loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Limao ni zaidi ya dawa, kiungo na sharubati!

FIKIRIA tunda linaloweza kutumiwa kukuza uchumi, kutumiwa kama dawa, kiungo, sabuni, dawa ya kuua viini, na kipodozi.

Aidha unaweza kulila, kunywa maji yake, na kukamua mafuta yake. Tunda hilo lina rangi ya kupendeza, linapatikana ulimwenguni pote tena si ghali, huenda hata sasa una tunda hilo jikoni.

Ni tunda gani hilo? jibu; Ni limau! Miaka ya karibuni wakulima hawakupata faida ya kilimo cha malimau, malundo ya tunda hilo yalionekana katika sehemu za kuhifadhia takataka sokoni mengine yakiozea shambani.

Adha, matumizi ya asili ya tunda hilo yalipungua kutokana na teknolojia ya kisasa ya kulisindika katika hali ya umajimaji na unga unga.

Hivi sasa matumizi ya limau yameongezeka hasa katika kipindi hiki cha janga la utandafu (Covid-19), kutokana baadhi ya wataalamU wa afya kulitaja tunda hilo kuwa ni kiini cha Vitamini C ambayo hupatikana katika matunda na majani mabichi.

Kikemia, ni aina ya asidi askobini na binadamu ni kati ya spishi chache ambazo haziwezi kutengeneza asidi hii mwilini, hivyo watu hutegemea chakula chenye vitamini hii.

Vitamini C Kwa mujibu wa wataalamu wa afya vitamini C ni muhimu kwa ukuzi na ustawishaji wa mwili.

Wanasema vitamini hiyo hupatikana katika vyakula vingi kama vile mboga za majani, nyanya, pilipili hoho, zabibu nyeusi, na stroberi.

Matunda ya jamii ya machungwa yakiwamo malimau ndiyo chanzo kikuu cha vitamini C. Kiasi cha vitamini C katika limau hutegemea mambo mengi, kama vile hali ya hewa ya eneo ambalo tunda hilo lilikuzwa, ubivu wa tunda, na hata mahali ambapo tunda hilo lilikuwa katika mti.

Baadhi ya wataalamu wanasema, kiasi cha vitamini C kinachopendekezwa kwa siku kwa mtu mzima mwenye afya ni miligramu 100 hivi. Limau lenye ukubwa wa wastani lina karibu nusu ya kiasi cha vitamini C kinachopendekezwa kwa mtu mzima.

Muuza genge maeneo ya Sinza A, Mwajabu Sultan anasema matumizi ya limau yameongezeka tangu mlipuko wa Covid-19, naye Arodia Kato anasema kutokana na maelekezo ya marehemu mume wake, mtaalamu wa afya na daktari alilitumia tunda hilo kutengenezea sharubati kila siku kwa matumizi ya familia.

Asili Inasemekana asili ya limau ni Kusini-Mashariki ya Asia. Baadaye matunda haya yalisafirishwa kwenda Magharibi kuelekea Bahari ya Mediterania. Milimau hustawi vizuri katika eneo lenye baridi na joto la kiasi.

Kutokana na sababu hiyo, miti ya malimau hustawi vizuri katika nchi za Argentina, Hispania, Italia, Mexico na sehemu za Afrika na Asia. Ukuaji huu hutegemea aina ya limau na eneo, mti uliokomaa unaweza kuzalisha kati ya malimau 200 hadi 1,500 kwa mwaka.

Aina mbalimbali za milimau huchanua maua katika majira tofauti, hivyo malimau yanaweza kuvunwa mwaka mzima. Italia.

Bado kuna mdahalo mkali ikiwa Waroma wa kale waliotesha malimau, hata hivyo baadhi maandishi yanathibitisha kwamba Waroma walikuwa na uelewa wa furungu tunda ambalo ni jamii ya machungwa linalofanana sana na limau kubwa.

Katika kitabu chake “Natural History”, mwanahistoria Mroma “Plini Mkubwa” (Pliny the Elder) alitaja kwa ufasaha mfurungu na tundalake. Hata hivyo, wataalamu wengine maarufu wanawataja Waroma waliyafahamu malimau kwa sababu picha zilizochorwa ukutani na picha nyingine zinaonesha malimau na si mafurungu.

Mfano mzuri ni nyumba ya kale iliyofukuliwa huko Pompeii, iliyobatizwa “Nyumba ya Miti ya Matunda”, kwa sababu imepambwa kwa picha zilizochorwa ukutani za mimea mbalimbali pamoja na mlimau. Ni kweli mti huo ulitazamwa kipekee na kutumiwa kama dawa tu.

Ni vigumu kuelewa wakati huo wa kale kama ilikuwa rahisi kustawisha malimau kwa wingi katika jamii za Kiroma.

Kisiwa cha Sicily kilichopo Italia, ambacho kina majira marefu ya kiangazi yenye joto na baridi ya kiasi; ndilo eneo ambalo huzalisha matunda ya jamii ya machungwa na malimau kwa wingi nchi. Hata hivyo, kuna maeneo mengine hasa Pwani ambapo malimau hustawishwa vizuri.

Aidha inaelezwa katika vyanzo mbalimbali kuwa, miji maridadi ya Sorrento Kusini kidogo mwa Naples na Kusini ya ghuba maridadi ya Amalfi yenye urefu wa zaidi ya kilomita 40 , Positano, Vietri sul Mare na miji midogo midogo kwenye ghubai hiyo hzalisha malimau kwa wingi. Malimau yanayostawishwa katika miji hiyo yana utambulisho maalumu.

Wenyeji wa miji hiyo wana haki ya kulinda utambulisho wa milimau yao kutokana na miti hiyo kupandwa kwa ustadi kwenye matuta kando ya mlima unaopata mwangaza wa jua unaosabababisha kuzalisha malimau yenye maji mengi na harufu nzuri.

Ustawishaji Wataalam wanasema huhitaji eneo kubwa ili kupanda mlimau inawezakana kuipanda kwenye veranda iliyo na mwangaza wa kutosha wa jua. Miti midogo ya malimau inaweza kustawishwa katika vyungu na pia kama mapambo. Mimea hiyo hustawi kwenye joto pasipo na upepo.

Hata hivyo, kunapokuwa na baridi kali kupita kiasi, mimea hiyo huhitaji kufunikwa au kuingizwa ndani ya nyumba iwapo vyungu vya mimea hiyo vipo nje. Matumizi zaidi ya malimau Je, wewe hutumia malimau mara ngapi? Baadhi hutia kipande katika kikombe cha chai, pombe kali na hata kunyunyizia maji yake katika matunda kama vile papai, parachichi, au kwenye mchanganyiko wa matunda.

Wengine kupitia uchunguzi wa mwandishi wa makala haya, imebainika kuwa hutumia ganda lake au maji yake katika keki, maandazi na nusu keki. Inawezekana hata wewe hutengeneza juisi ya limau.

Ni kawaida kwa wataalamu wa mapishi ulimwenguni kuhifadhi malimau kwa sababu huyatumia kwa njia mbalimbali katika mapishi yao. Je, umewahi kutumia maji ya limau kama dawa ya kuua viini au kuondoa madoa? Jaribu leo!

Baadhi hutumia nusu kipande cha limau kusafisha na kuua viini katika mbao zinatumika kukatia vyakula, ni mbadala wa dawa zenye klorini za kuondoa madoa au kusafisha sinki. Watu wengine hutumia mchanganyiko wa maji ya limau na magadi.

Aidha, kuweka nusu kipande cha limau ndani ya friji au mashine ya kuosha vyombo huondoa harufu mbaya na kufanya vifaa hivyo viwe na harufu nzuri.

Malimau hutoa asidi sitriki ambayo hutumika kuhifadhi na kufanya vyakula na vinywaji viwe na ladha chachu. Ganda la limau na upande wake wa ndani hutoa pektini ambayo hutumiwa katika viwanda vya vyakula.

Aidha mafuta yanayokamuliwa kutoka katika ganda hutumiwa katika vyakula, dawa, na vipodozi. Kuna matumizi mengine mengi ya tunda hilo. Limau ni tunda lenye rangi yenye kupendeza, lenye ladha nzuri, na lenye matumizi Mti wa Limao mengi.

BABA wa Taifa, Mwalimu Julius K Nyerere, ndiye Rais wa ...

foto
Mwandishi: Maria Inviolata

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi