loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

JPM- Huu ni ushindi mkubwa

RAIS John Magufuli amewapongeza Watanzania katika mafanikio, yaliyowezesha Benki ya Dunia kuitangaza Tanzania kuingia rasmi nchi za Uchumi wa Kati.

Rais alisema hayo katika akaunti yake ya Twitter jana, baada ya Benki ya Dunia kuitangaza Tanzania kuwa kuanzia Julai moja mwaka huu imeingia Uchumi wa Kati.

“Nawapongeza Watanzania wenzangu kwa mafanikio haya. Huu ni ushindi mkubwa na kazi kubwa tumeifanya, tulipanga kuingia Uchumi wa Kati ifikapo 2025, lakini tumefanikiwa 2020. Mungu Ibariki Tanzania” alisema Rais Magufuli.

Awali, akizungumzia hatua hiyo jana, Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbasi alisema uamuzi huo wa Benki ya Dunia, umedhihirisha kuwa ndani ya kipindi cha miaka mitano, Serikali ya Awamu ya Tano imetekeleza kikamilifu falsafa ya ‘Hapa Kazi Tu’.

“Hii ni miaka mitano kabla ya lengo la Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025. Asanteni sana wote,” alisema Dk Abbasi.

Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025, ambayo ilianzwa kutekelezwa mwaka 2000, imelenga kuongoza harakati za maendeleo ya uchumi na jamii, zitakazoliwezesha taifa hili ifikapo mwaka 2025 kuwa taifa la Uchumi wa Kati, likitegemea zaidi pato lake kutoka katika uchumi wa viwanda.

Dira hiyo ina vipengele vitano, ambavyo ni Kuboresha maisha ya watanzania; Kuwepo kwa mazingira ya amani,usalama na umoja; Kujenga utawala bora; Kuwepo na jamii inayoelimika vyema na inayojifunza; na Kujenga uchumi imara, unaoweza kukabiliana na ushindani kutoka nchi nyingine.

Ili kutimiza malengo hayo, serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kuboresha viashiria muhimu vya uchumi, kama vile kuchochea ukuaji wa pato la taifa, kushusha mfumko wa bei, kuwavutia wawekezaji kutoka nje, kupunguza ukosefu wa ajira na kuendeleza sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii.

Kwa mujibu wa Dk Abbasi ambaye pia Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Benki ya Dunia imeingiza Tanzania katika orodha ya nchi zenye kipato cha kati kutoka dola za Marekani 1,036 hadi dola 4,045.

Mbali na vigezo vingi vinavyoiweka nchi katika Uchumi wa Kati, yapo pia maboresho ya miundombinu, ambayo yanamfaidisha mwananchi wa kawaida, mfanyabiashara mdogo, wa kati na mkubwa, wakulima na wafugaji. Hii ni pamoja na kuwawezesha wananchi, kusafirisha mazao yao kutoka sehemu yao hadi kwenye soko.

Kuwepo kwa barabara zenye kiwango cha lami ambazo zinaunganisha mikoa ni moja kigezo, ambacho kinamwezesha mkulima na mfugaji, kusafirisha kwa urahisi mazao yake hadi sokoni.

Pia kuwepo na umeme wa uhakika usiokatikatika, unamwezesha mfanyabiashara mdogo, wa kati na mkubwa, kufanya biashara yake ambayo hatimaye inampa kipato.

Kwa Tanzania katika Serikali ya Awamu ya Tano, jambo hili la kukatika ovyo kwa umeme limedhibitiwa, kiasi cha kuwafanya wafanyabiashara wa aina zote, kufanya biashara katika mazingira wezeshi.

Pia kuwepo kwa umeme kwa kila kaya kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), kumewezesha Watanzania wengi kuwa na umeme wa uhakika majumbani katika kipindi hiki cha Serikali ya Awamu ya Tano.

Elimu bila Malipo ni kigezo kingine ambacho kinaondoa ujinga kwa walio wengi, hivyo kuifanya nchi kuwa na taifa linaloweza kufanya maamuzi sahihi kwa wakati wote.

Kwa sasa Serikali ya Tanzania inatoa elimu bila malipo kwa shule za awali, msingi na sekondari, imefanya ukarabati mkubwa wa shule nyingi kongwe na kujenga nyingine nyingi mpya za msingi, sekondari na vyuo. Pia kuwepo na vituo vingi vya afya, kumewezesha wananchi wa kawaida kupata huduma kwa haraka na kwa bei nafuu.

Hatua hiyo inamwezesha mwananchi kufanya kazi akiwa na afya yake, hivyo kujiongezea kipato cha uhakika. Usafiri wa anga, majini na ardhini umeimarishwa, kiasi kwamba wafanyabiashara wa kati na wakubwa, wanaweza kusafirisha bidhaa zao bila shida, hivyo kuinua vipato vyao.

Kwa hapa Tanzania, hivyo vyote vimefanyika ndani ya miaka mitano ya uongozi wa Rais Magufuli. Nchi za Afrika pamoja na Tanzania zilizopo kwenye orodha hiyo ni Angola, Algeria, Benin, Kenya, Lesotho, Mauritania, Senegal na Tunisia.

Benki hiyo inaonesha kuwa kwa mwaka wa fedha 2021, nchi za Uchumi wa Chini zimepimwa kulingana na kipato cha mtu mmoja, kinachofikia dola za Marekani 1,135 au chini ya hapo.

Nchi zenye Uchumi wa Kati, zilipimwa kulingana na kipato cha mtu cha kiasi dola za Marekani 1,036 na dola 4,045, wakati nchi za Uchumi wa Juu zilipimwa kwa kipato kinachofikia dola za Marekani 4,046 na 12,533 na cha juu kabisa kinaanzia dola za Marekani 12,536 na zaidi.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Profesa Faustine Bee alisema jana kuwa ni bahati kubwa na si kitu kidogo, kwa Tanzania kuondoka kwenye orodha ya nchi masikini na kuwa ya Uchumi wa Kati.

Alisema vigezo vinavyozingatiwa ni wastani wa Pato kwa Kila Mtanzania, ambalo Tanzania imevuka wastani wa dola za Marekani 1,000, tofauti na awali ambapo pato hilo, lilikuwa chini ya dola hizo.

Alitaja mambo yaliyochangia pato hilo kunyanyuka kuwa ni usimamizi thabiti wa raslimali hususani madini, kutilia mkazo mapato kwenye utalii, uwekezaji katika miundombinu, ongezeko la wawekezaji wa ndani na nje na uwepo sera nzuri zinazosimamiwa vyema na serikali.

“Sera nzuri zimetufikisha kwenye lengo mapema... tumetoka kwenye nchi masikini. Ni hatua kubwa,” alisema Profesa Bee.

Dalili zilionekana Tangu mwaka jana Benki ya Dunia (WB), ilikadiria mwaka huu Tanzania kupanda daraja kutoka nchi masikini kuwa ya kipato cha kati. Julai mwaka jana Mkurugenzi Mkazi wa benki hiyo nchini Tanzania, Bella Bird alisema muda wowote kuanzia sasa Tanzania itaingia kwenye orodha ya Nchi zenye Uchumi wa Kati.

Alisema hayo wakati wa uzinduzi wa Ripoti ya 12 ya Hali ya Uchumi Tanzania kuhusu umuhimu wa rasilimali watu katika kukuza utajiri.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango akizungumza na waandishi wa habari alisema kwa uamuzi huo Tanzania inakuwa ni miongoni mwa nchi tano duniani, kuingia kwenye kundi la nchi za uchumi wa kati.

Dk Mpango alisema hatua iliyofikiwa ina manufaa mengi yakiwamo ya kuongezeka kwa wigo wa upatikanaji wa fedha za mikopo ya kibiashara kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo, kuwa na uhuru wa kupanga matumizi na kuondokana na kadhia ya utegemezi.

“ Napenda kuujulisha umma wa Watanzania baada usimamizi madhubuti wa utekelezaji wa sera zake za kupeleka maendeleo kwa wananchi, Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi mahiri wa Rais John Magufuli ameandika historia nyingine ya Tanzania kwa kuiwezesha nchi yetu kufikia azma yake ya kuwa nchi yenye uchumi wa kipato cha kati kuanzia Julai 1, mwaka huu.

“Napenda kumshukuru Rais John Magufuli kwa jitihada kubwa za kukuza uchumi wa nchi yetu ulioiwezesha Tanzania kuingia kwenye nchi za kipato cha kati miaka mitano kabla ya lengo lililowekwa kwenye Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025. Pia naona fahari kwamba historia hii imeandikwa wakati nikiwa waziri.

“ Pia nawashukuru wakulima, wavuvi, wafugaji, wafanyabiashara, wachimbaji wa madini, mabenki na wananchi wote kwa ujumla kwa michango yao katika mafanikio haya,” alisema Dk Mpango.

Imeandikwa na Bantulaki Bilango, Beda Msimbe, Abdallah Bawazir, Stella Nyemenohi, Halima Mlacha, Dar na Anna Anyimike, Dodoma.

KATIBU Tawala Mkoa wa Kagera, Profesa Faustine Kamuzora, amewaomba wamiliki ...

foto
Mwandishi: Waandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi