loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Ataka uwekezaji zaidi kukabili umasikini

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, anayeshughulikia Uwekezaji, Angela Kairuki amewataka wawekezaji nchini kupanua wigo wa ajira kwa vijana na wanawake ili kuendana na Sera ya Serikali ya awamu ya tano ya kupambana na umasikini.

Waziri Kairuki alitoa wito huo jana wakati alipotembelea kiwanda cha kusindika mboga mboga na matunda cha Darsh Industries Limited (DIL), kilichopo mjini Arusha.

“Malengo ya serikali ni kuhimiza ujenzi wa viwanda ili kupanua wigo nafasi za ajira kwa wananchi wetu ili waweze kuondokana na hali ya umasikini,”alisema Kairuki.

Waziri huyo pia alizitaka halmashauri zote nchini kutenga ardhi na maeneo maalumu kwa ajili ya kilimo cha kisasa za mboga na matunda na wakulima wajiunge katika vikundi ili waweze kufikiwa kwa urahisi na maofisa ugani.

“Tuna ardhi ya kutosha yenye rutuba, tuna maji ya kutosha ya kufanya umwagiliaji, wakulima wetu wakielekezwa na kusimamiwa vizuri hawana tatizo,”alisema Kairuki.

Waziri huyo aliongeza kuwa, “naomba pia niwapongeze Darsh Industries Ltd kwa kuitangaza taswira ya nchi yetu kimataifa, na sisi kama serikali tunawahakikishia kuwa changamoto zinazowakabili zitafanyiwa kazi na kupatiwa ufumbuzi wa kudumu.”

Mkurugenzi wa kampuni hiyo ya (DIL), Bhadresh Pandit alisema kiwanda hicho kilichoanzishwa mwaka 1999 kina uwezo wa kuzalisha tani 15,000 kwa mwaka za bidhaa hizo ambazo zinatambulika na shirika la viwango la kimataifa la ISO.

“Kiwanda chetu cha Iringa kina uwezo wa kusindika tani 200 za nyanya kwa siku na ndiyo kiwanda pekee cha kutengeneza Tomato Paste katika ukanda wa Afrika Mashariki…kabla ya ujenzi wa kiwanda cha Iringa tulikuwa tunalazimika kuagiza Tomato Paste kutoka Uchina na kutumia fedha nyingi za kigeni lakini sasa tunatengeneza hapa kutosheleza mahitaji ya malighafi ya kiwanda chetu na pia tunauza nje katika nchi za Zambia na Kenya na nchi nyingine kama Oman na Jordan zimeonyesha nia ya kununua kutoka kwetu,”aliongeza.

Kampuni ya DIL inamiliki viwanda viwili vya kusindika mboga na matunda katika mikoa ya Arusha na Iringa na pia ina kiwanda maarufu kinachozalisha bidhaa za RedGold.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo viwanda hivyo viwili kwa pamoja vimetoa ajira rasmi kwa Watanzania zaidi ya 400 ambapo kati yao asilimia 70 ni wanawake na asilimia 30 ni wanaume na ajira zisizo rasmi zaidi ya 3,000 katika sekta kama ya wakulima wadogo wadogo,wasafirishaji, wabeba mizigo, wasambazaji, na wauzaji.

Aidha Pandit pia aliiomba serikali kuangalia uwezekano wa kupunguza au kuondoa kodi kwenye bidhaa ua malighafi na vifungashio ambavyo havizalishwi Tanzania,kama makopo, chupa za kuhifadhia bidhaa.

“Tumia teknolojia za kilimo na utawala bora kwa ukuaji wa ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu, Arusha

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi