loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Takukuru yanasa wanasiasa zaidi tuhuma za rushwa

WAKATI Tanzania ikielekea katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu, wimbi la wanasiasa wanaotiwa mbaroni kwa tuhuma za kujihusisha na rushwa ili kujitengenezea nafasi za uongozi, limeongezeka.

Katika kipindi cha wiki kadhaa sasa, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imewakamata makada kadhaa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa tuhuma za kujihusisha na rushwa.

Jumatano wiki hii mbunge wa Jimbo la Tabora Kaskazini aliyemaliza muda wake, Almas Maige alikamatwa na Takukuru akituhumiwa kuwa na viashiria vya rushwa. Inadaiwa kuwa mbunge huyo alikuwa na kundi la madiwani ofisini kwake Ipuli.

Maige anadaiwa kukamatwa majira ya saa sita mchana . Akizungumza tukio hilo, Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Tabora, Musa Chaulo alisema kwamba baada ya mahojiano walimpa onyo mbunge huyo.

Chaulo alisema kwamba atalitolea ufafanuzi tukio hilo baadae, kwa kuwa wapo katika uchunguzi. Nako Mkoani Shinyanga, taasisi hiyo imemtia mbaroni dereva teksi, Joseph Tasia kwa tuhuma ya kukutwa na doti 600 za vitenge vyenye nembo ya CCM na vitenge vya kawaida, vikiwa vimehifadhiwa nyumbani kwake.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Takukuru mkoani humo, Hussein Mussa alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa Juni 29, mwaka huu saa 3 usiku Mtaa wa Mwasele B nyumbani kwake akiwa na vitu hivyo.

Alidai kuwa Tasia alikutwa na doti 600 za vitenge vyenye nembo ya CCM na vya kawaida, vikiwa vimehifadhiwa nyumbani kwake, jambo linaloashiria kuwa vilikuwa vinaandaliwa kutumika katika kufanya ushawishi kwa wapiga kura. Alieleza kuwa uchunguzi uliofanywa na maofisa wa Takukuru mkoa wa Shinyanga, umebaini kwamba Tasia hana duka wala hafanyi biashara ya kuuza vitenge.

“Katika mahojiano na maofisa wa Takukuru baada ya mtuhumiwa kukamatwa na mzigo huo, alishindwa kutoa maelezo yanayojitosheleza na hata nyaraka za manunuzi ya mzigo huo alizowasilisha, hazijitoshelezi na hivyo kuongeza mashaka juu ya uhalali wa vitenge hivyo,” alisema Mussa.

Mussa alisema kuwa uchunguzi wa kina bado unaendelea, ili kubaini iwapo vitenge hivyo vilikuwa ni kwa ajili ya rushwa katika uchaguzi ujao au ni kwa ajili ya kufanya biashara katika msimu huu wa kuelekea uchaguzi mkuu wa viongozi.

Hivi karibuni Takukuru mkoani humo pia ilimkamata na kumshikilia Mjumbe wa CCM Mkutano Mkuu Taifa, Asha Makwaiya, mkazi wa Majengo Mapya Mjini Shinyanga, kwa tuhuma za kutoa rushwa kwa wajumbe wa Jumuiya ya Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT).

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari ilitolewa, Makwaiya alikamatwa Juni 28, mwaka huu. Mjumbe huyo wa mkutano mkuu alikamatwa akiwa na wajumbe wengine 10, ambao ni viongozi wa UWT Kata ya Ngokolo.

WANACHAMA wa vyama vya ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi