loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

IGP: Vijana msikubali kutumiwa

MKUU wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali (IGP) Simon Sirro( pichani), amewataka vijana kutokubali kutumiwa na mtu yeyote kwa maslahi binafsi. Alitoa hadhari hiyo juzi wakati akizindua Kituo cha Polisi Kisaki Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, ambacho ujenzi wake umegharimu Sh milioni 56.

Alisema vitendo vya kufanya vurugu na uhalifu hususani kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu, havikubaliki. Kituo hicho kimejengwa kutokana na maelekezo ya Rais John Magufuli, aliyoyatoa Julai 25, mwaka jana alipozungumza na wananchi wa Kata ya Kisaki.

Rais ambaye alichangia Sh milioni tano za ujenzi, alikuwa akienda kuweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa Bwawa la Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (JNHPP) wilayani Rufiji, Pwani.

“Msikubali kutumiwa na mtu yeyote kwa faida yake binafsi, siku zote wakati wa vurugu huwezi kuchagua kiongozi mzuri, kaeni mfikirie mtu anayekuja kukudanganya ufanye vurugu, uvunje sheria, mwambie mimi sitaki kwa vile umri wangu bado na sipendi kufia katika vyombo vya dola,” alisema Sirro.

Alisema pamoja na kila mtu kuwa na haki ya kushiriki katika uchaguzi, mara nyingi baadhi ya wanasiasa hutumia vijana, kama ngazi ya kupata kura kwa wananchi, kwa kuchochea matukio ya uvunjifu wa amani.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mutafungwa alisema kujengwa kwa kituo hicho, kutasaidia kupambana na uhalifu katika eneo hilo. Alisema kufunguliwa kwake, pia ni jitihada za mkakati wa mkoa kukabili migogoro ya wafugaji na wakulima.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, Rehema Bwasi alisema kutokana na ukubwa wa halmashauri hiyo, anamuomba IGP kuwapatia wilaya ya kipolisi kuongeza ulinzi katika eneo hilo kutokana na kuwepo mradi mkubwa wa Bwawa la Mwalimu Nyerere.

MSEMAJI Mkuu wa Serikali ...

foto
Mwandishi: John Nditi, Morogoro

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi