loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Serikali kuachana na nguzo za miti za umeme

SERIKALI itaachana na matumizi ya nguzo za umeme zitokanazo na miti na badala yake itatumia nguzo za zege ili kuepukana na uharibifu wa nguzo kuoza na kusababisha tatizo la ukatikaji wa umeme.

Hayo yamesemwa wilayani Rufiji mkoani Pwani na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu wakati alipotembelea kuona nguzo za zege 250 kutumika baadhi ya maeneo yaliyokumbwa na mafuriko kwenye wilaya hiyo kupitia miradi ya Wakala wa Umeme Vijijini (REA) kwenye wilaya za Rufiji na Kibiti.

Mgalu amesema mradi wa kuweka nguzo za zege umeanza kwa baadhi ya maeneo na mradi wa Kibaha na kwenye Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere na huo ni mpango kwa nchi nzima.

“Tumeanza kutumia nguzo za zege kwa ajili ya kusambaza umeme kwa miradi mbalimbali ambapo sehemu nyingine ni Muhoro ambako palikumbwa na mafuriko na kusababisha umeme kukosekana kwa zaidi ya mwezi hivyo ili kumaliza tatizo la umeme kukatika ni kuwa na nguzo za zege,” amesema Mgalu.

Amesema kwa Wilaya ya Rufiji watabadilisha kipande cha Daraja la Mkapa hadi Muhoro sehemu yenye matatizo ya mafuriko na kusababisha tatizo la umeme kukatika lakin nguzo za zege itakuwa suluhisho.

“Ukatikaji wa umeme hutokana na nguzo hizi za miti kuoza na kuanguka au pale yanapotokea mafuriko umeme hukatika hivyo kwa kutumia nguzo za zege ni suluhisho la ukatikaji wa umeme,” amesema Mgalu.

Aidha, amesema sasa vijiji ambavyo havina umeme Pwani ni 89 ambavyo vimewekwa REA awamu ya tatu mzunguko wa pili ambao kwa sasa uko kwenye mchakato wa kutangaza tenda kwa wakandarasi.

“Kwenye awamu hii ya tatu mzunguko wa pili wa utekelezaji mradi huo utakuwa ni wa miezi 12 ambapo tutaboresha utoaji kandarasi kwa kutowarundikia kazi nyingi kama ilivyo sasa kwa wakandarasi kuwa na mkoa zaidi ya mmoja ambapo lengo ni kutaka wakamilishe kazi kwa wakati,” amesema Mgalu.

Amesema matarajio ni kuhakikisha mwakani vijiji vyote vina umeme, ambao Pwani miaka mitano iliyopita vijiji vilivyokuwa na umeme ni 79, lakini kwa sasa vijiji 342 vina umeme, Sh bilioni 138 zikitolewa. Mbunge wa Jimbo la Kibiti, Ally Ungando alisema vijiji 41 vina umeme na vijiji 17 ndiyo vilivyobaki na hivyo viko kwenye Delta ambako wilaya hiyo ina vijiji 58.

Rais John Magufuli amemteua Dk Philemon Sengati kuwa Mkuu wa ...

foto
Mwandishi: John Gagarini, Rufiji

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi