loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Maji Ziwa Victoria kupelekwa Dodoma

SERIKALI inatarajia kuanza upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa mradi mkubwa wa kutoa maji Ziwa Victoria kwenda Dodoma kupitia Singida. aarifa hiyo imo kwenye hotuba ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyotoa Aprili mwaka huu bungeni kuhusu mapitio na mwelekeo wa kazi za serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za ofisi yake na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2020/21.

“Serikali pia itakamilisha miradi inayoendelea kuanza miradi mipya ya maji na kuanza upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa mradi wa kutoa maji Ziwa Victoria kupeleka Singida hadi Dodoma,” alisema Majaliwa.

Kwa mujibu wa Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa, matokeo ya utafiti na upembuzi wa awali kuhusu mradi huo wa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda Dodoma kupitia Singida, yanaonesha kuwa mradi unawezekana.

Profesa Mbarawa aliliambia gazeti hili kuwa mradi utakuwa na manufaa makubwa, kwa kuwezesha kupatikana kwa huduma endelevu ya maji katika miji ya Dodoma na Singida na hivyo kukabiliana na hali ya ukame katika mikoa hiyo.

“Ningependa kueleza kuwa utafiti huu ni sehemu ya utekelezaji wa mfumo wa Gridi ya Taifa ya Maji ambayo wizara imeanzisha,” alisema Profesa Mbarawa ambaye chini yake, kumekuwa na mabadiliko makubwa katika sekta ya maji, ikiwamo kuwabana makandarasi wa hovyo na miradi mingi kutekelezwa na kuzaa matunda.

Alifafanua kwamba Mfumo wa Taifa wa Usambazaji Maji, unalenga kuhakikisha maji yanapatikana kwenye maeneo yote nchini na katika kipindi chote cha mwaka, bila kujali iwapo eneo husika lina vyanzo vya maji au lina uhaba wa maji.

Kupitia mfumo huo, unafanyika ujenzi wa mtandao wa kusafirisha maji kutoka maeneo yenye maji mengi na kuyapeleka kwenye maeneo yenye uhaba wa maji, kama itakayofanyika kutoa maji Ziwa Victoria kwenda Dodoma.

Wakati huo huo ipo Programu ya Matumizi ya Maji ya Maziwa Makuu, itakayohusisha kuboresha huduma ya maji katika vijiji vilivyopo kando ya maziwa makuu; Tanganyika, Nyasa na Victoria kwa lengo la kuwapatia wananchi huduma ya majisafi.

Kwa kuzingatia makadirio ya idadi ya watu milioni 54 katika mwaka 2018, kiasi cha maji kilichopo kwa kila mtu kwa mwaka ni takribani wastani wa mita za ujazo 2,300. Taarifa ya wizara inasema kiasi hicho ni juu ya wastani wa mita za ujazo 1,700 ambacho ni kiwango cha chini cha mahitaji ya maji kwa mtu kwa mwaka kinachokubalika kimataifa.

Chini ya kiwango hicho nchi huhesabika kuwa na uhaba wa maji. Alipowasilisha hotuba yake bungeni, Waziri Mbarawa alisema kwa kuzingatia miradi ya maji 631 inayoendelea kutekelezwa nchini, serikali ina matumaini makubwa kuwa malengo ya kitaifa katika sekta ya maji yanafikiwa ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.

Wagombea kutoka vyama vya ...

foto
Mwandishi: Stella Nyemenohi

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi