loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mafanikio makubwa ya JPM nishati

AHADI za Rais John Magufuli katika sekta ya umeme, zimetimia kutokana na mafanikio makubwa yaliyoonekana katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake tangu alipoingia madarakani mwaka 2015 mpaka sasa.

Miongoni mwa ahadi zilizotimia ni pamoja na iliyohusu kuhakikisha umeme unapatikana wa kutosha, hatua ambayo imekomesha mgawo kutokana na kuwapo ziada ya umeme wa wastani wa megawati 325 kwa siku.

Utekelezaji wa ahadi za Rais Magufuli, alizotoa hususani kupitia hotuba yake ya ufunguzi wa Bunge mwaka 2015, umedhihirika kutokana na kukamilika kwa miradi ya umeme iliyokuwapo na kujenga mingine mipya, kuwezesha wananchi kunufaika na nishati ya umeme.

Mgawo umekoma

Miongoni mwa ahadi alizotoa Rais Magufuli ni kukomesha mgawo wa umeme, kwa kukabili watendaji waliokuwa wakisadikiwa kufanya hujuma dhidi ya upatikanaji wa umeme, zilizochangia upungufu wa kina cha maji na kusababisha kukatika kwa umeme mara kwa mara.

“Hujuma nyingine zinazofanywa na watendaji wa sekta ya umeme kwa mfano wakati mvua zinaponyesha, mtu analipwa fedha. Mfano pale Mtera, wanayafungulia maji, halafu ‘level’ yake haifiki kwa wakati. Kila siku maji hayatoshi, hizi tutazisimamia kikamilifu,”aliahidi Rais Magufuli na kuongeza:

“Kwa sababu pamekuwa na mtindo huu watu wanapotaka ku-supply (kusambaza) majenereta yao au kununua mafuta ya bei ya juu wanalipwa wanaohusika pale Mtera...Tuta ‘deal’ nao. Na mimi nawaambia nitadeal nao.”

Ongezeko la umeme

Akieleza mafanikio ya utekelezaji wa mpango wa bajeti ya Wizara ya Nishati kwa mwaka 2015/16 hadi 2020, Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani alisema katika kipindi cha miaka mitano cha Serikali ya Awamu ya Tano, lipo ongezeko kubwa la uzalishaji wa umeme. Hadi Aprili mwaka huu, uwezo wa mitambo ya kufua umeme umeongezeka na kufikia jumla ya megawati 1,601.84 kutoka megawati 1,308 mwaka 2015.

Mafanikio mengine ni kukamilika kwa miradi ya kuzalisha umeme ya Kinyerezi I wenye megawati 150 na Kinyerezi II wenye megawati 240 na jumla ya megawati 398.22 zimeingizwa kwenye Gridi ya Taifa; Ujenzi wa Mradi wa kuzalisha umeme wa maji wa Julius Nyerere (JNHPP) katika Mto Rufiji, utakaozalisha megawati 2,115 unaendelea na utekelezaji wake umefikia zaidi ya asilimia 85 kulingana na mpango kazi wa kazi zilizopangwa. Unatarajiwa kukamilika mwaka 2022.

Upo pia Mradi wa Rusumo wenye megawati 80 unaotekelezwa ambao umefikia asilimia 61. Mafanikio mengine ya serikali ya awamu ya tano ni kuunganisha mikoa ya Lindi, Mtwara, Njombe na Ruvuma katika Gridi ya Taifa na kuwezesha kusitisha uzalishaji wa umeme kwa kutumia mitambo ya mafuta mazito, yaliyokuwa yakigharimu Shirika la Umeme (Tanesco) wastani wa Sh bilioni 15.3 kwa mwaka.

Kukamilika kwa Mradi wa njia ya kusafirisha umeme kilovoti 220 kutoka Makambako hadi Songea, ambao ulikamilika Septemba mwaka 2018 na kuwezesha vijiji vyote 122 kuunganishiwa umeme.

Watumiaji umeme

Katika hotuba yake ya kufunga Bunge, Rais Magufuli alisema kutokana na hatua zilizochukuliwa na serikali yake, idadi ya watumiaji wa umeme imeongezeka kutoka asilimia 35 hadi asilimia 85.

“Na hii imechagizwa sana na ushushaji wa gharama za kuunganisha umeme kutoka shilingi 177,000 hadi shilingi 27,000,” alisema Rais Magufuli na kuongeza kuwa pia tatizo la kukatika kwa umeme limepungua.

Alisema katika kipindi chote cha miaka mitano, nchi haikuwahi kuingia gizani na zaidi ya hapo serikali imeokoa kiasi kikubwa cha fedha, kwa kuzima mitambo ya kuzalisha umeme wa mafuta ya Independent Power Tanzania Limited(IPTL), Aggreko na Symbion.

Hatua hiyo imeokoa Sh bilioni 719 kwa mwaka. Tanesco bila ruzuku Rais Magufuli alisema kuzimwa kwa mitambo hiyo, kumesaidia Tanesco kuanza kujiendesha.

Akizungumza juzi wilayani Sengerema, Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani alisema shirika hilo lililoimarika, sasa linajiendesha bila kupata ruzuku serikalini.

Alisema kuwa inatarajiwa kuwa ifikapo mwaka 2026 litakuwa limelipa madeni yake yote.

Dk Kalemani ambaye yupo kwenye ziara ya kufuatilia utekelezaji wa miradi ya usambaji umeme vijijini, kukagua hali ya upatikanaji wa umeme na ufuatiliaji wa huduma kwa wateja, aliitaka Tanesco kuanza kupeleka umeme kwenye visiwa kwa kutumia “Marine cable” ili wananchi wa maeneo hayo, wapate umeme wa gharama nafuu.

Visiwa hivyo ni Maisela cha Sengerema, Iramba Mrumi (Muleba) na Bwisa kilichopo Ukerewe, ambavyo vinapata umeme wa jua. Kwa mujibu wa waziri, kampuni za umeme wa jua zimekuwa zikitoza hadi Sh 3,500 kwa uniti.

“Tumia teknolojia za kilimo na utawala bora kwa ukuaji wa ...

foto
Mwandishi: Stella Nyemenohi

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi