loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

'Gaucho' ahukumiwa kifo

ALIYEKUWA mjumbe wa Taasisi ya Muungano wa Jamii Tanzania (Mujata), mkazi wa Nyamongo Tarime Mjini, Mwita Phillipo, maarufu kama ‘Gaucho’, amehukumiwa kunyongwa hadi kufa.

Amepewa adhabu hiyo baada ya kupatikana na hatia ya kushiriki katika mauaji ya kukusudia ya wanawake wawili wa familia moja.

Wanawake waliouawa ni wakazi wa Kijiji cha Kemange Kata ya Nyandoto, Robhi Mang’enyi (45) na wifi yake, Blasia Mahende (34).

Wanawake hao walivamiwa nyumbani kwao usiku na kukatwakatwa mapanga na kupigwa nondo sehemu mbalimbali mwilini, hivyo kusababisha vifo vyao. Hukumu ya kesi hiyo ilisomwa juzi na Jaji wa Mahakama Kuu, Ephery Kisanya.

Jaji Kisanya alisema kuwa ameridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka bila ya kuwa na shaka yoyote na anamhukumu Phillipo kunyongwa hadi kufa, kutokana na kupatikana na hatia ya kushiriki katika mauaji ya wanawake wawili wa familia moja kwa kukusudia, kwa kuwakata mapanga na nondo wakati wakiwa wanakula nyumbani kwao usiku, huku mama wa familia hiyo akishuhudia mauaji hayo.

Awali, wanasheria wa serikali, Donasian Chuwa na Peter Ilole walidai mahakamani hapo kuwa Februari 10, mwaka jana Phillipo akiwa na wenzake watatu, akiwemo Tano Chacha na wawili ambao hawakufahamika, wakiwa na silaha za jadi, mapanga na nondo, walivamia nyumbani kwa Charles Wambura na kuwakuta Robhi, Blasia na mama mkwe wa Rhobi na mama mzazi wa Blasia aitwaye Nyanchama Chacha (76) wakila chakula pamoja na kuanza kuwashambulia kwa kuwakata mapanga.

Robhi alikatwa kwa panga shingoni na begani na kuvuja damu kwa wingi na kusababisha kifo chake. Blasia alichomwa na nondo yenye ncha kali sikioni na kuingia ndani na kusababisha kuvuja damu kwenda kwenye ubongo na kusababisha kifo chake.

Nyanchama alikatwa kichwani kwa panga na kujeruhiwa vibaya.

Nyanchama alipiga yowe kuomba msaada kutoka kwa majirani, ambao walijitokeza kutoa msaada. Mashahidi watatu walieleza kuwa marehemu waliuawa kwa kukatwa mapanga na kuchomwa nondo yenye ncha kali.

Fomu za kitabibu pia zilionesha wanawake hao waliuawa kwa kukatwa mapanga na kuchomwa na nondo yenye ncha kali.

Watuhumiwa wawili, kati ya wanne, walitambuliwa akiwemo Phillipo na Tano Chacha, ambaye alitoroka baada ya tukio hilo.

Wenzake wengine pia hawajapatikana hadi sasa. Nyanchama alidai kuwa anamfahamau Phillipo, kwani alikuwa akifika nyumbani hapo akiwa na na Tano. Mashahidi wengine, Joice na Wambura, waliwatambua pia Phillipo na Tano kuhusika na kuwepo katika tukio hilo la mauaji hayo.

Mawakali hao wa serikali, Donasian na Ilole, waliomba mahakama kutoa adhabu kali kwa watuhumiwa hao kwa kufanya mauaji ya kukusudia. Phillipo alikuwa akitetewa na mawakili wawili, Leonard Magwayega na Paulo Kibeja.

Shahidi mwingine alikuwa mke wake, aliyedai kuwa Februari 10 mwaka jana saa 2 hadi saa 4, mumewe(Phillipo) alikuwa kwenye biashara zao za grosali ya Mujata akiangalia mpira. Alidai kuwa mumewe hakuhusika na tukio hilo.

Mtuhumiwa mwenyewe alikiri kuwa Tano ni rafiki yake na alikuwa anataka kumuuzia gari lake aina ya Noah. Baada ya kusikiliza mashahidi wa pande zote mbili, akishirikiana na Wazee wa Baraza, Jaji Kisanya aliungana na upande wa mashitaka na kumtia hatiani mtuhumiwa Phillipo, kwa makosa mawili ya kuvamia na kuua.

“Mahakama hii inakuhukumu kunyongwa hadi kufa. Una siku 30 za kukata rufaa kama utaona hukutendewa haki,” alisema Jaji Kisanya.

Pia wadau mbalimbali walichanga hadi ujenzi ukafikia hatua ya kuezekwa ...

foto
Mwandishi: Samson Chacha, Tarime

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi