loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wakulima wasipangiwe bei ya kuuza mazao

KATIKA miaka ya karibuni msimu wa mavuno kumekuwa na watu wanaojitokeza kuwalaghai wakulima kisha kuwapangia bei za kuuza mazao yao, badala wao wenyewe kufanya hivyo kutokana na nguvu waliyoiwekeza.

Jambo hilo sio zuri, kwa sababu linamfanya mkulima ajisikie mpweke kwenye mazao yake mwenyewe, kwa kushindwa kupanga bei anayoitaka kutokana na nguvu aliyoiwekeza.

Ndio maana katika siku za karibuni Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga akifungua Maonesho ya Kilimo Biashara 2020 yaliyoandaliwa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (Tari) Kituo cha Ilonga wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro, alionya tabia hiyo inayofanywa na baadhi ya watu.

Hasunga alisema hao watu wanaojitokeza kipindi cha mavuno na kuwapangia wakulima bei, wawaachie wakulima wapange wenyewe bei wanayoitaka ili iweze kuwapatia faida. Hasunga alisema hayo akiwa katika kijiji cha Majambaa Kata ya Msowero wilayani Kilosa baada ya kupokea malalamiko mbalimbali kutoka kwa wakulima.

Jambo hilo si la kupuuzia, kwani kiuhalisia wakati wa kulima wakulima wanalima wenyewe, lakini wanapoanza kuuza watu hao hujitokeza na kutoa masharti magumu ya kuwazuia kufanya biashara.

Ifike mahali sasa mkulima asisumbuliwe na mtu yeyote, bali aachwe afanye biashara kwa uhuru, auze popote anapoona panafaa na sio kupangiwa bei.

Kitendo cha kuwadhulumu wakulima ambao wametumia nguvu, muda na fedha ili kuvuna mavuno yao, hakikubaliki hata kidogo.

Kwa ujumla kilimo ni sekta muhimu katika maendeleo na uchumi wa wananchi na taifa, hususan katika kuufikia uchumi wa kati ambao msingi wake mkubwa ni viwanda.

Mbali na kuwaacha wakulima kupanga bei zao kwa uhuru, pia huu ni wakati muafaka wa kutumia teknolojia bora, zinazoleta matokeo chanya, ikiwa ni pamoja na kutumia mbegu bora zinazozaa kwa wingi na kutoa mazao mengi, ili wanapoyauza yalete faida kubwa.

Pia wakulima wasichoke kutafuta utaalam, ujuzi na teknolojia bora kutoka kwa watafiti mbalimbali wa kilimo nchini.

Kwani hivi sasa Tari ipo kwa ajili ya kuhaulisha teknolojia kwa wakulima, ili waweze kupata mazao bora yenye tija, hivyo kuondokana na kilimo cha kujikimu na kwenda kwenye kilimo cha biashara.

Wakulima wakitumia mbegu bora na teknolojia za kisasa, uchumi utaongezeka kwa mkulima mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

WAKATI zikiwa zimebaki siku ...

foto
Mwandishi: Lucy Ngowi

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi