loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Zumo afunguka maisha yake

SANAA haikuwa ndoto yake, wala shule hakuitaka pengine alikuwa ni mtu tofauti kabisa na watoto wa mtaani kwao, wakati anaenda shule akili yake ilikuwa kwenye magari, huwezi kunielewa endelea kusoma utanielewa.

Pengine zile kelele za Ubungo, Msata, Mwenge Mbagala, alivutiwa nazo na akaona hapa ndipo sehemu sahihi ya kupiga pesa, kwa bahati nzuri alikuwa ni dereva asiyepeleka gari gereji, hujaanza kunielewa tu?

Mwaka 2003 alianza kutimiza ndoto zake za udereva baada ya kuingia kwenye ufundi wa magari, shule akaweka kapuni na kufuata alichokipenda, wanasema usimlazimishe punda kunywa maji, muache.

Pengine huko aliko hawezi kumsahau rafiki yake Oscar Martin, maana bila yeye sijui ingekuaje, huenda leo hii angekutengenezea gari lako, lakini ndio hivyo ameenda kutimiza ndoto ambayo hakuwahi kuiota.

Hapa namzungumzia ‘Anko Zumo’ amefunguka mengi sana kuhusu maisha yake mpaka sasa alipo, Zumo ni mchekeshaji wa tofauti sana nchini anafanya kazi hiyo na familia yake, cha kuvutiwa zaidi familia nzima ime- anza kunywa yale maji.

FAMILIA NA KUONGEZA MKE

Zumo anasema ana watoto wanne, Omary, Feisal, Mai na Zahir, anasema yeye ni mtu wa Pwani haswa, suala la kuwa na mke wa pili lipo na atahakikisha anaoa mke wa pili, licha ya kuwa bado mipango ya kufanya hivyo haijakaa sawa.

Zumo kwa sasa ana mke mmoja, Habiba aliyempata kupitia, mdogo wake ambaye anafanya naye kazi kwa jina la ‘ Mishi Baby’ anasema alianza kuwa na urafiki na mke wake kabla ya kumuoa.

MAI ZUMO ANAIBEBA FAMILIA

Zumo anasema mchango wa Mai ni mkubwa sana kutokana na kipaji alichonacho, anasema amefanya jamii iwatambue na kwamba yeye ndo anafanya Mai aonekane kuwa na kipaji.

Anasema kila kitu kinachotoka kwa Mai, watu wafahamu kimetoka kwa wazazi wake, hivyo pamoja na Mai kufanya vizuri kwenye uchekeshaji, wazazi wake ndiyo msingi imara wa mtoto huyo kuwa hivyo.

MAGARI SIO ISHU KWAKE

Wengi wao wanafahamu mafanikio, ni kuwa na vitu vya thamani, kama gari, nyumba au hata maisha mazuri, ila kwa upande wa Zumo anakwambia hivyo vitu vipo tu sio ishu kwake.

Zumo anasema mafanikio makubwa kwake ni kukutana na baadhi ya viongozi wa juu wa nchi, akiwemo Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Waziri wa Habari, Dk Harrison Mwakyembe, Rais Mstaafu Jakaya Kikwete na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

UTANI NA MKEWE

Zumo anasema ametoka kijiji kimoja na mkewe Habiba, hivyo wanajuana vizuri na huwa wanataniana kutokana na aina ya maisha waliyotengeneza hapo nyuma. Hivi karibuni Zumo na Habiba wamekuwa wakitaniana kwa kuchapisha picha za zamani ‘Instagram’ ambazo kimsingi zinafurahisha, Zumo anasema wanakutana na maoni mengi hasi lakini hayawezi kuharibu ndoa yao.

MAISHA YAKE KABLA

Zumo anaweka wazi kuwa hakupenda kusoma, hivyo aliamua kuingia kwenye masuala ya ufundi magari na alianza kuwa dereva wa teksi kabla ya kuwa dereva wa mabasi yaendayo mikoa ya Kusini. Zumo anasema amewahi kuendesha daladala la Mwenge kwenda Mbagala, pamoja na Ubungo kwenda Msata, anasema baada ya kupita humo aliamua kuingia kwenye vichekesho kupitia mtandao wa ‘Instagram’ na kwamba kama asingekuwa mchekeshaji maarufu nchini, huenda angekuwa fundi magari.

KUINGIA RASMI KWENYE SANAA

Zumo anafunguka kuwa baada ya shughuli zote za kimaisha, rafiki yake wa karibu anatambulika kama Oscar Martin ndiye aliyemshawishi kuingia kwenye uchekeshaji, baada ya kumwambia kuwa ana uwezo mzuri. Baada ya kumwagiwa sifa hizo, Zumo aliamua kuingia mazima kwenye sanaa na hapo ndipo alianza kuchekesha kwa video fupi na baada ya hapo vituo vya habari vilipenda kazi zake.

ANAOWAKUBALI KWENYE SANAA

Haji Mboto ni mchekeshaji namba moja wa Anko Zumo, anasema pamoja na uwepo wa wachekeshaji wengi nchini, lakini namba moja wake anabaki kuwa Mboto. Katika upande wa wanamuziki, Zumo anasema anamkubali sana Khadija Kopa na kwamba yani ameanza kumkubali muda mrefu sana na anapenda staili ya uimbaji wa mashairi yake.

ALICHOKIONA KWENYE SANAA

Zumo anaendelea kufunguka kuwa, kuna changamoto ameziona, anasema kinachowaangusha waigizaji wengi ni kutokuwepo kwa soko la kuuzia kazi zao, hali hiyo inafanya baadhi ya wasanii wasiumize kichwa kwenye ufanyaji wa kazi zao. Zumo anashauri Serikali iingilie kati kwa kuweka soko, ambalo litaamua kununua kazi nzuri tu na kuacha zile ambazo hazina ubora, bila kujali mhusika wa hizo kazi sizisokuwa na ubora.

ULINZI KWA MAI

Zumo anasema atahakikisha Mai anabaki katika maadili ambayo kwa sasa analelewa, atahakikisha wanasimama imara kuhakikisha Mai anabaki kwenye mstari, hata hivyo anaongeza kuwa baada ya Mai kukua atamuacha achague anachopenda kufanya, kwa msingi wa maadili. Zumo anakubali kuwa baadhi ya watoto wanalelewa vizuri, lakini mwisho wa siku watoto hao wanabadilika baada ya kukua, kwa upande wake anasema Mai atahakikisha anabaki kwenye aina ya maisha anayopitia kipindi hiki.

CHANGAMOTO KWA HABIBA

Zumo bwana anajifanya ‘Shahrukh Khan’ et anakwambia akaunti ya ‘Instagram’ ya mke wake anayo na yake anayo mke wake, hivyo changamoto ya mke wake kutumiwa jumbe za ajabu lazima azione ila anatulia kwanza. Anasema hiyo ni moja ya changamoto ndogo ila hamna tatizo, mambo yanaenda sawa, hata hivyo kuwa wakati wanapishana mawazo wakati wa kufanya kazi zao na kwamba hizo ndio changamoto ndogo ndogo alizonazo.

foto
Mwandishi: Rahimu Fadhili

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi

Kila mchezaji wa kigeni mil 4

masaa 21 yaliyopita Rahel Pallangyo

KLABU ya ...

Kila mchezaji wa kigeni mil 4

masaa 21 yaliyopita Rahel Pallangyo

KLABU ya ...

Simba yamuwekea kizuizi Senzo Yanga

masaa 21 yaliyopita Mohammed Mdose

SIKU moja ...