loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kunywa maji mengi uokoe figo, fedha

FIGO ambayo jukumu lake kubwa ni kuchuja damu na kutoa taka mwilini kwa njia ya mkojo ni kiungo muhimu ndani ya mwili wa binadamu.

Licha ya umuhimu wa kiungo hicho, kuna uwezekano wa kupata maradhi mbalimbali ikiwemo mawe.

Tatizo la mawe kwenye figio ambalo makala haya yanaliangazia kwa kina inaelezwa kwamba linaanzia kwa kwa kuwepo kwa baadhi ya madini kwa wingi katika mkojo.

Mfano wa madini hayo ni calcium oxalate na citric acid na wakati mwingine mawe kwenye figo yanatokana na mtu kutengeneza kiwango kidogo cha mkojo kutokana na kutokunywa maji ya kutosha.

Wakati mwingine maambukizi ya bakteria katika mfumo wa mkojo yanaweza pia kusababisha mawe kwenye mfumowa mkojo na tatizo hili huwaathiri zaidi wanaume, hususani wenye umri wa kuanzi miaka 40.

Dalili za mawe kwenye figo ni maumivu ya tumbo, kukosa dalili zozote na hali hii hujulikana mtu anapopimwa kwa sababu nyingine. Haya mawe huitwa ‘mawe kimya’.

Dalili nyingine ni kukojoa na kuhisi kutaka kukojoa kila mara, kichefuchefu na kutapika, kukojoa damu (haematuria) na uchungu au kuwashwa unapokojoa. Kuhusu maumivu ya tumbo ukali wake huwa tofauti kati ya mtu mmoja na mwingine kutegemea aina, ukubwa na mahali jiwe lilipo.

Kumbuka maumivu hayalingani na ukubwa wa jiwe. Jiwe dogo lisilo laini husababisha maumivu makali kuliko jiwe kubwa ambalo ni laini.

Habari njema kwa watanzania ni kwamba hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila kwa mara ya kwanza imeanza kutoa rasmi huduma ya matibabu ya kusaga mawe kwenye figo kwa kutumia njia ya mawimbi mshtuko.

Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Profesa Lawrance Museru anasema tangu Juni mosi mwaka huu huduma hiyo ilipoanza rasmi hadi makala haya yanaandikwa mwishoni mwa wiki wagonjwa 10 walikuwa wamepata huduma hiyo.

Profesa Museru anasema huduma hiyo inafanywa kwa kutumia mashine ambayo inatoa mawimbi sauti yanayosafiri kupitia ngozi hadi kwenye figo katika sehemu vyenye mawe.

Mawimbi hayo hugeuka kuwa nishati yenye uwezo wa kuvunja mawe kuwa madogo mithili ya mchanga ambapo yakishasagwa yanatoka kwa njia ya haja ndogo.

“Huduma hii haimlazimu mgonjwa kulazwa wala kufanyiwa upasuaji,” anasema Profesa Museru.

Kuanzishwa kwa huduma hiyo ni mwendelezo wa kutekeleza juhudi za serikali kuboresha huduma bobezi za kibingwa ili kuongeza wigo wa utoaji huduma ambazo huko nyuma zilikuwa hazitolewi hapa nchini.

Gharama ya kutoa huduma hiyo kwa mgonjwa mmoja ni shilingi 500,000 kulingana na kundi alilopo mgonjwa na shilingi milioni 4.2 kwa mgonjwa kutoka nje ya nchi.

Endapo mgonjwa atasafirishwa kwenda nje ya nchi gharama za kusaga vijiwe hufikia shilingi milioni 10 kwa mgonjwa mmoja hivyo kwa wagonjwa 10 ambao wamepatiwa huduma hiyo, serikali imeokoa shilingi milioni 95.

Katika kipindi cha mwaka 2019 jumla ya wagonjwa 1,035 wenye mawe kwenye figo walionwa katika kliniki za wagonjwa wa nje katika hospitali ya Muhimbili ambapo kati yao wagonjwa wapya ni 425 wakati waliolazwa kutokana na tatizo hilo ni 114.

Kwa sasa Mloganzila ina uwezo wa kuwahudumia wagonjwa watano kwa siku na kadiri wagonjwa watakavyoongezeka watakuwa na uwezo wa kutoa huduma hiyo mara tatu kwa wiki.

Katika kipindi cha mwaka 2010 hadi 2017 wagonjwa 23 wenye matatizo ya mawe kwenye figo walipatiwa rufaa kwenda nje ya nchi. Profesa Museru anataja faida ya matibabu kwa njia ya mawimbi kuwa ni pamoja na mgonjwa kutohitajika kulazwa hospitali kwani mgonjwa hutibiwa ndani ya dakika 45 hadi saa moja na kuruhusiwa kuondoka siku hiyo hiyo.

Kwa upande wake, daktari bingwa wa mfumo wa njia ya mkojo Muhimbili- Mloganzila, Hamisi Isaka, anasema kabla ya kuanza kwa huduma hiyo ilikuwa inamchukua mgonjwa mwezi mmoja hadi mitatu kufanikisha kuondoa mawe kwenye kibofu na kurudi kwenye maisha ya kawaida.

Anazidi kufafanua kwamba ilimlazimu mgonjwa kufanyiwa upasuaji mkubwa na ndio maana ilimchuku mtu wastani wa mwezi mmoja hadi mitatu kuimarika na kurudi kwenye majukumu yake ya kawaida.

Anasema katika utaratibu wa sasa, mgonjwa huendelea kuangaliwa hali yake kwa wiki moja mpaka mwezi na hapo atakuwa amepoana na kuendelea na majukumu yake bila ya kuwa na maumivu.

“Wakati wa kusaga mawe magonjwa hapewi dawa yoyote hata za usingizi isipokuwa dawa ya maumivu kwa njia ya mshipa. Kama kuna jiwe kwenye figo huonekana kwa njia ya radiolojia,” anafafanua.

Dk Isaka anashauri watu kuwa na utamaduni wa kunywa maji kwa wingi kuanzia lita mbili hadi tatu na nusu kwa siku ili kuepuka tatizo kupata mawe kwenye figo. Pia anawataka kula matunda kwa wingi na mbogamboga.

Anasema ni muhimu kuwa makini na milo ya vyakula inayoliwa ili kutokutengeneza kemikali nyingi yenye kusababisha figo na kwamba vyakula vya kuepuka ni pamoja na nyama nyekundu. Hata hivyo, anasema kuna ambao miili yao hutengeneza kemikali hizo kwa kutokea kwenye ini.

Mwajuma Mohamed ni mmoja wa watu waliotibiwa kwa njia hiyo ya kusaga mawe bila kufanyiwa operesheni. Akizungumza na waandishi huku akionesha mawe yaliyotoka kwa njia ya haja ndogo

Anasema hivi sasa afya yake imeimarika na hivyo anashukuru huduma aliyopata hospitalini hapo na kuwataka wananchi kutoogopa bali kujitokeza kuhudumiwa.

“Niliumwa kwa muda mrefu na nilishawahi kufanyiwa upasuaji lakini hali haikubadilika hivi sasa baada ya kupatiwa huduma mpya afya yangu imeimarika, nawashukuru sana Muhimbili,” anasema. Kwa upande wake, Samson Makorere, mkazi wa Kinondoni jijini Dar es Salaam, anasema alipatiwa huduma hiyo ndani ya mfupi na kwamba hakuhisi maumivu yoyote.

“Ilikuwa Juni 5, 2020 nilipofanyiwa huduma hii na hata wakati mawe hayo yanatoka wala sikuhisi maumivu ila kulikuwa na kipande cha jiwe kimoja kikubwakubwa ndicho kilinchonianya nihisi kama kuna kitu kinatoka,” anasema.

Makorere anasema awali alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa unaotokana na uambukizo kwenye mfumo wa mkojo (UTI) na kwamba alikuwa akipata matibabu katika hospitali mbalimbali.

Anasema mwanzoni mwa mwaka huu alifanyiwa upasuaji katika hospitali binafsi uliogharimu jumla ya Sh milioni saba lakini hali iliendelea kutokuwa shwari sana.

Makorere anapongeza huduma hiyo ya kuvunja mawe hospitalini hapo kwa kuwa alipomaliza kupatiwa huduma alinyanyuka mwenyewe na kwenda benki kwa ajili yakuchukua fedha za malipo.

Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Mloganzila, Dk Julieth Magandu anasema uwezo wa hospitali hiyo kutoa matibabu hiyo ni wa kuridhisha na kwa sasa wanatoa huduma hiyo kila wiki siku ya Jumanne na kwamba wana uwezo pia wa kuwafanya huduma hiyo wagonjwa watano kwa siku.

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimembariki Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea ...

foto
Mwandishi: Lucy Lyatuu

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi