loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wakuu vyuo vya kilimo waagizwa kuhuisha mitaala

KATIBU Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya, amesema wakuu wa vyuo vya mafunzo ya kilimo vya serikali na binafsi wana wajibu wa kuhuisha mitaala ya mafunzo ili iendane na mahitaji ya sasa ya nchi, ambayo ni kuandaa wataalamu kuwe na uzalishaji wenye tija kulingana na uchumi wa viwanda.

Kusaya alitoa rai hiyo jana wakati alipokutana na wakuu wa vyuo vya mafunzo ya kilimo vya serikali na vyuo binafsi nchi nzima kwa lengo ni kuboresha utoaji wa mafunzo ya kilimo kwa kuzingatia Tanzania ya viwanda.

Alisema Wizara ya Kilimo ina lengo la kuongeza tija na uzalishaji katika sekta ya kilimo ili kuongeza Pato la Taifa kupitia sekta hiyo, ambalo kwa sasa ni asilimia 28, huku mchango wa sekta ndogo ya mazao ukiwa ni asilimia 16.

Alisema mchango huo unaweza ukaongezeka endapo vyuo hivyo vitazalisha wagani bora.

“Tija na uzalishaji kwenye sekta ya kilimo inachangiwa na aina ya wagani wanaozalishwa na vyuo vya mafunzo,” alisema.

Kusaya alisema ili vyuo vya mafunzo ya kilimo vya serikali na binafsi viende sambamba na kasi ya mabadiliko ya hali ya ukuaji wa uchumi wa nchi, kunatakiwa kuwe na ushirikiano wa wadau mbalimbali ndani na nje ya nchi.

“Katika kufanya hayo yote, wakuu wa vyuo vya mafunzo ya kilimo wanapaswa kushirikiana na wadau wengine wa maendeleo katika kuboresha teknolojia na mbinu za ufundishaji,” alisema.

Aliwashukuru wadau wa maendeleo mashirika ya Sustainable Agriculture Tanzania (SAT) na Lutheran World Relief (LWR) kwa kuwa mstari wa mbele kufanya kazi za kuimarisha taaluma na mafunzo katika vyuo vya mafunzo ya kilimo nchini.

Mkurugenzi wa Idara ya Mafunzo, Huduma za Ugani na Utafiti, Wizara ya Kilimo, Dk Wilhelm Mafuru, alisema maboresho ya mitaala katika vyuo vya mafunzo ya kilimo vya serikali na binafsi, yamehuishwa na yataendela kuhuishwa ili kuwaandaa wanafunzi na wahitimu kujiajiri badala ya kuwa na fikra za kuajiriwa.

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu, Morogoro

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi