loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wasanii sasa mambo safi

WASANII sasa mambo yao safi baada ya serikali kuwarahisishia utendaji wao wa kazi, wakiwemo wa fi lamu ambao wamepunguziwa tozo kutoka Sh 500,000 hadi 50,000 ili kuwawezesha kutengeneza kazi nyingi na zenye ubora wa hali ya juu.

Hayo yalisemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Hassan Abbasi jana kwenye hafla fupi ya makabidhiano ya Taasisi ya Hakimiliki Tanzania (Cosota) iliyotoka Wizara ya Viwanda na Biashara.

Makabidhiano hayo ni utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli kuitaka Cosota kuhamia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ili kuwa karibu na wadau wenye mwelekeo mmoja.

“Tumekamilisha kanuni mpya za Bodi ya Filamu na tumeshazitangaza kupitia gazeti la serikali, ambapo miongoni mwa mambo yaliyopo ni kupunguza tozo zilizokuwa zinawakwamisha wasanii wengi, ”alisema.

Dk Abbas alisema wameshusha tozo hizo kwenye vibali na kuhakikiwa, lengo likiwa kusaidia wasanii kutengeneza filamu nyingi na bora, huku akiahidi pia kuwa wanaendelea kufanya kazi na bodi husika kutengeneza masoko ndani na nje ya nchi.

Alisema fedha zilizobaki Sh 450,000 anataka zitumike kuwekeza kwenye kuandika vizuri miongozo ya filamu na wakati huo huo, akiwahidi kuwapa mafunzo mbalimbali wasanii yatakayotolewa na magwiji wa filamu wa kimataifa watakaoalikwa nchini.

Pia, alisema kupitia kanuni mpya zilizopo wameunda kamati kwa ajili ya kufuatilia mikataba na maslahi ya wasanii. Suala lingine alisema wameokoa fedha za wasanii kutoka kwa wajanja zaidi ya Sh milioni 200 ambapo kati ya hizo, zipo zinazowahusu waigizaji maarufu nchini, ambao ni marehemu Amri Athuman au Mzee Majuto akitolea mfano kuwa familia ya mzee huyo imekabidhiwa Sh milioni 65 na za marehemu Steven Kanumba milioni 20 zimekabidhiwa familia yake.

Alisema ndani ya saa 24 zijazo, atafanya mambo magumu makubwa ikiwemo kukutana na Cosota kujua mikakati yao ikoje kumsaidia msanii awe maarufu tajiri na sio maskini.

Pia, alisema serikali imeridhia kurejesha Mfuko wa Sanaa na Utamaduni ndani ya mwezi mmoja. Na kingine watarejesha viwanja vya sanaa za maonesho vilivyoporwa maeneo ya Mirambo, Upanga na Mihayo, Dar es Salaam.

Awali, Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Profesa Riziki Shemdoe aliwahimiza Cosota kuendeleza yale mazuri waliyokuwa wakifanya walipokuwa huko kuhakikisha wasanii wananufaika na kazi zao.

Mtendaji Mkuu wa Cosota, Dk Doreen Sinare aliomba kupata ushirikiano na mahitaji muhimu kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo huku wakieleza changamoto zao ni uhaba wa watendakazi.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Godfrey Mngereza alisema wamewapokea Cosota kwa mikono miwili kwa lengo la kujenga Tanzania ya wasanii na sanaa.

BAADA ya Namungo FC ...

foto
Mwandishi: Grace Mkojera

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi