loader
Dstv Habarileo  Mobile
Magufuli: Msichafuane

Magufuli: Msichafuane

MGOMBEA pekee wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya CCM, Dk John Magufuli amerudisha fomu ya kuwania nafasi hiyo kwa awamu ya pili, huku akiwataka wagombea mbali mbali wakiwemo wa urais Zanzibar, kuacha kuvurugana na kuchafuana, kwani kufanya hivyo watakidhoofi sha chama dhidi ya wapinzani.

Amesema ameamua kuchukua fomu licha ya kufanya mengi katika kujenga uchumi wa nchi, lakini bado miradi mingine aliyoanza haijakamilika kama reli ya kisasa, umeme wa Nyerere, umeme vijijini na miradi mingine, kwani akichukua mwingine hawezi kufanya vizuri, kama wao wanavyoweza kukamilisha.

Akirudisha fomu Makao Mkuu ya Chama jijini hapa jana, Rais Magufuli aliyedhaminiwa na wanaCCM 1,023,911, alisema wagombea wanatakiwa kuheshimiana na kutochafuana kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Alisema ameanza kuona dalili kwa wagombea urais 32 waliojiotokeza kuwania nafasi ya urais baada ya Dk Ali Mohamed Shein, kuwa wameanza kuchafuana kwenye mitandao ya kijamii na katika vyombo vya habari.

Aliwataka waache mtindo huo, kwani mwisho wa yote mshindi ni mmoja na Mungu anamjua. Rais Magufuli alisema wagombea wa urais, wanatakiwa kushindana kwa kunadi sera zao na wasiumizane kwa kupakana matope katika mitandao ya kijamii, kwani kufanya hivyo wapatawapa nafasi washindani wao. Alisema pia amesikia katika baadhi ya majimbo, wamejitokeza watia nia zaidi ya 25 hata 50.

Aliwataka wasiumizane wala kulogana bure, wasivunje umoja uliopo katika chama wa kuvumiliana na kuheshiana bila kuchafuana wakati wa kampeni, kwani watakifanya chama kupoteza mwelekeo.

“Atakayechaguliwa atakuwa amechaguliwa, wagombea wengine tunatakiwa kumbeba kwa nguvu zetu zote, kwa ajili ya kupata ushindi wa chama katika kushindana na vyama vingine,” alisema Rais Magufuli.

Rais Magufuli alisema watakaoshindwa nafasi hizo, bado kuna nafasi nyingi za uteuzi Bara na Zanzibar, hivyo kinachotakiwa ni kushikamana ili kupata ushindi kama chama ili kuendelea kushika dola.

Alivitaka vyama vyote vya siasa, CCM na vyama vya upinzani, wakati wanateua wagombea wasiwasahau wanawake, vijana na wenye ulemavu na hata wazee, kwani busara yao inatakiwa.

Alisema mara nyingi kipindi cha kampeni, kinakuwa kipindi cha kukibomoa chama, kwa kubomoana wagombea wenyewe na kuumizana. Aliomba kampeni za mwaka huu, ziwe za utulivu na ustaarabu.

Aliwatakia kila la heri wale wote wanaotia nia katika kutafuta nafasi za uwakilishi, ubunge na udiwani, kwamba wanaruhusiwa kuanza kujipitisha pitisha kuanzia Julai Mosi mwaka huu, lakini wanatakiwa kufanya kwa ustaarabu.

Alisema kuanzia leo majimbo yapo wazi kwa ajili ya kila mwenye nia ya kugombea, hivyo wagombea wa nafasi hizo za uwakilishi, ubunge na udiwani, wanaweza kuanza kujipitisha pitisha. Alisema aliamua kuchukua fomu Juni 17, mwaka huu kimya kimya, lakini katika kurudisha alibanwa ili aeleze ratiba na vijana walikuwa wakikesha wakimsubiri.

Aliwashukuru lakini alisema anasuburi uamuzi wa chama kama kitampitisha kuwa mgombea kwa muhula wa pili na wa mwisho kikatiba. Katika kutafuta wadhamini nchini, Rais wa Zanzibar, Dk Shein pia alishiriki kikamilifu kutafuta wadhamini wake licha ya wale wa mikoa ya Unguja na Pemba na amemdhamini Rais Magufuli kwa kumtafutia wadhamini 800.

Rais Magufuli amepata mafuriko ya wadhamini katika mikoa na katika jumuiya za chama. Baadhi ya wanachama wamelaumu kwa kukosa kumdhamini kutokana na fomu chache kutumwa katika mikoa yao.

Aliwaomba radhi wote waliotaka kumdhamini, lakini kutokana na uchache wa fomu wakawa wachache. Alisema azma yao ya kumpa nafasi ya kuwa rais kwa awamu ya pili, waitumie katika kupiga kura CCM ikimpa ridhaa.

Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally alisema kuanzia leo majimbo na kata zipo wazi, hivyo si wakati wa kampeni bali ni wakati wa kujipitisha pitisha. Alisema fomu zitaanza kuchukuliwa Julai 14, mwaka huu.

Dk Bashiru alisema kwa wale ambao watakiuka maadili kwa kuanza kufanya kampeni kabla ya muda uliopangwa, Makamu Mwenyekiti, Philip Mangula yupo atawashughulikia, kwani watakuwa wameenda kinyume.

Alisema wagombea wa nafasi ya urais, walipewa nafasi ya kuchukua fomu kati ya Juni 15-30, lakini wagombea wa ubunge, uwakilishi na udiwani, watachukua fomu za kugombea kati ya Julai 14 hadi 17, mwaka huu Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma, Godwini Mkanwa alisema wenyeviti wa chama hicho, wameweka azimio kuhakikisha Rais Magufuli anapata ushindi kwa asilimia 100 katika mikoa yote nchini. Tofauti na uchaguzi wa 2015 ambao wagombea 42 walijitokeza, katika uchaguzi huu wanaCCM wamempa heshima Rais Magufuli kuwa mgombea pekee.

Lakini, Mkutano Mkuu utakaofanyika Julai 11, ndiyo utakaopitisha jina lake kugombea wa chama hicho, ili kushindana na wagombea wengine kutoka vyama vya upinzani. Katika kupata wagombea wa urais, Halmashauri Kuu ya Taifa itakutana jijini Dodoma kupitisha jina la mgombea urais wa Zanzibar Julai 10 na Julai 11 Mkutano Mkuu utapitisha jina la mgombea urais wa Muungano.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/0cd8584e078f4b309e00af148a3d122e.jpg

ALIYEKUWA Mbunge Mteule wa Jimbo la Konde ...

foto
Mwandishi: Magnus Mahenge, Dodoma

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi