loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Uwekezaji miundombinu, huduma unavyopaisha nchi

UWEKEZAJI mkubwa kwenye huduma, miundombinu wezeshi ya kiuchumi na usimamizi thabiti wa mapato ya ndani, umetajwa kuwa chachu ya mageuzi ya kiuchumi, yanayoendelea kuipaisha kimataifa hatimaye kuondolewa kwenye orodha ya nchi masikini.

Taarifa zinaonesha mapato ya ndani yameongezeka kutoka Sh trilioni 11.0 mwaka 2014/15 hadi Sh trilioni 18.5 2018/19, huku usimamizi na udhibiti thabiti ukitajwa kuwa umewezesha serikali kutekeleza miradi ambayo ni chachu ya maendeleo ya nchi na kuboresha huduma mbalimbali ikiwamo elimu na afya. Elimu bila malipo ni miongoni mwa maeneo yanayotajwa kuwa na mchango mkubwa wa maendeleo.

Serikali inatoa Sh bilioni 23.8 kila mwezi kugharimia elimu bure. Katika hotuba yake ya kufunga Bunge hivi karibuni, Rais John Magufuli alisema tangu mpango uanze kutekelezwa mwaka 2016, mpaka Februari mwaka huu serikali imetumia Sh trilioni 1.01 kugharimia elimu bure. Vile vile kuanzia mwaka 2015 hadi mwaka huu, lipo ongezeko la shule za msingi kutoka 16,899 hadi 17,804 na sekondari kutoka 4,708 hadi 5,330.

Wanaojiunga mwaka wa kwanza vyuo vikuu, wameongezeka kutoka 65,064 hadi 87,813 ; na wenye kupata mikopo idadi yao imeongezeka kutoka 98,300 mwaka 2014/2015 hadi 130,883 mwaka 2019/20.

Alipozungumza na gazeti hili hivi karibuni, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Profesa Faustine Bee alisema maboresho katika sekta ya elimu ni mwelekeo mzuri wa nchi, kwani hakuna nchi duniani iliyoendelea bila kuwekeza kwenye elimu.

Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia, Abbas Mwalimu ambaye ni mchambuzi wa masuala ya uchumi na diplomasia, anataja uwekezaji kwenye afya ni chachu ya maendeleo kutokana na kumfanya Mtanzania kupata huduma bora, jambo ambalo ni kichocheo cha kufanya kazi kwa bidii.

Sekta ya afya imeimarishwa kwa kuboresha matibabu ya kibingwa, ambayo yamesaidia serikali kuokoa mamilioni ya shilingi, kwa kutolazimika kupeleka watu kutibiwa nje ya nchi. Idadi ya rufaa za kwenda nje ya nchi, zimepungua kwa asilimia 95.

Upatikanaji wa dawa na vifaa tiba umeimarishwa kwa kuongeza bajeti kutoka Sh bilioni 31 mwaka 2015 hadi Sh bilioni 270. Magari 117 ya kubebea wagonjwa, yamenunuliwa na kusambazwa na madaktari bingwa 301 wamesomeshwa.

Ujenzi wa barabara na madaraja ni vielelezo vingine ambavyo wachumi wanasema vinachangia kukua kwa uchumi. Serikali ya Awamu ya Tano imejenga barabara 3,500 kwa kiwango cha lami na kufanya nchi kuwa na takribani kilometa 13,000 ya barabara za lami. Barabara nyingine zenye kilometa 2000 zinaendelea kujengwa.

foto
Mwandishi: Stella Nyemenohi

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi