loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Ridhiwani Kikwete anavyopambana Chalinze

MWAKA 1995 Serikali ilitangaza jimbo jipya la uchaguzi la Chalinze lenye kata 15 katika Wilaya ya Bagamoyo, Mkoa wa Pwani.

Katika miaka 25, wananchi wameshuhudia maendeleo makubwa lakini mbunge wa Chalinze aliyemaliza awamu yake ya pili, Ridhiwani Kikwete (CCM) anasema bado ziko changamoto za maendeleo ya jamii, afya, elimu, kilimo, mifugo na masoko, nishati na maji.

Ridhiwani kwa niaba ya madiwani kutoka Kata za Halmashauri ya Chalinze anasema kwa kutambua changamoto hizo, yeye na madiwani walifanya kazi usiku na mchana. Anasema, kuna upungufu wa nyumba za wauguzi na mazingira magumu ya ufanyaji kazi, sekta ya elimu, uhaba wa madarasa, nyumba za walimu, mabweni ya wanafunzi wa sekondari, na mazingira magumu ya watoto wa kike.

Kuhusu Utawala Bora, Ridhiwani anasema kukosekana kwa ofisi za Serikali katika baadhi ya vijiji, kata na makao makuu ya Halmashauri na ofisi ya mbunge ilikuwa changamoto pia.

Nyingine ni kukosa mawasiliano ya barabara zinazounganisha vijiji na makao makuu ya kata na minara ya mawasiliano ya simu kulikonyima mawasiliano baadhi ya maeneo pamoja na hali mbaya ya kiuchumi iliyokwamisha ustawi wa jamii. Nyingine anasema ni umeme kwa viwanda na masoko, ukosefu wa stendi na soko la kisasa Chalinze, viwanja vya michezo na usalama wa raia.

Ridhiwani anasema, Ilani ya CCM 2015-2020, ilielekeza vijiji viunganishwe na makao makuu ya kata zao, kumwondolea Mtanzania umaskini na kujenga uchumi shirikishi. Ilani pia ilitaka zahanati kwa kila kijiji na vituo vya afya katika kila kata huku kila halmashauri ikielekezwa kuwa na hospitali ya Wilaya.

Kwa upande wa elimu, anasema ni kuhakikisha mfumo wa elimu unawawezesha watoto wote wa kitanzania kwenda shule na elimu iwe bure na Serikali kuwezesha upatikanaji wa elimu hiyo na ujenzi wa miundombinu; majengo ya madarasa na nyumba za walimu kama kwenye eneo la afya.

Kuhakikisha dhamira inafanikiwa, Ridhiwani anasema, alishirikiana na madiwani na wananchi wa Chalinze kutekeleza mambo hayo. Mafanikio Anasema, katika miaka hii mitano, wamepata mafanikio mengi yakiwemo kutatua shida ya maji, ujenzi wa zahanati na vituo vya afya na kutoa vifaa tiba, ujenzi wa shule za msingi na sekondari na mabweni kwa wanafunzi wa kike.

Anasema, barabara zilikarabatiwa, mpya nyingi kufunguliwa. Katika kilimo anasema kampeni ya kupanda zao la korosho kwa kugawa miche maeneo muhimu kama shule, vijiji na zao la muhogo vimeshamiri na wananchi wanafaidika.

Anasema, kilimo cha umwagiliaji kimeonesha mafanikio makubwa katika kata za Vigwaza, Msata na Kiwangwa na katika ufugaji halmashauri imeneemeka na ufugaji kupitia mpango mpya wa serikali na uwekezaji ranchi (NARCO) kwa kugawiwa maeneo mapya na vijiji kunufaika kwa kupewa maeneo kata Vigwaza; Fukayosi.

Mbunge huyo anasema, katika ufugaji, wamepiga chapa mifugo, ujenzi wa malambo ya kunyweshea mifugo yetu, kugawa chanjo na dawa kwa mifugo na kupiga chapa mifugo katika kata na utatuzi wa migogoro ya wakulima na wafugaji.

Kwa maendeleo ya jamii, anasema, Chalinze pia wamefungua milango ya fursa za fedha za mikopo ya wanawake, vijana na walemavu. Ridhiwani anawashukuru viongozi wa CCM wa mashina hadi Taifa kwa ushirikiano mkubwa waliompa katika kipindi cha kwanza cha miaka mitano ya kwanza ya uongozi wa awamu hii na kusema ana nia kuendelea kuomba ubunge tena.

Anasema, uongozi haukuwa rahisi kwake lakini kwa usimamizi wao, walimsaidia kutekeleza mazuri hayo yote. Anasema CCM ilimwamini akiwa kijana mdogo kurithi nafasi ya aliyekuwa Mbunge Saidi Bwanamdogo aliyefariki dunia.

Anamshukuru Rais John Magufuli kwa msaada na uongozi thabiti. Anawashukuru pia wazazi wake, Rais mstaafu wa awamu ya nne, Dk Jakaya Kikwete na Mama Salma Kikwete.

Anawashukuru pia madiwani kwa ushirikiano katika kazi, wasaidizi wake, watendaji wote wa Halmashauri ya Chalinze, ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri yao hadi vitongoji na mitaa ya mamlaka ya mji mdogo wa Chalinze, mkoani Pwani. Anasema, Jimbo la Uchaguzi la Chalinze ni moja ya majimbo mawili ya uchaguzi Wilaya ya Bagamoyo lingine likiwa Bagamoyo.

Anaorodhesha mafanikio zaidi kuwa ni ukarabati wa nyumba ya mwalimu Shule ya Msingi ya Hondogo uliofanywa kwa Sh milioni 11 kutoka Halmashauri ya Chalinze na ujenzi wa matundu saba ya choo katika Shule ya Msingi Kilemera kwa Sh 4,972,000 za halmashauri. Mengine ni ukarabati chumba cha darasa Shule ya Msingi ya Kilemera kwa Sh milioni tatu. Katika sekondari, anasema kata ya Mandera ina shule mbili za Serikali.

Mwaka 2014/15 ilikuwa shule moja tu ya Serikali ya wasichana na ya kitaifa. Katika kukabiliana na changamoto ya vijana ya kusoma kutoka mbali, mbunge anasema alisimamia ujenzi wa shule mpya Rupungwi iliyo katika hatua ya ujenzi.

Kutokana na juhudi za mbunge, kuna mwamko na ongezeko la ufaulu kufuatia ongezeko la madarasa, wanafunzi na nyumba za walimu. Utengenezaji meza na viti katika Sekondari Mandera umekamilika kutokana na Sh 6,000,000 za halmashauri.

Lingine linalofanyika anasema ujenzi wa sekondari Rupungwi unafanywa na wananchi na mhisani kwa Sh 6,728,500 na kwamba madawati 90 yamekamilika kwa Sh milioni 2.2. Pia anasema kuna ujenzi wa tangi la lita 100,000 za maji shuleni hapo kusaidia wanafunzi linalogharomu sh milioni 50.

Changamoto za elimu Kata ya Mandera anasema ni uhaba wa vyumba vya madarasa, mabweni na ukosefu wa nyumba za walimu na maabara. Kuhusu maji, Ridhiwani anasema, Serikali, Halmashauri ya Chalinze na Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Chalinze (CHALIWASA), wamewezesha upatikanaji wa maji Mandera.

Anasema, kumejengwa tangi la lita 100,000 Shule ya Sekondari Mandera kwa Sh milioni 50 za halmashauri na vioski saba kijiji cha Mandera kwa Sh milioni 92 za serikali. Ujenzi wa vioski vipya vitano kijiji cha Kibaoni na vitongoji vya umasaini vya Chatanga na Mnazi Mmoja unaogharamiwa na Serikali Kuu. Katika sekta ya kilimo Ridhiwani anasema Kata ya Mandera inaongoza kilimo na maendeleo makubwa yamefanyika kwa wananchi kutumia zana za kisasa.

Kwa upande wa miundombinu na nishati anasema wakati wanaingia madarakani mwaka 2014/15 barabara za kata ya Mandera nyingi zilikuwa hazipitiki kuunganisha vijiji na makao ya kata lakini sasa mambo ni mazuri.

Anasema mbunge, madiwani na viongozi wa serikali za vijiji kwa kushirikiana na Wakala wa Barabara (Tanroads) wamefanikiwa kuzifungua barabara zote zinazounganisha vijiji na makao makuu ya kata na vitongoji vyake.

Pia barabara za kata zimekarabatiwa na kwamba kupitia vikao, viongozi hao wa kata wakishirikiana na mbunge wamefanikisha kujenga madaraja ya kitongoji cha Mchikichini, Mandera kwenda Miono kwash 147,885,000 zilizotoka kutoka Serikali Kuu. Anasema barabara zinazounganisha kata na vijiji zinapitika muda wote isipokuwa kutokana na hali ya mabadiliko na mvua.

Kwa kushirikiana na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) anasema mipango ya marekebisho ya barabara za kata imefanyika. Kwa upande wa miundo mbinu ya mawasiliano anasema kata ya Kiwangwa inaendelea kupata mawasiliano ya Vodacom, Tigo, TTCL, Airtel na wananchi wanafurahia huduma. Kuhusu umeme, Ridhiwani anasema vijiji vyote vya Kata ya Mandera vimefikiwa kupata umeme unaosambazwa na Wakala wa Umeme Vijijini (REA).

Anasema ofisi ya mbunge na Halmashauri ya Chalinze wamesimamia mifuko ya kuwezesha akina mama (Women Development Fund -WDF) na kusaidia Vijana, Youth Development Fund (YDF) na Walemavu (People with Disability Development Fund- DDF) ambapo vikundi 22 vya akinamama na vijana vilipewa Sh milioni 75.

Anasema kupitia mfuko wa jimbo Sh milioni tatu zilitolewa ili kujenga mfumo wa maji katika Zahanati ya Kiwangwa. Matarajio anasema ni kuimarisha zahanati hii kuwa kituo cha afya.

Kuhusu ujenzi anasema yeye kama mbunge amekuwa akitoa michango mbalimbali kuhakikisha kazi za chama zinakwenda vizuri sio tu katika ngazi ya wilaya, lakini pia katika kata na matawi sambamba na kusaidia jumuiya za chama

FIGO ambayo jukumu lake kubwa ni kuchuja damu na kutoa ...

foto
Mwandishi: Godfrey Lutego

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi