loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Skana 2 za nishati ya mionzi bandarini kuanza kazi Septemba

MASHINE mbili za kukagua mizigo (scanners) bandarini, zinazotumia teknolojia ya nishati ya mionzi kutoka China, zitaanza kutumika Septemba mwaka huu, zikiwa na uwezo kwa kupima makontena 200 kwa wakati mmoja.

Mashine hizo zinazoendelea kujengwa bandarini, zimekamilika kwa asilimia 90 na zinajengwa kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 5.5 ikiwa ni ufadhili wa serikali na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).

Kamishna wa Petroli na Gesi katika Wizara ya Nishati, Adam Zuberi alisema mradi huo uko chini ya Wizara ya Nishati na unasimamiwa na Shirika la Mafuta (TPDC).

Alisema hayo wakati wa ziara ya Kamati ya Usimamizi wa Mradi wa Uboreshaji wa Taasisi za Usimamizi wa Rasilimali Asilia na Ukusanyaji wa Mapato, kuangalia maendeleo ya ujenzi wa mashine hizo.

Alisema mradi huo ni kwa ajili kupima mizigo, inayoenda na kutoka bandarini na kuwa wameridhika na ujenzi wake uliokamilika kwa asilimia 90 na unatarajia kukamilika mwezi Septemba na kuanza kazi.

Mkurugenzi Mkuu wa TPDC, James Mataragio alisema mpaka sasa mradi una maendeleo mazuri na tayari jengo limekamilika kwa asilimia 99. Alisema kilichobaki sasa ni kufunga skana, ambayo imefikia asilimia 51 na wana uhakika wa mashine hizo kuanza kazi mwezi Septemba mwaka huu.

Mataragio alibainisha kuwa hakuna madhara katika matumizi ya mionzi kufanya ukaguzi wa mizigo, kwani tahadhari zote zimechukuliwa na wakandarasi wamezingatia usalama kwa kuhakikishia hakuna athari kwa watumiaji.

Meneja wa Mradi huo, Asiad Mrutu alisema lengo la mradi ni kuboresha taasisi zinazosimamia rasilimali asilia na kuimarisha ukusanyaji mapato katika taasisi tisa zinazonufaika na mradi huo, ikiwemo wizara ya nishati, TPDC, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA).

Alisema katika ukusanyaji mapato, mradi huo utaboresha mifumo ya TRA na bandari katika kukagua mizigo, ikiwemo ujenzi wa mashine mbili, kwa kurahisisha ukaguzi wa mizigo bandarini na kuongeza usalama wa nchi, kwani itakuwa rahisi kutambua kilichopo kwenye makontena ya mizigo kutoka nje.

WANACHAMA wa vyama vya ...

foto
Mwandishi: Theopista Nsanzugwanko

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi