loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Vyama viteue wagombea wenye sifa

UCHAGUZI Mkuu wa Rais, wabunge, wawakilishi na madiwani, utafanyika Oktoba mwaka huu. Tayari vyama mbalimbali vya siasa, vimeanza mchakato wa kuteua wagombea wa nafasi hizo.

Hivyo, tunaomba vyama kuteua wagombea safi, watakaoweza kuhimili ushindani mkali kuanzia mwanzo hadi mwisho kutoka vyama vingine.

Hatutaki vyama viteue wagombea wenye mazoea ya kujitoa njiani huku wakitoa visingizio mbalimbali.

Tunataka wagombea imara, ili watakapopitishwa na vyama vyao, wakabiliane kikamilifu na wagombea wa vyama vingine pamoja na changamoto zingine za uchaguzi.

Ni vema wagombea wakumbuke kuwa kampeni za uchaguzi, huchukua muda mrefu, hivyo kinachotakiwa ni kufanya maandalizi mapema.

Tunapongeza vyombo vinavyosimamia uchaguzi huo, kwa kuanza kutoa mafunzo na semina kwa viongozi wa vyama vya siasa, ili kuwezesha uchaguzi huo kufanyika kwa haki, amani na utulivu.

Kwa mfano, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini juzi iliendesha semina kwa viongozi wakuu wa vyama 19 nchini. Lengo la semina hiyo muhimu lilikuwa kuviandaa vyama vya siasa na kuvijengea uwezo kwa ajili ya uchaguzi huo wa Oktoba.

Kwenye semina hiyo viongozi hao walifundishwa mada mbalimbali, mfano Maadili ya Viongozi wa Umma, Masuala muhimu katika Sheria ya Vyama vya Siasa na Kanuni za Usajili na Ufuatiliaji za mwaka 2019.

Tunaungana na Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Mohamed Ali Ahmed, kwa wito wake aliotoa kwa vyama vya siasa, ambapo alivitaka kujikosoa na kuhakikisha vinaingia kwenye uchaguzi mkuu bila ‘makandokando’ ya aina yoyote.

Kwamba vyama vyote vishirikiane, kuhakikisha uchaguzi huo unakuwa wa amani na utulivu. Pia, virekebishe kasoro na kuweka ushindani imara, badala ya kuwa wasindikizaji.

Tunasisitiza kuwa vyama vinatakiwa viwe imara na vijisafishe wakati vikielekea kwenye uchaguzi mkuu. Viingie kwenye uchaguzi vikiwa safi, vyenye nguvu na uwezo.

Kwa upande wa wananchi, tunaomba wafuatilie kikamilifu mchakato wa uteuzi wa wagombea wa nafasi hizo mbalimbali katika vyama vya siasa na kuwafichua wagombea wabovu, ili wasipitishwe kugombea.

Ni muhimu kuhakikisha kuwa wagombea wabovu, hawapenyi kwenye michujo ya vyama vya siasa, kwani wakipenya na kupelekwa kushindana, wanaweza kushinda hivyo kusababisha jamii kupata viongozi waovu.

foto
Mwandishi: Mhariri

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi