loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Bei ya petroli, dizeli yapanda

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetangaza bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli zinazoanza kutumika kuanzia leo, huku zikionesha kupanda kwa kati ya Sh 169 hadi Sh 173 kwa lita moja.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ewura iliyotolewa jana, bei hizo zinatokana na mabadiliko ya bei za mafuta katika soko la ndani, mabadiliko ya bei za mafuta katika soko la dunia na gharama za usafirishaji. Katika bei hizo, petroli kwa Dar es Salaam itakuwa Sh 1,693 kwa lita na dizeli Sh 1,716.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Godfrey Chibulunje, hakuna shehena ya mafuta iliyopokelewa kupitia Bandari ya Mtwara mwezi uliomalizika jana, Juni.

Hivyo, kwa mwezi Julai 2020, bei za jumla na rejareja kwa mafuta ya dizeli kwa mikoa ya Kusini yaani Mtwara, Lindi na Ruvuma hazitabadilika, ikilinganishwa na toleo lililopita la Juni 3, mwaka huu.

Chibulunje alisema kutokana na upungufu wa mafuta ya petroli katika maghala ya mafuta mkoani Mtwara, wamiliki wa vituo vya mafuta katika mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma, wanashauriwa kununua mafuta hayo kutoka Dar es Salaam.

Hata hivyo, bei za rejareja za petroli kwa mikoa hiyo zinatokana na gharama za mafuta hayo kutoka Dar es salaam pamoja na gharama za usafirishaji wa mafuta hayo hadi mikoa husika.

Aidha, alisema kwa kuwa hakuna mafuta ya taa katika Bandari ya Mtwara, wamiliki wa vituo vya mafuta katika mikoa tajwa wanashauriwa kununua mafuta hayo kutoka Dar es Salaam na hivyo bei za rejareja za bidhaa hiyo, zinatokana na gharama za mafuta hayo kutoka Dar es Salaam na kusafirishwa hadi mkoa husika.

Akifafanua, Chibulunje alisema bei za jumla na rejareja za mafuta ya petroli na dizeli yaliyopokelewa nchini kupitia Bandari ya Dar es Salaam zimeongezeka, ikilinganishwa na toleo lililopita la Juni 3, mwaka huu.

Aidha, alisema bei za mafuta ya taa zitaendelea kuwa zile zilizotangazwa katika toleo lililopita la Juni, kwa sababu hakukuwepo na shehena ya mafuta hayo iliyopokelewa mwezi uliopita kupitia Bandari ya Dar es Salaam.

“Kwa mwezi Julai 2020, bei za rejareja za petroli na dizeli zimeongezeka kwa Shilingi 173/lita (sawa na asilimia 11.38) na Shilingi 170/lita (sawa na asilimia 10.98) vilevile, ikilinganishwa na toleo la mwezi uliopita, bei za jumla za petroli na dizeli zimeongezeka kwa Shilingi 172.39/lita (sawa na asilimia 12.35) na Shilingi 169.22/lita,” alisema Chibulunje.

Alisema bei kikomo za mafuta kwa eneo husika, zinapatikana pia kupitia simu za mkononi kwa kupiga namba *152*00# na kisha kufuata maelekezo, ikiwa ni huduma ya bure katika mitandao yote ya simu za mkononi nchini. Aidha, alisema kwa mujibu wa Sheria ya Mafuta ya Mwaka 2015, bei za bidhaa za mafuta ya petroli zitaendelea kupangwa na soko.

Rais John Magufuli amemteua Dk Philemon Sengati kuwa Mkuu wa ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi