loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

TPSF yataka juhudi zaidi sekta ya kilimo

BAADA ya Tanzania kuingia uchumi wa kati, sekta binafsi imesifu hatua hiyo kubwa na kutaka juhudi zaidi ziwekwe katika kukuza sekta ya kilimo, ambayo itaongeza uzalishaji wa malighafi za viwandani.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Godfrey Simbeye alisema jana kuwa lengo la nchi, siyo kubaki hapo ilipofikia, bali kupanda hadi kufikia nchi ya uchumi wa kipato cha kati cha juu.

Simbeye alisema moja ya njia ya kufikia uchumi wa kipato cha kati cha juu, ni kuwekeza kwenye kilimo ili kukifanya kiwe cha biashara. Alisema ukuaji wa sekta ya kilimo, unapaswa kuongezeka kutoka asilimia 3.4 ya sasa hadi kufikia asilimia 6 au 7, na kwa kufanya hivyo Tanzania itapanda haraka kutoka nchi ya uchumi wa kipato cha kati cha chini hadi kuwa nchi ya kipato cha kati cha juu.

“Tulipoingia kwenye uchumi wa kati ni sahihi, lakini ili tukue zaidi, nguvu iwekezwe kwenye kilimo ambacho pia kitakuza uzalishaji wa viwanda; wastani wa pato la mwananchi kwa mwaka katika nchi yenye pato la kati la chini ni Dola za Marekani kati ya 1,006 hadi 3,955 ambapo Tanzania tulikuwepo kwa kuwa pato la wastani la Mtanzania kwa mwaka kwa sasa ni Dola za Marekani 1,026 sawa na wastani wa Dola 2 kwa siku,” alisema Simbeye.

“Ili Tanzania tuwe nchi ya kipato cha kati cha juu, lazima pato la wastani la mwananchi kwa mwaka lifikie Dola za Marekani 3,956 hadi 12,000; kwa hiyo tunahitaji kuwekeza zaidi kwenye kilimo cha kibiashara ili tupande na kufikia hatua hiyo ya pili ya uchumi,” aliongeza mtendaji huyo wa TPSF.

Simbeye alisema taasisi yao, ina mchango mkubwa katika kuiwezesha nchi kufikia uchumi wa kati. Alisema TPSF wamewekeza kwenye sekta mbalimbali ikiwemo viwanda, biashara, kilimo na madini.

Hoja hiyo ya kuboresha kilimo iliungwa mkono na Mtaalamu wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Humphrey Moshi, aliyesema ni hatua kubwa kwa Tanzania kufikia uchumi wa kati miaka mitano kabla ya muda uliokadiriwa kwenye Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025, ambayo yeye alishiriki kuiandaa. Profesa Moshi alisema hatua hiyo kiuchumi, inamaanisha kasi ya umaskini, imepungua na uchumi wa nchi unakua kuelekea kuwa uchumi wa viwanda.

Alisema hayo ni matunda ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli ya kuitekeleza Dira ya Maendeleo kwa vitendo, kwa kuboresha mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara.

“Kwa kuingia uchumi wa kati, tunatakiwa kuhakikisha sekta ya kilimo inakuwa na tija zaidi, kuwe na uzalishaji wa kutosha kwa ajili ya viwanda, na viwanda vizalishe bidhaa kwa wingi kwa ajili ya kuuza nje, hivyo baada ya kuingia uchumi wa kati, tunatakiwa sasa tubadilike kwa kasi na kuwekeza zaidi katika kilimo cha kisasa cha umwagiliaji,” alieleza Profesa Moshi.

Profesa Moshi alisema kilimo kitakuza kwa haraka sekta ya viwanda, ambayo itasaidia katika uzalishaji wa bidhaa na huduma, kuongeza ajira zenye hadhi, kama ilivyofanyika kwenye baadhi ya nchi za Asia ikiwemo Japan, Indonesia, Hon Kong na Taiwan.

“Nchi ikishaingia uchumi wa viwanda, kinachofuata ni kuwekeza zaidi kwenye sayansi na teknolojia. Nchi ikishakuwa na watu wengi walioingia kwenye mkondo wa sayansi na teknolojia, watasaidia kuendeleza na kukuza uchumi wa viwanda na pato la wastani la mwananchi litakuwa hadi kufikia Dola za Marekani 10,000 kwa mwaka kama ilivyo kwa Wachina,” alieleza Profesa Moshi.

Pia wadau mbalimbali walichanga hadi ujenzi ukafikia hatua ya kuezekwa ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi