loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Handeni wataka viongozi wanaoendana na kasi ya JPM

UCHAGUZI Mkuu umekaribia, wananchi katika maeneo mbalimbali ikiwemo majimboni na katika kata wamekuwa na ndoto za viongozi wanaotaka kuwaongoza baada ya uchaguzi huo kwa kuhakikisha maeneo hayo yanapata huduma muhimu lakini majimbo hayo yanakuwa na maendeleo.

Tayari vyama vya siasa vimeanza michakato ya kupata wagombea wake katika nafasi mbalimbali na katika kufahamu ndoto za wananchi wa wilaya ya Handeni, gazeti hili lilitaka kufahamu ndoto waliyonayo wananchi hao hususan katika jimbo la Handeni mjini.

Imami wa Msikiti wa Bomani wilaya ya Handeni, Abdallah Mohamed anaeleza kuwa kwa mujibu wa dini inataka mtu anapotoa ahadi ahahakikishe anatimiza na hata anaposhindwa kutokana na changamoto mbalimbali ni vema akazungumza na wananchi na kueleza sababu.

“Hivyo katika uchaguzi ujao tutataka viongozi wanaosimamia ahadi zao na kuzitekeleza kama anavyofanya Rais John Magufuli kwa kila wakati kueleza alichofanya na lengo lake ili wananchi waweze kuelewa nia yake na wapi anataka kuifikisha nchi,” anasema.

Anabainisha kuwa hata kama kiongozi haonekani mara kwa mara anatakiwa kuwa mchapakazi na kusikiliza changamoto za wananchi wake.

Mohamed anatoa mawazo yake kuwa kwa sasa wanahitaji mabadiliko kama ikiwezekana vyama vya siasa kuwasimamisha wagombea wanawake kwani mara nyingi wanawake wanasimamia kile wanachoamini na mwanamke akipewa majukumu anahakikisha anakabili changamoto mbalimbali muhimu ikiwemo suala la maji,miundombinu na nyinginezo bila kusahau kuwa mama ni mlezi wa familia.

Shehe wa wilaya ya Handeni, Shabaka Kizulwa anaeleza kuwa inatakiwa kufanya ibada ili Mungu awaoneshe kiongozi mwenye kujali maslahi ya wananchi bila kuangalia udini kama ilivyo serikali jambo la msingi ni kuzingatia kazi.

Padre Joseph Sekija wa Parokia ya Handeni anapongeza serikali ya awamu ya tano kwa jinsi ilivyosimamia ahadi zake na kuleta maendeleo ya wananchi.

Anasema serikali na viongozi wa kisiasa katika wilaya hiyo wamejitahidi kufanya kazi kwa kadri walivyojaliwa kwani hata tatizo la maji kwa sasa angalau yanatoka katika maeneo ya pembezoni huku akitaka jitihada zaidi kumaliza changamoto hiyo.

Padre Sekija anasema jambo la muhimu katika kupata viongozi ni kufuata demokrasia huku watakaochaguliwa kufanya kazi kwa kasi na zaidi ya ilivyo sasa ili kuendana na kasi ya serikali ya awamu ya tano.

Mkazi wa wilaya hiyo katika eneo la Chanika, Kitwanga Kitwanga anabainisha kuwa kumekuwa na changamoto katika sekta ya umeme kwa transfoma kulipuka na kukatika umeme mara kwa mara pamoja na katika Hospitali za serikali suala la Kilini ya mama na mtoto malipo yake yakiwa hayawekwi wazi.

“Katika suala hili, kuna wakati tuliambiwa ni bure lakini sasa tunalipa na inapofika kupata dawa unaelekezwa duka la kununu hivyo ni vema viongozi kusimamia suala hili kama ilivyo maeneo mengine nchini tunapoona viongozi wanafanyia kazi.

“Anabainisha kuwa pia kuna changamoto ya maji kwa kukosa mifumo ya kuaminika , kukosekana kwa ajira kwa kufungwa migodi midogo iliyofungwa kwa zaidi ya miaka mitatu kadha ana vijana kuishia vijiweni,” anasema Kitwanga.

“Sisi tunataka kuwepo na mikutano ya wabunge na madiwani wetu ili kuweza kujadili kero zetu lakini hakuna mikutano mpaka kiongozi mkubwa wa nchi aje”analalamika mkazi wa eneo hilo la Chanika,” anasema Kalabaka Juma.

Kwa upande wa mkazi wa eneo hilo Sadiki Mbwana anataka serikali kuangalia upya suala ya bunge kuoneshwa moja kwa moja kwani inasaidia kufahamu mbunge wao jinsi anavyowawakilisha lakini sasa hakuna anayeelewa hata kama aliwasilisha hoja na haijafanyiwa kazi na serikali.

Mwenyekiti wa CCM ,wilaya ya Handeni, Athumani Malunda anaeleza kuwa hakika hakuna pepo bila ibada hivyo ikiwa viongozi waliopita hawajafanya vema ni ngumu kutarajiwa kurejea tena katika uongozi.

“Msiwatishe na kuwawekea wigo wenye nia ya kugombea nafasi za udiwani au ubunge kwani kila mwanachama wa CCM mwenye akili timamu ana nafasi ya kugombea nafasi yeyote,” anasema.

Mkazi wa Kata ya Kwamagome, jimboni humo, Tecla Mhina, anasema pamoja na serikali kutatua changamoto kadhaa walizokuwa nazo, bado wana changamoto nyingi ambazo hazijafanyiwa kazi.

Anasema wanatarajia kupata mbunge atakayeweza kuendana na kasi aliyonayo Rais Magufuli katika kutekeleza ahadi atakazoziahidi.

“Shida kubwa hapa hatuna maji safi… tunahangaika kupata maji, tunatamani mbunge atakayekuja aanze na hilo kwanza mengine yafuate,” anasema Tecla.

Anasema changamoto nyingine ambayo wanatarajia mbunge ajae kutatua ni eneo lao kukosa huduma ya umeme,mbunge kuwa karibu na kuvisaidia vikundi vya wajasiriamali hasa wanawake ambao wanajaribu kujinasua na umasikini. M

wananchi mwingine, Msingwa Lucas anasema changamoto nyingine ni ucheleweshwaji wa kuunganisha umeme wa Mradi wa Umeme Vijijini (REA) kwa wananchi ambao wanalipia.

Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Ng’ombe katika mnada wa Handeni, Abdi Mhandeni anawashauri wanawake kujitokeza kwa wingi kuchukua fomu za uongozi wa nafasi za ubunge katika jimbo hilo kwa kuwa wamekuwa wakionesha uwezo mkubwa wa kuongoza.

“Hata ukiangalia mawaziri wengi wanawake hawajamuangusha Rais Magufuli katika utendaji kazi wake na sisi tunatamani kama tungepata mbunge mwanamke,” anasema Mhandeni.

Katibu wa Mbunge anayemaliza muda wake, Kaboga Mkali, anasema kuna mafanikio makubwa yaliyopatikana katika miaka mitano ya uongozi wa mbunge Omari Kigoda.

Anaeleza kuwa kulikuwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa majisafi na salama ambapo walitumia Sh milioni 277 kukarabati miundombinu ya maji na kuanzisha vituo vingine.

“Tumeweza kuongeza upatikanaji wa maji katika jimbo kutoka asilimia 26 hadi kufikia 70 kupitia vyanzo tofauti vya mabwawa na visima,” anasema Kaboga.

Anasema changmoto ni kubomoka na kusombwa na maji mabwawa matatu ya kuhifadhia maji kati ya kumi yaliyopo jambo linalochangia kurudisha nyuma jitihada za serikali.

Kaboga anasema upande wa elimu wamepunguza changamoto kubwa iliyokuwapo ya vyumba vya madarasa pamoja na kusimamia udhibiti ubora wa elimu.

Anasema wamefanikiwa pia kujenga jengo la maabara katika hospitali ya wilaya ambalo linahudumia wilaya tatu za Mvomero, Kilindi na Handeni. Katibu wa CCM Wilaya , Salehe Kikweo anasema wanaamini watapata ushindi kwa kuwa wametekeza ilani ya CCM kwa asilimia zaidi ya 85.

Anasema chama hicho kinatarajia kuwa na wagombea wengi watakaochukua fomu kwa ngazi ya udiwani na ubunge kwa kuwa kuna udhoofu kwa upinzani katika wilaya hiyo.

Anatoa mfano kuwa mwaka 2015 kwa mujibu rejista ya Chadema ilikuwa na wanachama 3,959 lakini hadi kufikia uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka jana walibaki 104 na hivi karibuni wakati wa ziara ya Naibu Katibu Mkuu, Rodrick Mpogoro, karibu nusu ya waliobaki walirudi CCM.

Anasema kwa kuwa wanaohamia CCM nao ni wanasiasa watahitaji pia kugombea na kushiriki katika uchaguzi, hivyo mwamko ni mkubwa lakini anatoa onyo kwa wagombea ambao watakwenda kinyume na maadili ya chama hicho hasa suala la kutoa rushwa na kusema kuwa hawatawavumilia.

“Tunamshukuru Rais Dk John Magufuli kwa kupiga marufuku suala la rushwa ili wagombea watakaochaguliwa wawe na uwezo na wenye kuchaguliwa na wananchi kwa haki,” anasema Kikweo.

Anaeleza kuwa miradi ya maji barabara na huduma za kilimo imefikia asilimia 85,malalamiko ya kero za wananchi yamepungua huku kukiwa na amani na utulivu chini ya mkuu wa wilaya anayetoa ushirikiano mkubwa.

Anazungumzia changamoto ya maji kuwa inaendelea lakini siyo kama awali kwani katika mradi wa maji ndelema ,mashine zaidi ya 20 zimefungwa kupeleka maji mijini na juhudi za kukarabati mradi wenye chanzo cha maji Segera umekarabatiwa na baadhi ya maeneo kupata maji baada ya kupata fedha toka India na makandarasi wameishapatikana .

Anasema tatizo la maji litazidi kupungua kwani juhudi zinafanyika ili wilaya ya Handeni kijiografia ni wilaya kame hivyo ili watu wapate maji lazima maji yahame kutoka eneo moja kwenda lingine na kuletwa wilayani hapo kama ilivyo katika mradi wa kuvuta maji kutoka Ruvu mpaka mkata na ule wa Handeni Trunk Main HTM ukitarajia kukarabatiwa pamoja na mabwawa na visima virefu ili kupunguza tatizo la maji.

Pia, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Wilaya Awadh Chanyendo anasema katika uchaguzi ujao wananchi wanapenda kupata viongozi shupavu wanaosimamia demokrasia na uhuru wa kutoa mawazo.

Anasema katika uchaguzi ujao ni vema wananchi wakaachiwa kuchagua kiongozi wanaomtaka na katika hilo vyama vya upinzani vitasimama imara.

“Handeni tumeangalia maendeleo yetu tunatamani yawe kama yale ya Kilindi… kwa sasa ni bora tukamchagua mwanamke anaweza kutuwakilisha vema na kubadili jimbo letu na tayari CUF mgombea wetu mwanamke amechukua fomu,” anasema.. Chanyendo anasema jimbo hilo kwa sasa linahitaji kiongozi ambaye ataleta wazo la uwepo wa viwanda vingi ili kuzalisha ajira kwa vijana kwani hadi sasa kuna kiwanda kimoja tu cha chokaa.

BABA wa Taifa, Mwalimu Julius K Nyerere, ndiye Rais wa ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi