loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tujivunie Tanzania kuingia uchumi wa kati

TANGU Rais John Magufuli alipoingia madarakani mwaka 2015, ndoto na malengo yake makubwa ilikuwa ni kuhakikisha ifi kapo mwaka 2025, Tanzania inakuwa ni miongoni mwa nchi zilizo katika uchumi wa kati.

Na aliainisha utekelezaji wa ndoto hiyo kupitia falsafa yake ya Hapa Kazi Tu, akimaanisha kila Mtanzania anawajibika kuchapa kazi popote alipo kwa lengo la kujiinua kiuchumi lakini pia kuinua uchumi wa taifa kwa ujumla.

Hapa Kazi Tu ni falsafa ya kisiasa, kiuchumi na kijamii inayowahimiza watu kufanya kazi, ni falsafa inayomaanisha kwamba, mtu yeyote kuanzia rais, makamu wa rais, waziri mkuu, mawaziri na viongozi wengine nchini kote lazima wafanye kwa lengo moja la kuwakomboa watu wanaowaongoza.

Rais Magufuli alihimiza bila kuchoka na kuonesha kwa vitendo umuhimu wa kila sekta, kilimo, miundombinu, huduma za jamii kama vile maji, afya na elimu, sekta ya usafiri kwa maana ya anga, barabara na reli kuimarishwa.

Ndani ya miaka yake mitano ya uongozi, ameonesha kwa vitendo utendaji wa serikali yake kuanzia miradi mikubwa inayoendelea kujengwa kama vile reli ya kisasa (SGR), ujenzi wa madaraja ya juu Tazara na Ubungo, mradi wa umeme wa Mwalimu Nyerere (Rufiji) na miradi mingine nchini kote.

Ameboresha kwa kiwango kikubwa bajeti ambapo fedha nyingi zimetengwa kwa matumizi ya maendeleo na kupaisha sekta za afya, elimu na maji. Kipaumbele chake kimekuwa ni kujenga uchumi kupitia mapinduzi ya viwanda, jambo alilofanikiwa kiasi kikubwa kwani alihimiza mnyororo mzima wa viwanda, tangu mkulima hadi mzalishaji kiwandani kuboreshwa.

Serikali haikuwa nyuma kuleta mapinduzi sekta ya madini ambayo miaka mingi imekuwa ikipigiwa kelele kutokana na faida yake kutoonekana. Sasa Tanzania ni mmoja wa wamiliki wa kampuni kubwa ya madini ya Twiga ikipata mgawo na imefanyia marekebisho sheria ya madini kwa kuhakikisha nchi inanufaika na madini hayo badala ya kuachiwa mashimo.

Serikali pia ilileta uwajibikaji kwa watendaji wote ikiwemo kuwachukulia hatua wale wote waliofanya ubadhirifu, rushwa na kuendeleza urasimu. Kutokana na jitihada hizo, ndoto yake imetimia kabla ya wakati.

Benki ya Dunia imeingiza nchi katika orodha ya nchi zenye uchumi huo wakati. Tanzania imeingia miaka minane mbele ya makadirio yake, kutokana na kuongezeka kwa wastani wa kipato cha mtu mmoja mmoja hadi kitaifa.

Imeelezwa Tanzania imekuwa miongoni mwa nchi 50 duniani, nchi ya 24 kwa Afrika na ya pili kwa Afrika Mashariki kuingia katika uchumi wa kati. Kwa hatua hiyo, Rais Magufuli katika mtandao wa tweeter aliwapongeza Watanzania kwa mafanikio hayo na kueleza kuwa huo ni ushindi mkubwa unaotokana na kazi iliyofanywa na Watanzania wote kwa ujumla wao.

Alisema hatua hiyo ni kubwa na Watanzania wote wanapaswa kujivunia jambo la msingi likiwa ni kuendelea kuchapa kazi kwa mafanikio zaidi.

foto
Mwandishi: Halima Mlacha

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi