loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Makamu Mwenyekiti achukua fomu urais Zanzibar

MAKAMU Mwenyekiti wa chama cha siasa cha Ada Tadea, Juma Ali Khatib, amechukua fomu kuomba ridhaa ya kuwania nafasi ya urais wa Zanzibar kupitia chama hicho, huku akitangaza kuyalinda Mapinduzi ya Zanzibar na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kama tunu za kitaifa.

Khatib alichukua fomu hiyo jana katika ofisi za chama hicho zilizopo Kwa Mchina mjini Unguja na kukabidhi Sh 300,000 ikiwa ni malipo ya fomu kwa mujibu wa Katiba yao.

Naibu Katibu Mkuu wa Ada Tadea Zanzibar, Rashid Mshenga, alimkabidhi Khatibu fomu hiyo ya kuwania nafasi ya urais. Baada ya kukabidhiwa fomu hiyo alielekezwa kutafuta wadhamini 300 katika mikoa ya Unguja na Pemba na kukamilisha kazi hiyo katika kipindi cha wiki moja.

“Nakukabidhi fomu ya kuomba ridhaa ya kuwania nafasi ya urais wa Zanzibar kwa tiketi ya chama cha Ada Tadea, unatakiwa kupata wadhamini kutoka Unguja 150 na Pemba 150 na kurudisha fomu hii katika kipindi cha wiki moja,” alieleza Mshenga.

Khatib ambaye ni Waziri Asiye na Wizara Maalumu katika Serikali ya Zanzibar, alisema amejifunza mambo mengi katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wa Rais Dk Ali Mohamed Shein, ikiwamo uongozi wa busara uliotawaliwa na uvumilivu wa kisiasa na hekima kubwa.

Alisema akichaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar, atahakikisha Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 yanalindwa kwa nguvu zote, huku Muungano ambao ni tunu ya kitaifa unaimarishwa kwa maslahi ya pande mbili pamoja na kujikita zaidi katika kukuza uchumi na maendeleo.

“Mimi ni muumini wa Muungano na Mapinduzi ya Januari 12, mwaka 1964. Nikichaguliwa nitaendeleza dhamira iliyoasisiwa na viongozi wetu na kuona Muungano unaimarishwa katika uchumi na maendeleo,” alisema.

Aidha, Khatib alisema miradi mikubwa ya kimkakati ikiwamo ujenzi wa Bandari ya Mpiga Duri, ataiendeleza na kuikamilisha kwa ajili ya serikali kupata fedha za kukuza uchumi.

“Ipo miradi ya kimkakati ambayo imeanzishwa na Rais Dk Ali Mohamed Shein katika kipindi chake, mimi nikichaguliwa nitaiendeleza ikiaemo ujenzi wa Bandari ya Mpiga Duri na jengo la maabara na hospitali ya kisasa ya rufaa iliopo Binguni,” alisema.

Kwa upande wa wanawake, alisema atahakikisha watakaojifungua watapata posho ya miaka miwili kwa ajili ya malezi ya watoto na ukuaji bora wenye siha bora.

Alisema pia atahakikisha anapambana na vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia ambayo vimekuwa kikwazo kwa kundi hilo katika kupiga hatua za maendeleo.

“Zanzibar tunakabiliwa na tatizo la vitendo vya udhalilishaji kwa wanawake na watoto, ambavyo vinachangiwa na wanaume. Nikichaguliwa nitapambana na ukatili huo kwa kuweka sheria kali,” alisema.

Tayari vyama sita vya siasa vimeanza uchukuaji fomu ndani ya vyama vyao kwa nafasi ya urais wa Zanzibar, vikiwamo Chama Cha Mapinduzi (CCM), ACTWazalendo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na AAFP Wakulima.

foto
Mwandishi: Khatib Suleiman, Zanzibar

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi