika wa madini hayo walikuwa Wachina 3 na Mtanzania mmoja aliyekuwa dereva wa gari lao.

Wafanyabiashara hao Wachina ni pamoja na Yong ZheYe (32), Chang Shaolo (31), Xaolin Wang (25) na dereva Mtanzania, Herinoko Shija (51) waliokuwa wakisafirisha madini hayo katika Barabara Kuu ya Musoma - Sirari kwenda nchi jirani ya Kenya kinyume cha utaratibu.

Baada ya kufikishwa mahakamani na kupatikana na hatia, madini hayo na gari lililokuwa linatumika yalitaifishwa na wahusika wapigwa faini na fidia ya kila mmoja kulipa Sh 105,000,000 au kwenda jela miaka 5 kwa Wachina hao.

Walilipa faini na fidia ya Sh milioni Sh 315,000,000 na kukwepa kifungo hicho. Magari mengine yaliyokamatwa yakisafirisha magendo yakiwamo zaidi ya mapipa 400 ya kemikali aina ya spiriti kwenda Kenya kupitia njia za panya ni pamoja yenye namba KBY 753 Y lenye tela namba ZE 7297.

Lingine ni lori lenye namba za usajili KBD 673 W na tela lenye namba ZD 216 Y yaliyokamatwa katika Kijiji cha Kubiterere yakivushwa kwenda Kenya kinyume cha sheria.

Kwa mujibu wa Meneja wa TRA Mkoa wa Mara, Walles Mkande, bidhaa nyingine zilizokamtwa zikiingia nchini kwa njia za panya ni pamoja na mafuta ya kula, sabuni, sukari, viberiti na chumvi.

Lori aina ya Scania lilikamtwa likiwa na katoni zaidi ya 2000 za sigara kutoka Burundi zilizokuwa zikisafirishwa kwenda Kenya bila vibali wala leseni ya kusafirisha sigara hizo za zaidi ya Sh milioni 300 huku mapipa ya kemikali ya spiriti zaidi ya 500 yakikamatwa yakisafirihwa kwenda nje ya nchi bila vibali.

Mkande anayataja maeneo yaliyoshamili magendo ni hasa yale ya mipaka ya Vijiji vya Sirari, Kubiterere, Borega, Kegonga, Ikoma na Kogaja.

Mei 21, 2020 maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Kituo cha Sirari na maofisa wa usalama walikamata lori aina ya Fuso lenye namba za usajili T 806 DSY mali ya Victor Nyagoye wa Arusha likiwa na Marobota 222 ya vitenge vilivyotengenezwa China na kupitishwa njia za Panya kutoka nchini Kenya katika mpaka wa Kijiji cha Kubiterere kukwepa ushuru wa Serikali.

FIGO ambayo jukumu lake kubwa ni kuchuja damu na kutoa ...

foto
Mwandishi: Samson Chacha

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi