loader
Mwanamke mpambanaji anavyotamani gari la Serikali

Mwanamke mpambanaji anavyotamani gari la Serikali

MIONGONI mwa vitu vinavyoweza kututofautisha binadamu ni namna tunavyopokea changamoto na kuzishughulikia ili mwisho wa siku maisha yaendelee hata baada ya changamoto kupita.

Changamoto ni hali yoyote ya mazingira kinzani au ya upinzani ambayo mtu anakumbana nayo kinyume cha mategemeo.

Ni aina ya vikwazo au vipimo ambavyo vinainuka katika maisha ya mtu kwa lengo la kumpima. Hata hivyo kadri mtu anavyoendelea kuishi ndivyo anavyoendelea kusheheni uzoefu katika maeneo mbalimbali ya maisha.

Yapo mambo mengi ambayo hata shuleni hayafundishwi ila kupitia maisha tunapata maarifa na uzoefu mkubwa. Kupitia changamoto mtu anayo fursa adimu ya kujifunza na kuimarika ikiwa atafaulu kuvuka hiyo changamoto na kuwa na maarifa ya kujisaidia na kusaidia watu wengine.

Fatuma Masoud (25) ni mwanamke aliyepitia changamoto nyingi ambazo kwake alizitumia kuwa ni fursa iliyomuwezesha kutoka katika ugumu wa maisha yake na kuwezesha kusaidia familia yao .

Anazungumza na mwandishi wa habari wa safu hii , namna alivyokabiliana na ugumu wa maisha baada ya kushindwa kuendelea na elimu ya sekondari hali iliyochangikiwa na hali duni ya maisha ya familia yao kijijini Pawaga ,mkoa wa Iringa.

Anasema kutokana na ugumu wa maisha ya familia yao alikatsiha masomo ya sekondari akiwa kidato cha tatu mwaka 2013 na kuamua kuondoka kijijini kumfuata dada yake aliyekuwa anaishi mkoani Morogoro akifanya kazi ya uuguzi kwenye hospitali ya Mzinga ili kujaribu maisha mengine .

Fatuma anasema licha ya kuushi na dada yake aliamua kujitafutia maisha yake kwa kuanza kufanya kazi ndogo ndogo ili kujipatia riziki badala ya kuendelea kumtegemea kwa kila kitu dada yake huyo .

Kujitosa biashara ya kukanaga chipsi na kutembeza bagia mitaani.

Anasema kazi ya kwanza kuifanya akiwa mtaani ni kufungua genge na kupika chipsi, bagia na kuzitembeza mitaani kwa lengo la kujipatia kipato cha kijikimu kimaisha .

“Hii biashara ya kutembeza bagia mitaani niliona ni ngumu ndipo nilifikiria niende kuomba kazi kwenye magari ya daladala kuwa kondakta… nilienda kuomba kazi ya ukonda kwenye daladala, dereva mmoja nilipomueleza jambo hili alinikubalia na nikaanza kazi kama kondakta msaidizi wa daladala (Coaster ) mwaka 2014,” anasema Fatuma.

Anasema kuwa mara baada ya kupata kazi hiyo aliamua kuachana na shughuli za kupika chipsi na bagia kwa ajili ya kuzitembeza mitani ili kujipatia kipato.

“Namshukuru Mungu dereva aliyenipokea, alinipangia kazi ya kuwa kondakta msaidizi na miongoni mwa kazi zangu zilikuwa ni kuita abiria , kutangaza vituo kufungua na kufuga mlango ila sikuwa kondakta wa kupokea au kuchukua fedha kwa abiria,” anasema Fatuma.

Anasema wakati alipoanza kufanya kazi kwenye daladala kama kondakta mzaidizi , watu wengi hasa abiria, walimshangaa na walimchukulia kuwa ni mwanamke wa aina ya tofauti na wengine.

“Kiukweli si rahisi kwa mkoa wetu wa Morogoro , watu walikuwa bado na hadi sasa wengi wanaamka sasa, watu wengi bado wana uzito wa kuelewa na waliendelea kunishangaa , wengine waliniona ni mhuni , mshamba , walinidharau lakini mimi sikujali sana hayo,” anasema Fatuma.

Pamoja na hayo anasema kazi ya ukondakta msaidizi aliifanya kwa kipindi cha mwaka mmoja katika magari tofauti ya daladala .

“Namshukuru Mungu niliielewa kazi hii kwa kukomaa mwenyewe kama kondakta msaidizi na kipindi hicho cha mwaka mmoja nilikuwa nikijiwekea akiba ya fedha kwani niliamini kazi ya ukondakta si ya kudumu kwani nitahitaji kubadili maisha ya kazi,” anasema.

Kwa mujibu wa Fatuma wakati wote huo alikuwa akihangaika huku na kule kufanya kazi katika daladala tofauti, mawazo yake yote yalikuwa ni kumpata dereva mzuri atakayeweza kumfundisha kuendesha gari .

“Nilipata dereva ambaye alikubali kunielekeza namna ya kuendesha gari, niliweza kujifunza udereva kwa kusoma kozi ya awali na baadaye kwenda kusoma VETA na kupata leseni ya kuendesha magari madogo ya abiria,” anasema .

Baada ya kupata leseni ya kuendesha magari madogo ya abiria alijaribu kuhangaika kupata gari , lakini hakuweza kufanikiwa na ilimlazimu kufanya kazi ya ‘udeiwaka’ kama dereva msaidiziwa baadhi ya daladala za Manispaa ya Morogoro.

“Namshukuru Mungu wakati ninafanya kazi ya ukondakta kwenye moja ya daladala , bosi mwenye gari hiyo aliniamini baada ya kumueleza kuwa mimi ni dereva kamili, aliniamini na kunipatia gari la kuendesha nikiwa dereva kamili,” anasema .

Fatuma anasemea mwaka 2015 alianza kazi ya udereva na aliendesha daladala ya kwanza aliyokabidhiwa kwa kipindi cha mwaka mmoja. Hata hivyo, daladala hiyo ilipata ubovu na mmiliki wa gari alishindwa kuitengeneza na kuirudisha tena kufanya kazi za usafirishaji wa abiria.

“Nilianzaa kuendesha magari ya daladala mwaka 2015 na ni kampuni mbili pekee ndizo zimeweza kufanya nazo kazi na ya sasa ni Lillahil Hamdu na safari zake ni Manyuki- Mjini Moro na nafanya kazi hiyo hadi sasa,” anasema.

Fatuma anasema siri ya yeye kupata daladala la kuendesha kulitokana na uaminifu wake wakati akiwa kondakta na tabia hiyo ilimfanya mmiliki wa gari hilo kumuamini na kumkabidhi chombo hicho cha usafiri.

“Siku zote nimekuwa muaminifu kwa tajiri yangu, naye ananiamini , sijivuni , gari yake nina itunza ipo safi haijachunwa na kwa sasa kwenye kampuni hii nina miaka mitatu nafanya kazi ya udereva,” anasema.

Changamoto alizokaabiliana nazo Fatuma anasema changamoto zipo nyingi katika nyanja hiyo na kubwa inayomkera na haipendi kabisa ni dharau kwa mtoto wa kike akiwa yeye ni dereva mwanamke .

Anasema baadhi ya madereva hasa wa daladala wamekuwa wakimdharau tangu alipokuwa akifanya kazi ya ukondakta msaidizi , wengine ni kwa kumuonea wivu na anaongeza kuwa suala la dharau pia lipo kwa baadhi ya abiria.

“Baadhi ya madereva wanaona wivu na kunidharau kwa sababu tu ni mwanamke , wanafikia hata kunifanyia fujo (kuniwekea bodi ya gari) ili kunipima akili zangu , lakini sasa wamenizoea, kwani hizo vurugu zao hata mimi naziweza, sasa tunaheshimiana,” anasema.

Pia anasema, “baadhi ya makondata wanaume wanajiuliza kwa nini wanasimamiwa na dereva mwanamke , hivyo baadhi niliyofanya nao kazi walidiriki kuiba fedha ili nionekane kwa bosi sifanyi kazi , hili nimepambana nalo na huyu kondakta Leons Protas ni mzuri tunaelewana kwenye kazi.”

Malengo yake ya baadaye

Fatuma anasema matarajio yake ya baadaye ni kuwa na chuo chake cha kufundisha watu masuala ya udereva au kuwaelimisha wanawake waache woga na wapambane na maisha ili kufikia ndoto za malengo yao.

“ Tufanye kazi , tusimame kama wanawake , tusiwe waoga , napenda siku moja niwe na chuo changu cha kuwafundisha watu udereva au kuwaelimisha wanawae waache uwoga , tupambane , tuache woga,“ anasema.

Fatuma anaongeza kuwa, “nimetoka mbali na nina ndoto zangu, nimepitia changamoto nyingi na hapa siwezi kuzisema zote ninaweza kulia sana.”

Anasema pia anapenda sana kuendesha mabasi makubwa au magari ya serikali , lakini changamoto yake ni kushindwa kumaliza masomo ya sekondari baada ya kuishia kidato cha tatu na kuwa hana cheti cha kuhitimu kidato cha nne.

“Kiukweli nimetoka mbali sana na nina ndoto zangu toka nimekuwa dereva wa daladala, ninapenda sana kuendesha basi kubwa la abiria na kuendesha magari ya serikali lakini changamoto inayonikabili shule nilishia njiani kidato cha tatu kutokana na hali na maisha magumu ya familia yangu, kwa sababu nina mzani mmoja ‘baba’ anakaa kijijini Pawaga , Iringa,” anasema.

“Nimekuwa nikililia sana kupata kazi ya kuendesha magari ya serikali kwani huku sekta binafsi hasa daladala kuna changamoto nyingi , upatikanaji wa fedha ni mchache , magari ni mengi yananyang’anyana abiria. Unaamka mapema alfajiri , unafikiria fedha ya bosi , mafuta , kuitunza gari licha ya kupata fedha za kujikimu lakini si kivile,” anasema.

Fatuma anasema anatamani sana siku moja apate basi kubwa la abiria au gari ya serikali, lakini kwenye mabasi inabidi uwe na mtu wa kukushika mkono ili uweze kuaminiwa.

Anasema anapenda kuendelea na shule, lakini sasa hataweza kwa vile ana majukumu mengi hasa ya kumlea mtoto wake wa kike aliyemtaja kwa jina la Sabiha ,ambaye anasoma darasa la kwanza na anaishi na dada yake.

“Sina mume ninayeishi naye ila nimezaa mtoto mmoja wa kike yupo darasa la kwanza na nikienda shule sitaweza kupata fedha za kumsomesha mtoto , kwa sasa napambana kutafuta fedha kwa ajili ya kumsomesha mwanangu , kwani baba yake ni mtu wa hali ya chini na familia yangu pia ni ya hali ya chini,” anasema.

Ushauri kwa serikali

Fatuma anaishauri serikali iangalie makundi ya vijana walioshindwa kumaliza elimu ya sekondari na kupata cheti lakini wamekuwa na ujuzi wa fani mbalimbali za kusomea ili watambuliwe kusaidia kupata ajira zinazoweza kufanywa na watanzania hasa vijana .

Anasema kumekuwepo na fursa za ajira kwa wanawake ama vijana zikiwemo za udereva wale wenye kuwa na ujuzi waweza kutambulika na kuwezeshwa kupata ajira hizo licha ya kutokuwa na cheti za kidato cha nne .

“Wapo vijana wazuri katika fani fulani ikiwemo udereva , wamepitia Veta ,lakini wanakosa sifa ya kuwa na cheti cha kidato cha nne hawa wapewe upendeleo kwani cheti kisiwe kigezo cha ujuzi,” anasema.

Fatuma anasema yeye amekuwa ni muumini wa kauli mbiu ya Rais Dk John Magufuli anayosisitiza kuwa Hapa Kazi Tu na ile ya Watanzania chapeni kazi , kwani Rais yupo sahihi na hizo zimekuwa ni faraja kwake kufikia malengo yake ya kimaisha .

Pamoja na hayo anawashauri wanawake hawa vijana wasimame na kujitoa kufanya kazi badala ya kuwa tegemezi wa watu wengine wakiwemo waume zao hata kama wao wanafanya kazi. Historia yake fupi.

Fatuma Masoud ni miongoni mwa watoto wanne kati yao watatu ni wanawake na mmoja ni mwanaume na ni watoto wa mzee Abdi Masoud.

Alisoma shule ya msingi iliyopo katika kijiji cha Pawaga, Iringa Vijijini pamoja na sekondari katika kata hiyo, hata hivyo hakuweza kumaliza elimu yake na badala yake aliishia kiddato cha tatu kutokana na hali ngumu ya kifamilia.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/913a6c5174e0c367f02f1a2dacbbaf32.JPG

NCHINI Tanzania kuna matajiri wengi wakubwa walioanzia ngazi ...

foto
Mwandishi: John Nditi

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi