loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Waziri aliyebaki wa Baraza la kwanza la Nyerere afariki

MWILI wa aliyewahi kuwa waziri katika Baraza la kwanza la Mawaziri la Serikali ya Awamu ya Kwanza chini ya Mwalimu Julius Nyerere, Balozi Job Lusinde aliyefariki dunia jana katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili- Mlonganzila , Dar es Salaam utasafi rishwa leo kuelekea Dodoma, kusubiri taratibu za maziko yake.

Taarifa ya kusafirishwa kwa mwili huo, zimetolewa na mdogo wake, John Malecela , ambaye ndiye Msemaji wa Familia. Alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake, jana.

Alisema kwamba kwa kuwa kaka yake alifariki dunia jana, ukoo bado haujakutana na kwamba ukishakutana tarehe ya maziko itaelezwa. Alisema kwamba mwili wa marehemu, utahifadhi wa mochwari Dodoma wakati familia inajadiliana namna ya kumhifadhi ndugu yao.

Ofisa Uhusiano wa Hospitali ya Mloganzila, Neema Mwangomo alisema Lusinde alifariki jana saa 12:42 asubuhi na alifikishwa hospitalini hapo tangu Juni 16, 2020.

Malecela ambaye aliwahi kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania kuanzia Novemba 1990 hadi Desemba 1994, alisema kwamba kutokana na ukaribu wa kaka yake na jamii na serikali katika utumishi wake wa muda mrefu tangu akiwa katika baraza la kwanza la mawaziri la Tanganyika huru, itachukua muda kujadili mazishi yake.

Malecela alisema kwamba atamkumbuka kaka yake kutokana na msaada mkubwa, alioutoa kwake na kwa jamii kwa ujumla. Alisema kwamba ndugu yake alianza kuugua kuanzia Februari mwaka huu na alitibiwa Hospitali ya Benjamin Mkapa mjini Dodoma kisha kupewa rufaa kwenda Muhimbili-Mloganzila, Dar es Salaam.

Kwa upande wake, Peter Mavunde alisema kwamba amefika nyumbani kumsalimu Sara Lusinde na kumpa pole kutokana na msiba huo. “Sikutarajia kwamba akiondoka mzee hatarejea”, alisema Mavunde ambaye alishiriki kumpandisha ndege kwenda kwenye Muhimbili-Mlonganzila.

Alisema kwamba Lusinde ana upekee wa aina yake katika wale waliohudumu. Alisema kwamba atamkumbuka kutokana na uaminifu wake katika mambo mengi aliyofanya, ikiwa kuhudumia Kanisa Anglikana. Alisema kuwa Lusinde alikuwa ni mfano wa kuigwa kwa uchapakazi. Pia, alikuwa mwanasiasa mahiri kwa kusimamia na kuimarisha Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Mavunde alisema kuwa Lusinde ndiye aliyefanya aingie katika siasa na alianzia uenyekiti wa kata hadi udiwani na kisha Meya wa Dodoma. Alisema Balozi Lusinde amefanya mambo mengi mazuri kwa umma na jamii. Aliomba Mungu aipokee roho ya marehemu peponi. Wengine waliokuwepo katika msiba ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu), Antony Mavunde ambaye alisema kwamba amepokea kwa masikitiko makubwa kifo hicho.

Alisema mzee huyo alikuwa sehemu ya busara kwa vijana wengi na hasa juhudi zake za kuipenda Dodoma kwa moyo wake wote. Alisema alikuwa wa kwanza, kumshawishi kuwa mbunge wakati alipoomba kwa mara ya kwanza akiwa na miaka 25. Alijenga mazingira na kipindi cha pili akapata ubunge. Alisema anatumaini kwamba fikira zake zitazidi kudumu. Lusinde alishawahi kuwa mbunge wa Dodoma Mjini.

Lusinde ni nani? Lusinde ambaye ni mwenyeji wa mkoa wa Dodoma, alizaliwa Septemba 10 mwaka 1930 eneo la Kikuyu mjini Dodoma. Ni mmoja wa Watanzania walioanzisha vuguvugu la kudai Uhuru.

Desemba 9, 1961 Tanganyika ilipopata Uhuru, alikuwa mmoja wa mawaziri 11 wa kwanza wa Tanganyika. Baraza hilo lilikuwa na Waafrika wanane, Wazungu wawili na Mhindi mmoja.

Katika baraza hilo la kwanza, Waziri Mkuu alikuwa Mwalimu Julius Nyerere na Waziri asiye na Wizara Maalumu alikuwa Rashid Kawawa; Waziri wa Elimu, Oscar Kambona; Waziri Serikali za Mitaa Job Lusinde; Waziri wa Mawasiliano, Nguvu za Umeme na Ujenzi, Amir Jamal na Waziri wa Biashara na Viwanda, Nsio Swai.

Wengine ni Waziri wa Ardhi na Upimaji, Tewa Saidi Tewa; Waziri wa Sheria, Abdallah Fundikira; Waziri wa Afya na Elimu Derick Bryson; Waziri wa Kilimo, Paul Bomani; Waziri wa Fedha, Ernest Vassey na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Kahama.

Vilevile, alishiriki kikamilifu matayarisho ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na alishuhudia utiaji saini wa Hati za Muungano Aprili 22, 1964. Alihudumu katika wizara tofauti, ambapo kuanzia 1961-63 alikuwa Waziri wa Serikali ya Mitaa, 1963-65 (Mambo ya Ndani), 1965-67 (Mawasiliano, Ajira na Kazi), 1967-70, (Mawasiliano, Uchukuzi na Ajira) na 1970- 74 (Mawasiliano na Kazi ) na 1974-75 (Kazi).

Pia alikuwa Waziri wa Kwanza wa Mambo ya Ndani wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Oktoba 6, 1975 aliteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini China. Alihudumu huko hadi Septemba 1984 alipoteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Kenya. Mei 19 mwaka huuu Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alimtembela Lusinde na kumjulia hali nyumbani kwake Uzunguni jijini Dodoma.

Imeandikwa na Sifa Lubasi, Dodoma na Lucy Lyatuu, Dar.

Pia wadau mbalimbali walichanga hadi ujenzi ukafikia hatua ya kuezekwa ...

foto
Mwandishi: Waandishi Wetu

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi