loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

JPM awaonya viongozi Kilosa migogoro ardhi

RAIS John Magufuli amewaonya kwa mara nyingine viongozi wa Wilaya ya Kilosa, kwa kutoshughulikia ipasavyo kero mbali mbali za wananchi hususani migogoro ya ardhi, akiwemo Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, kwa kuidhinisha kuuza shamba kubwa kwa mwekezaji mmoja, ilihali wananchi wanakosa mahali pa kulima.

Rais aliwaonya viongozi hao juzi, alipowasalimu wananchi wa Kijiji cha Ilonga wilayani humo akiwa njiani kutoka Mkadage. Wananchi hao walilalamikia kitendo cha Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo, Asajile Mwambambale kuidhinisha mwekezaji, Swai Frank Palilo aachiwe shamba lenye ukubwa wa ekari 1,200.

Alimuidhinishia mwekezaji huyo aachiwe shamba hilo hata kabla Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi hajatoa uamuzi baada ya timu aliyounda kushughulikia mgogoro wa shamba hilo, kuwasilisha ripoti ya uchunguzi kwake.

Kutokana na sakata hilo, Mwambambale aliwaomba radhi wananchi wa Kijiji cha Ilonga na Rais Magufuli, kwa kuidhinisha shamba kubwa kwa mwekezaji mmoja, ilihali wananchi wanakosa mahali pa kulima.

Alipoulizwa na Rais kwa nini alifanya kazi ambazo hazimhusu, mkurugenzi mtendaji huyo alijitetea na kumwomba radhi Rais na wananchi hao wa Ilonga.

“Mheshimiwa Rais naomba unisamehe kwa kosa nililofanya…Mheshimiwa Rais nilidhani natekeleza majukumu kumbe nimejikwaa, Mheshimiwa Rais naomba unisamehe,” Mwambambale aliomba radhi kwa Rais Magufuli.

Kutokana na kuomba radhi kwake mbele yake, Rais alimpa maelekezo ya kuandika katika barua yake hiyo kwa maandishi. Rais Magufuli alimwambia “Andika hapo kwamba nimewakosea wananchi wa Ilonga kwa kufanya kazi ambayo sina mamlaka nayo…wananchi wa Ilonga mnisamehe na Mungu anisamehe.”

Rais Magufuli alisema kilio cha wananchi kimesikilizwa, na kuwa Lukuvi ataleta ripoti yake wiki moja au mbili na atawafikishia majibu akiambatana na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Loata ole Sanare na kiongozi wao wananchi.

“Na haya yote aliyoliyofanya mkurugenzi yamefutika na kwamba ninyi mpaka leo mpo kama mlipokuwa zamani mpaka tatizo hili litakapoletwa kwangu,” alisema Rais Magufuli.

Kabla ya kuzungumza na wananchi wa Ilonga eneo la Mkadage, alibainisha kwa kusema, “Nimeambiwa hata Mkurugenzi wa hapa Kilosa ana matatizo…ajirekebishe, siwezi kumtumbua mbele ya Askofu...DC wa Kilosa naye ajirekebishe hivyo hivyo, taarifa zao ninazo za kutosha.”

Aidha, Rais Magufuli aliiagiza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, kuanza maandalizi ya ujenzi wa barabara ya lami ya Kilosa – Mikumi yenye urefu wa kilometa 70 na barabara ya Ifakara – Malinyi – Londo, inayounganisha na Wilaya ya Namtumbo Mkoa wa Ruvuma.

MWITO umetolewa kwa wakulima kwenye mikoa yanayozalisha chakula kwa wingi ...

foto
Mwandishi: John Nditi, Morogoro

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi