loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Rangi ya Mbatia upinzani ina matumaini kwa umma

TANGU Tanzania iingie katika mfumo wa siasa wa vyama vingi, imeshuhudia kuwapo kwa viongozi wa namna mbalimbali wakiwamo wanaotaka demokrasia inenepeshwe zaidi, na wengine wanaotaka ‘kuibemenda’ kwa kupitia ‘domokghasia.’

Viongozi na wanasiasa ambao ni wafuasi wa domokghasia, wengi wakionekana kutoka katika baadhi ya vyama vya upinzani, wao wamejigeuza na kutembelea mikono, badala ya kutembelea miguu.

Maisha yao ni mithili ya maisha ya bundi; mchana bundi analala wakati wanyama wengine wakiwamo binadamu wanafanya kazi za hapa na pale ‘mkono uende kinywani’ na kujiongezea maendeleo katika nyanja na sekta mbalimbali.

Bundi yeye wakati huo, amelala; anasubiri usiku wakati wengine wamelala, yeye ndo kumekucha; ndiyo maana bundi anahusishwa zaidi na ushirikina katika baadhi ya jamii (watu). Wapinzani wengi; siyo wote, hawana tofauti na bundi na ndiyo sababu baadhi yao kila wanapoanza kuzungumza, lazima mamia kwa mamia ya watu watasikika wakitoa miguno “Khaaa!” na kufuatiwa na maneno:

“Huyu naye,.. ameanza.” Hii inaonesha kuwa, thamani ya wanasiasa imechacha na kuharibu ladha kutokana na maneno na matendo yao yanayoonesha kuwachekea ‘wananchi mchana’, lakini ‘usiku wanawazomea’ wananchi haohao. Hao ndio wanasiasa wanaosema nchi inataka kiongozi makini; lakini kiongozi makini anapopatikana wanalalamika. Wanasema wanataka maji, maji yakipatikana wanalalamika. Yapo mengi ambayo wapinzani wamekuwa wakiyapigia kelele na kufanikiwa kufanya mvuto kwa wananchi ndiyo maana katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015, Chama Cha Mapinduzi (CCM) ilibidi kifanye kazi kubwa kumpata mgombea wa urais aliyekubalika vinginevyo, kilikuwa hatarini ‘kuangukia pua.’

Cha kushangaza, Mgombea Urais wa Tanzania kupitia CCM mwaka 2015, John Magufuli alipozoa kura na kuanza kutumikia Watanzania akiwa rais, akawa msikivu katika serikali sikivu.

Kwangu mimi, Rais Magufuli alianza kufanyia kazi zile kero ambazo wapinzani walikuwa wanazipigia kelele wakitaka ziondolewe.

Akaziondoa. Akafanya yale ambayo wapinzani walikuwa wakisema kama yakifanyika, Watanzania watapata maendeleo. Akayafanya kwa ubora zaidi. Mwisho japo siyo kwa umuhimu, akatekeleza Ilani ya CCM.

Matokeo, ndiyo maendeleo tunayoyashuhudia katika sekta mbalimbali ikiwamo miundombinu na ubora wa huduma za usafiri na usafirishaji (ndege, barabara, boti na meli), huduma za mawasiliano hata ya simu zimeimarika mpaka vijijini kulikosahaulika, sasa wapo katika mtandao; na elimu bila malipo hadi kidato cha nne iliyowezesha watoto wa maskini nao kupatta haki hiyo.

Ongezeko la idadi ya wanafunzi na upungufu wa madarasa unaosikika mara kwa mara ni changamto ndani ya mafanikio ya sera ya elimu bure maana watoto wengi sasa wanakwenda shule na wengi wanakwenda sekondari.

Yapo mengi mazuri na makubwa aliyoyafanya Rais Magufuli kuitikia kilio cha Watanzania wakiwamo wanasiasa wa upinzani.

Kubwa kilichowakera Watanzania hata kuchoshwa na muundo wa wanasiasa wa upinzani, ni tabia ya kukosoakosoa hata linalohitaji kupongezwa pamoja na kasumba ya kuchunguza ‘mambo ya nyumbani’ kuyapaka matope na kisha kwenda kusimulia kwa ‘majirani’ familia za nje ambazo nazo zina mambo yao yanazishinda.

Mfano wa hao, Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo, Kabwe Zitto ambaye kwake, kupongeza jambo zuri ni ‘mwiko na jinai.”

Sijui kakulia katika jamii ya namna gani sambamba na mzee Freeman Mbowe! Ukiona kiongozi wa chama, tena Mtanzania, anakimbia kwenda kwa Wazungu kuishitaki Tanzania ili ikwamishwe mambo yake kama anavyofanya mara kwa mara Zitto Kabwe, ni vigumu kutofautisha mtu huyo na mchawi maana mchawi siyo lazima awe anayetumia ushirikina na tunguli, bali tabia isiyo njema katika jamii nayo ni uchawi. Wengine ndiyo hao wa ‘ukoo’ mmoja wanazidi ‘kujiteka’ kila kukicha ili kutafuta huruma ya Wazungu kwa chama chao.

Ndiyo maana ninasema, wapo wengine, lakini Mwenyekiti wa chama cha siasa cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia, amekuwa mfano wa kuigwa na wapinzani kutokana na namna ambavyo mara nyingi, anaendesha siasa za upinzani; ‘siasa za ushindani wa hoja na ndiyo maana mara nyingi anasema: “Hoja kwa kielelezo.”

Siyo kwamba ninamfagilia, lakini ninauona ukweli kuwa hata katika michango yake, penye kukosoa, Mbatia anakosoa kiustaraabu na kuonesha njia mbadala wakati akina Freeman Mbowe; Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Kabwe Zitto, wao ni kukosoa na kutukana au kuzusha.

Hawana tofauti na mwanafunzi ambaye badala ya kusikiliza anachofundisha mwalimu ili aelewe, anasikiliza ili aulize swali ili kufurahisha wenzake matokeo yake, siku zote anaishia maswali, lakini hakuna tija anayoipata yeye na jamaa yake. Kilichonisukuma leo kumkumbuka Mbatia, ni namna anavyosisitiza suala la amani na haki wakati akizungumza na watia nia wa NCCR-Mageuzi wapatao 113 aliposisitiza haki kutendeka kwa watu na pande zote.

Hili ni njambo la msingi kabisa ndiyo maana hata Rais John Magufuli kila mara anasisitiza kuwa, Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2020 utakuwa huru, haki na utafanyika kwa amani na usalama.

Katika mkutano huo jijini Dodoma, Mbatia ambaye amemaliza muda wake wa ubunge jimboni Vunjo katika Mkoa wa Kilimanjaro, anavigeukia vyama vya upinzani na kuvitaka kuingia katika kinyang’anyiro cha Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020 vikiwa na ajenda ya kushindana kwa hoja si kwa propaganda, matusi, kashfa na uzushi usio na tija kwa umma.

Hili ni jambo la kupongeza linaloonesha kuwa hata upinzani, wapo wanasiasa wachache wenye moyo wa uzalendo kwa taifa maana wapo watu wenye mawazo ya kijamaa katika nchi za kibepari.

Anasema: “Niombe sana vyama vishindane kwa hoja siyo propaganda za kuchafuana; hakuna siasa za kumtoa mtu ngeu wala propaganda…” Anakataa hoja ya chama fulani cha upinzani kinachopenda kujaribu kuendesha vyama vingine akisema:

“Hakuna chama ambacho ni kiranja wa mwenzake; hapa kwetu ndipo kuna mageuzi ya kweli na tunamtanguliza Mungu.” Kuhusu suala la ukabila, Mbatia anasema: “Kuna minong’ono ya ukabila.

Hili kwetu halipo… Chama kimoja chenye nguvu nchini, kimekuwa kikilaumiwa kwa kuendekeza udhalilishaji wa kijinsia ili kupata nafasi mbalimbali zikiwamo za uteuzi na kuendekeza ukabila na umajimbo. Suala hilo, ni moja ya mambo yaliyowafanya Watanzania kukerwa na chama hicho na uongozi wake. Mei Mosi, 1995 wakati akizungumza na wafanyakazi mjini Mbeya, Baba wa Taifa Mwalimu Julius K. Nyerere, alitaja ukabila kama moja ya nyufa zinazoitafuna Tanzania sambamba na sumu ya udini na rushwa.

Nyerere alionesha kusikitishwa na tabia ya baadhi ya Watanzania kuanza kuonesha ugonjwa wa kutaka kutambuana kwa ukabila.

Kwamba, eti hata kama mtu hana sifa, hana uwezo na hakubaliki, lakini mtu anasisitiza kuwa atamchagua kwa kuwa tu, ni wa kabila lake.

Kwa upande mwingine, akashangaa akisema ugonjwa wa ukabila unaweza kumnyima nafasi mtu mwadilifu, mchapakazi na mpenda watu jambo ambalo siyo zuri.

Kinachofanya Watanzania wengi kuwapenda Mbatia na Mwenyekiti wa chama cha TLP, Augustine Mrema tofauti na wanasiasa wengine wa upinzani, ni utayari wao kupongeza wazi waziwazi jambo zuri waziwazi na kuliunga mkono hata kama limefanywa na chama tawala (CCM) mradi lina maslahi kwa umma.

Ni kwa msingi huo, kwa mamlaka ya rais kupitia Ibara 66(1)(c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, Mei 2012, Rais Jakaya Kikwete (Mstaafu wa Awamu ya Nne), alimteua Mbatia kuwa Mbunge.

Kimsingi, Tanzania inataka wanasiasa waliouvaa utanzania na siyo wanasiasa wanaojiita Watanzania japo kweli ni Watanzania, lakini wanachumia tumbo kwa kukosoa kila kitu hata chenye manufaa kwa umma ili waonewe huruma au kupongezwa na mabeberu wanaotaka tuwe watumwa wao siku zote. Wanasiasa kama hao, ni wazi wanatuuza utumwani ndiyo maana hawapaswi kupewa nafasi na ninasema:

“Kwa rangi hii ya Mbatia, upinzani una nafuu kidogo maana maana waungwana kama Mbatia na Mrema ni wachache.”

FIGO ambayo jukumu lake kubwa ni kuchuja damu na kutoa ...

foto
Mwandishi: Joseph Sabinus

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi