loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

‘Mkara’ wa Nyerere, hatma urais Z’bar na mrithi JPM 2025

“SASA kumekucha, sasa kumekucha, jogoo limekwishawika Dodoma… Kada wa CCM apewe kura za ndiyo. Yuko wapi, yule pale, yule pale, yule pale mnamuona.. kada wa CCM, apewe kura za ndiyo. JPM amechukua, ameweka, waah…CCM eh shangilia ushindi unakuja!”

Hivyo ndivyo mambo yatakavyokuwa Dodoma mwisho wa wiki Chama Cha Mapinduzi (CCM) kitakapofanya vikao vya uteuzi wagombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar katika ukumbi wa kimataifa wa Kikwete.

Wimbo huo unatarajiwa kuhanikiza wakati wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa watakapokuwa wakimpitisha kwa kishindo, Rais John Magufuli kupeperusha bendera ya CCM kuwania urais katika muhula mwingine Julai 11.

Hadi siku ya mwisho ya kurejesha fomu za kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM, ni Rais Magufuli pekee aliyekuwa amechukua na kurejesha fomu CCM.

Kutokana na hali hiyo, Kamati Kuu (CC) ya CCM inatarajiwa kujadili jina lake, kulipendekeza kwa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM ili wajumbe waliidhinishe kwenda Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM kupigiwa kura na wajumbe.

JPM anapeta akisubiri kupeperusha bendera ya CCM uchaguzi mkuu. Akiwa amedhaminiwa na wanachama zaidi ya milioni moja wa mikoa ya Tanzania Bara na Visiwani Zanzibar, ana uhakika wa kupitishwa kwa kishindo kuwania tena urais.

Wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema, changamoto yake kama Mwenyekiti wa CCM Taifa ni atakavyosimamia uteuzi wa mrithi wa Rais Ali Mohammed Shein anayemaliza muda.

Changamoto hiyo inafuatia ukweli kwamba, mgombea atakayependekezwa na kupitishwa na NEC kupeperusha bendera ya CCM Zanzibar anaakisi urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ni kwa sababu hiyo, macho na masikio ya Watanzania wengi na jumuiya ya kimataifa yanaelekezwa Zanzibar kwani Rais huyo ni mtu muhimu wa ustawi wa Muungano wa Tanzania.

Je, kati ya wagombea 31 kati ya 32 walioomba urais Zanzibar na kurudisha fomu na mwishoni mwa wiki kujadiliwa na Kamati Maalumu ya NEC Zanzibar, nani atapitishwa na NEC Taifa kupeperusha bendera ya CCM Zanzibar 2020?

Hilo ndilo swali baada ya Kamati Kuu Maalumu Zanzibar kuchuja wagombea 31 na kupendekeza watano watakaojadiliwa na CC kabla ya watatu kati yao kupelekwa NEC Taifa kupigiwa kura.

Ingawa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Juma Abdallah Juma Mabodi alikataa kutaja watano waliopendekezwa kujadiliwa na CC, wachambuzi wa siasa wamebashiri waliopenya wakirejea siasa za uteuzi wagombea urais wa Zanzibar 2020 na mrithi wa JPM mwaka 2025.

Ni hapo ndipo wabashiri hao wanadhani na kuamini kuwa, huenda jina la Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Dk Hussein Mwinyi likawa moja ya majina. Wengine wanaodhaniwa kuwa huenda wamo katika ‘tano’ hiyo kuwa ni Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa, Khamis Mussa Omar, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Waziri wa zamani wa Fedha Zanzibar, Dk Khalid Mohamed Salum.

Mwingine ni mkongwe Shamsi Vuai Nahodha, Waziri Kiongozi mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais Dk Salmin Amour, Zanzibar na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mstaafu.

Wadadisi wa masuala ya siasa wanaobashiri wagombea hao kupitishwa wanaegemea siasa za Zanzibar na makandokando yake wakihusisha pia na siasa za mrithi wa JPM Muungano 2025.

Mfano, wanaamini ni muhimu kwa jina la Dk Khalid anayenadiwa kuwa chaguo kuwemo ili kuwaridhisha wanachama wanaomwona anafaa. Hata hivyo, Dk Khalid anatajwa kukabiliwa na changamoto ya kupenya tatu bora hadi mwisho kufuatia doa la kuondolewa kwenye uwaziri. Sababu zilizomfanya Rais Shein ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar amtoe kwenye uwaziri, huenda zikamrudi akijadiliwa.

Wanaodai anatosha ni wale wanaohusishwa na kundi la wanasiasa wanaotaka Zanzibar ipate mgombea wanayeamini atasimamia watakayo. Yupo pia Khamis Mussa Omar, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha ambaye muktadha wake katika siasa za Zanzibar na Bara hauko wazi.

Mussa na Dk Khalid wana changamoto moja inayofanana, wanakubalika Zanzibar, lakini wasifu wao katika siasa za Muungano si mkubwa. Kama watakuwa miongoni mwa walioteuliwa kwenda CC, huenda wakapungukiwa sifa za kupenya NEC kwa kuwa upigaji kura NEC unahusisha pia wajumbe kutoka Tanzania Bara.

Ni wazi kinyang’anyiro kinaonekana kuwa kikali zaidi kati ya Profesa Makame Mbarawa, Dk Hussein Mwinyi na Shamsi Vuai Nahodha. Wadadisi wa masuala ya siasa wanaowapa hao alama nyingi wanaegemea historia zao kisiasa na utendaji Zanzibar na Serikali ya Muungano.

Hata hivyo, kati yao Nahodha ndiye ana rekodi nzuri zaidi ya kuwahi kufanya kazi sehemu zote akiwa Waziri Kiongozi Zanzibar kwa miaka 10. Sababu nyingine inayompa nafasi ni kuwahi kwake kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano.

Wadadisi wa masuala ya siasa wanaamini kwa kufanya kazi kwake sehemu zote za Muungano, anapata fursa pana ya kufahamika kwa wengi. Kipimo kikubwa cha Vuai katika hili ni rekodi yake ya utendaji alipokuwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi yenye changamoto nyingi zaidi.

Wako wanaomwona kama mtu mpole mno na ambaye hakuacha alama Mambo ya Ndani na wako wanauona upole wake kama silaha kuu ya kumsaidia kuongoza kama alivyokuwa Shein.

Pamoja na yote, Shamsi ni zao la siasa za Dk Salmin Amour, Rais mstaafu mwenye ushawishi mkubwa na kuonekana akiwakilisha kundi hilo. Ni wazi, baada ya chaguo lao 2010, Dk Gharib Bilal kushindwa na Dk Shein, huenda safari hii kundi la uzao wa Dk Salmin Amour likapenya. Hata hivyo, kupenya kwao huenda kusiwe rahisi kwa mara nyingine kutokana na mgombea mwingine, Dk Mwinyi kuonekana tishio pia.

Dk Mwinyi ambaye ni mtoto wa Rais wa Tatu wa Zanzibar na baadaye wa awamu ya pili wa Jamhuri ya Muungano, Mzee Ali Hassan Mwinyi alitajwa kama ‘mrithi’ muda mrefu.

Mgombea huyo amewahi kuwa Waziri wa Afya wa Jamhuri ya Muungano, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano) na sasa ni Waziri wa Ulinzi. Kwa nyadhifa hizo hasa Ulinzi alikokaa muda mrefu zaidi, ameonekana machoni mwa watu wengi kama mtu aliyeandaliwa kumrithi Rais Dk Shein kwa sababu ya utii na upole wake. Hata hivyo, wakati watu wakisubiri tu apitishwe kirahisi NEC, lundo la wagombea lililochukua fomu liliashiria kuwepo kwa tatizo kwake pia.

Wadadisi wa masuala ya siasa wanakariri watu wasiomkubali wakidai, kinyume na wagombea wenzake, hakusomea wala kufanya kazi huko. Madai hayo na yale ya CCM Zanzibar kutaka Rais aliyezaliwa Zanzibar, mwenye nasaba hasa na huko na siyo kuhamia tu na wazazi wake ni sumu tosha kwenye safari yake ya urais huko.

Pamoja na hayo, Dk Mwinyi anabebwa na sifa za kukubalika zaidi katika siasa za Muungano akiwa amefanya kazi Wizara ya Muungano na pia Afya na Ulinzi ambayo pia ni ya Muungano.

Ndiyo maana pamoja na baadhi ya watu kujenga hoja ya kumtoa nje kwa madai hakusoma huko, CCM ikitafuta Rais, ina vigezo zaidi ya hivyo. Ni vigezo kama hivyo vilivyomfanya Rais Amani Karume aliyekuwa wa tano kwa wagombea waliopitishwa mwaka 2000, apitishwe Dodoma na kufanya Wazanzibari waliojua wana chaguo lao, wakasirike ‘kwa kuchaguliwa Rais’ Bara.

Pamoja na kasoro hiyo na kwa kurejea kauli ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Idd kuwa moja ya sifa ni kulinda Muungano, Dk Mwinyi bado anapewa nafasi ya kuteuliwa urais.

Hii inakolezwa na uzoefu mkubwa alioupata katika masuala ya Muungano na ulinzi, mambo makuu kwa uongozi wa Zanzibar na Muungano. Hata hivyo, Dk Mwinyi anakabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa Waziri wa Maji, Profesa Mbarawa aliyeibuliwa na Rais wa Awamu ya Nne, Dk Jakaya Kikwete na kukomazwa kwa utendaji bora Awamu ya Tano ya Rais Magufuli.

Profesa Mbarawa anayetokea Kisiwani Pemba kama alivyo Rais Shein; anapewa nafasi kubwa pia ya kuwa ‘tano bora’ na hatimaye kuteuliwa na CCM kupigiwa kura NEC kwa rekodi nzuri ya kazi. Akiwa Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi katika utawala wa Rais Magufuli, Profesa Mbarawa alisimamia miradi mikubwa ya ujenzi wa viwanja vya ndege, bandari, reli na kudhibiti mianya ya ulaji fedha.

Ameendelea kuonesha maajabu ya kazi nzuri alipohamishiwa Wizara ya Maji baada ya kunyoosha mambo ya miundombinu akifumua mikataba ya wakandarasi ‘iliyolala’ miaka mingi.

Profesa Mbarawa amekuwa gumzo hasa Bara kufuatia maji sasa kutoka kila kona ya nchi kiasi cha watu kumwona mmoja wa watu walioelewa somo la JPM na kufaa kumrithi mwaka 2025. Ni rekodi hiyo na ukweli kuwa, siasa Zanzibar zinahitaji mtu makini, aliyeiva kisiasa, utendaji kupambana na mgombea wa ACT Wazalendo aliyetangaza nia kwa mara ya tano ndani ya miaka 25, Maalim Seif.

Mgombea kutoka Pemba Wazanzibari wanaomwona Profesa Mbarawa chaguo sahihi; wanadai bado kunahitajika mtu makini, mwenye nguvu ya kumdhibiti Seif anayetoka Pemba pia kuua kabisa hoja yake (Seif) ya Mpemba kutoongoza iliyofifishwa na Dk Shein.

Profesa Mbarawa ni turufu nzuri kupumzisha siasa za Maalim Seif ambaye umri ‘umesonga’ akikosa sasa yatabaki majaliwa tu. Profesa Mbarawa huenda akawa mwanafunzi mzuri wa JPM kwani wanarandana staili za usimamizi rasilimali na umakini kazini.

Hata hivyo, Profesa Mbarawa ana kigingi cha ndoa akidaiwa mkewe ni raia wa kigeni hoja ambayo wengine wanaona ni dhaifu kwani mke anafundisha moja ya vyuo vikuu nchini na zaidi Mwalimu Nyerere aliwahi kukemea ubaguzi ukiwamo wa ugonjwa wa ukabila.

Katika moja ya hotuba zake alitumia mfano wa Mkara, kabila dogo wilayani Ukerewe, Mwanza ambalo lilichukuliwa kuwa dhalili kwa kufanya kazi za suluba (mikokoteni) akisema kuhoji kama hata Mkara anafaa kuchaguliwa kuwa rais ni dhambi kubwa.

Ni kauli hiyo inayotarajiwa kumpa unafuu Profesa Mbarawa na kupenya tano bora na kuteuliwa ili 2025 awe hazina ya kuwa Rais wa Muungano. Wanaompa nafasi kubwa wanapiga hesabu za Dk Mwinyi kupata upinzani mkubwa Unguja na kuacha ushindani kwa Nahodha na Mbarawa. Je, ni nani kati ya watano kama kweli ndio hao waliojadiliwa na Makala haya atateuliwa Ijumaa hii, Julai 10, 2020 ni suala la muda.

Hata hivyo, lolote linaweza kutokea kama Karume 2000 na Bilal 2010 aliposhindwa akateuliwa mgombea mwenza wa Rais Kikwete. Hata hivyo, wadadisi wa masuala ya siasa wanaona kibao kikimgeukia Dk Mwinyi, atakuwa amezua changamoto ya mgombea mwenza wa JPM.

CCM ina utamaduni mzuri kwamba, licha ya kutegemea sifa, mara nyingi Rais wa Muungano akitoka Bara na wa Zanzibar Unguja, mgombea mwenza hutoka Pemba kuleta uwiano kwa Muungano. Rais Mkapa alimteua Dk Omary Ali Juma kama mgombea mwenza kutoka Pemba na alipofariki, alimpendekeza Rais Shein na Rais Kikwete alimpendekeza Dk Bilal wa Unguja.

Yamkini ya Dk Mwinyi na Nahodha kupata hata umakamu wa Rais ni finyu, unashikiliwa na Mama Samia Hassan Suluhu wa Makunduchi, Unguja na JPM hajasema kama ataendelea naye ili kuenzi wanawake au atataka chaguo jipya. Ni ukweli huo unaowaacha Wazanzibari katika tanziko la kuendelea na Rais kutoka Pemba kufuta kabisa ndoto za Maalim Seif au wachague kati ya wagombea kutoka Unguja.

Hata hivyo, Upemba na Uunguja siyo sifa ya CCM kupata kiongozi; wanavyo vigezo vyao bora zaidi. Kimsingui, CCM kiendelee kufuata wosia wa Nyerere wa kutochagua Rais (kiongozi) kwa kuangalia ukabila, undugu, eneo moja bali uwezo wake.

BABA wa Taifa, Mwalimu Julius K Nyerere, ndiye Rais wa ...

foto
Mwandishi: Godfrey Lutego

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi