loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Lukuvi ataka maelezo vijiji vinavyochipukia kuwa miji

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi (pichani) amewataka Maofi sa Mipango Miji nchini kuzisaidia wilaya kuhakikisha maeneo yote ya vijiji yanayochipukia kuwa miji anapelekewa ili ayatangaze kuwa maeneo ya Mipango Miji.

Lukuvi alisema hayo jana wakati akizindua ofisi ya ardhi mkoa wa Kigoma, ikiwa ni mfululizo wa uzinduzi wa ofisi za ardhi katika mikoa mbalimbali nchini. Tayari ofisi za ardhi kwenye mikoa ya Tanga, Arusha, Manyara, Singida, Iringa, Njombe, Songwe, Rukwa, Katavi zimezinduliwa.

Alisema wizara yake kwa sasa ina mpango wa kupima kila kipande cha ardhi nchi nzima sambamba na kuhakikisha maeneo yanapangwa ili kuepuka ujenzi holela.

“Maeneo yote ambayo vijiji vinachipukia nileteeni nitangaze kuwa maeneo ya mipango miji na maofisa mipango miji mzisaidie wilaya katika hili,” alisema Lukuvi.

Kwa mujibu wa Waziri Lukuvi, baada ya maeneo hayo ya vijiji vinavyochipukia kutangazwa maeneo ya mipango miji wananchi wake hawatapewa tena hati za kimila na badala yake watapata hati za miaka 99 kama wanavyopata watu wanaoishi mijini.

Alisema mpango wa kuyatangaza maeneo hayo ya vijiji inavyochipukia siyo lazima uanzie wizarani bali Maofisa Mipango Miji katika halmashauri za wilaya wanatakiwa kuyawahi mapema ili kuepuka ujenzi holela.

Akizungumzia utendaji kazi katika ofisi za ardhi za mikoa, Waziri Lukuvi alisema ofisi hizo zimekamilikia kutokana na kuwa na wataalamu wa fani zote kama vile Upimaji, Uthamini, Mipango Miji pamoja na Usajili wa Hati na kubainisha kuwa vifaa vya kisasa vya upimaji navyo vimepelekwa kwenye ofisi hizo na sasa mwananchi halazimiki kufika wizarani kwa kuwa huduma zote zinapatikana ofisi za mikoa.

Kuhusu upungufu wa watumishi wa sekta ya ardhi kwenye halmashauri za wilaya, Lukuvi alisema kuwa baada ya kupeleka watumishi ngazi ya mkoa, zoezi linalofuata ni kuwapanga upya watumishi katika ngazi ya halmashauri kwa kuzingatia wataalamu wa fani zote.

Akigeukia suala la utoaji hati miliki za ardhi nchini, Lukuvi aliagiza wananchi wote waliopimiwa ardhi kwenye mkoa wa Kigoma kwenda ofisi za halmashauri za wilaya kuomba kutengenezewa hati na kubainisha kuwa, atakayeshindwa baada ya siku tisini atapelekewa hati ya malipo na kudaiwa kuanzia tarehe aliyopimiwa kiwanja chake.

Kwa mujibu wa Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Kigoma, Chediel Mrutu, mkoa huo una wamiliki wa viwanja 14,746 ambao hawajachukua hati zao pamoja na kukamilika taratibu zote za umilikishwaji ikiwemo kuwekewa alama, jambo linaloikosesha serikali mapato sambamba na wamiliki wake kukosa fursa za kiuchumi zinazotokana na kuwa na hati miliki.

WANACHAMA wa vyama vya ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu, Kigoma

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi