loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mageuzi makubwa sekta ya maji

MAGEUZI makubwa yamefanyika katika sekta ya maji katika kipindi cha miaka mitano tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani, yakiwemo ya kutoa maji katika maeneo yenye maji mengi na kuyapeleka kwa yenye upungufu.

Zaidi ya Sh trilioni tatu zimetolewa kutekeleza miradi ya maji tangu Rais John Magufuli aingie madarakani mwaka 2015 na kufanikisha ongezeko la upatikanaji wa maji safi na salama vijijini na mijini. Chini ya mageuzi hayo, upatikanaji wa maji safi na salama vijijini umefikia asilimia 70.1 mwaka huu kutoka asilimia 43 mwaka 2015.

Kwa mijini, upatikanaji umetoa asilimia 74 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 84 mwaka huu. Mafanikio haya ni majawabu ya malalamiko ya ukosefu wa maji, ambayo Rais Magufuli kupitia hotuba yake ya kuzindua Bunge, Novemba 20, 2015, alikiri kuyapokea wakati wa kampeni za uchaguzi.

Katika hotuba hiyo, pamoja na masuala mengine, Rais Magufuli aliahidi serikali itahakikisha inaongeza kiwango cha upatikanaji wa maji kufikia asilimia 85 kwa vijijini na asilimia 96 kwa maeneo ya mjini ifikapo mwaka 2020.

Aliahidi kukamilisha miradi iliyokwishaanza na kuanzisha mingine mikubwa na midogo kutoka katika mito, maziwa na vyanzo vingine mbali mbali ikiwa ni pamoja na kuvuna maji ya mvua; jambo ambalo linaendelea kutekelezwa kama ambavyo taarifa za serikali zinaonesha.

Akihutubia wakati wa kufunga Bunge hivi karibuni, Rais Magufuli licha ya kubainisha ongezeko la upatikanaji wa maji safi na salama vijijini, alisema serikali imetekeleza miradi 1,423 ambayo kati yake, 1,268 ni ya vijijini na 155 ni mjini. Miongoni mwa miradi mikubwa inayoendelea kutekelezwa ni wa kutoa maji Ziwa Victoria kwenda Nzega, Tabora na Igunga.

Mradi wa Mji wa Arusha na wa kupeleka maji kwenye miji 28, pia unatekelezwa kwa gharama ya Sh trilioni 1.2.

Kuzinduliwa hivi karibuni kwa mradi mkubwa wa maji wilayani Kisarawe mkoani Pwani uliotumia Sh bilioni 10.6, ni sehemu ya miradi inayodhihirisha hatua za serikali za kumaliza kabisa kero ya maji katika maeneo mbali mbali nchini kwa kutumia fedha za ndani.

Kwa mujibu wa Rais Magufuli, zaidi ya Sh trilioni tatu zimetolewa kutekeleza miradi mbalimbali ya maji tangu aingie madarakani mwaka 2015 na kufanya upatikanaji wa maji safi na salama vijijini kufikia asilimia 70.1 mwaka huu kutoka asilimia 43 mwaka 2015 na mijini kwa kipindi hicho hicho kufikia asilimia 84 kutoka asilimia 74.

Waziri wa Maji, Profesa Makame Mnyaa Mbarawa aliliambia gazeti hili kwamba mageuzi yamedhihirisha kwa takwimu na matokeo ya miradi ya maji inayohudumia wananchi.

Mageuzi hayo chini ya uongozi wa Rais Magufuli, pia yanaonekana kupitia juhudi za kutoa maji katika maeneo yenye maji mengi, kupeleka katika maeneo yenye upungufu wa maji.

MWITO umetolewa kwa wakulima kwenye mikoa yanayozalisha chakula kwa wingi ...

foto
Mwandishi: Stella Nyemenohi

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi