loader
ZINDZISWA MANDELA: Nyota iliyozimika na kuacha alama nyingi

ZINDZISWA MANDELA: Nyota iliyozimika na kuacha alama nyingi

NI mwanasiasa, mwanaharakati shujaa na asiyetishika tangu akiwa mtoto. Alipinga sera za kibaguzi. Alikosoa bila woga sera tata za serikali.

Miongoni mwa matukio anayokumbukwa kuyafanya, ni namna alivyojitosa bila kujali umri wake wa miaka 12, kumtetea mama yake dhidi ya serikali ya kibaguzi ya Afrika Kusini. Huyu si mwingine bali ni Zindziswa Mandela; binti wa Rais wa Kwanza mwafrika wa Afrika Kusini, Nelson Mandela aliyekutwa na mauti akiwa na umri wa miaka 59.

Alifariki Jumatatu, Julai 13, mwaka huu mjini Johannesburg. Kifo chake kilitokea hospitalini na kutangazwa na Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa. Haikuelezwa chanzo cha kifo. Zindziswa maarufu kama Zindzi, ni binti mdogo wa Mandela aliyepaza sauti bila woga kama mwanaharakati na mshairi.

Mauti yamemkuta siku chache kabla ya Siku ya Nelson Mandela ambayo hufanyika kila Julai 18 ambayo taifa hilo na dunia huadhimisha kumbukumbu ya kuzaliwa kwa baba yake (Mandela). Mandela alikuwa mwanamageuzi aliyepinga ubaguzi wa rangi na Rais wa Kwanza mwafrika aliyefariki mwaka 2013.

Hadi anafariki, Zindzi alikuwa Balozi wa Afrika Kusini nchini Denmark tangu mwaka 2015. Kwa mujibu wa Rais Ramaphosa, Zindzi alikuwa nyumbani Johannesburg akisubiria kwenda kuwa balozi nchini Liberia kwenye kituo kingine cha kazi. Shujaa Zindzi alizaliwa Desemba 23, 1960, katika mji wa Soweto, Johannesburg.

Akiwa na umri wa mwaka na nusu, baba yake alikamatwa na kuhukumiwa kwa madai ya hujuma na uhaini. Wakati Mandela akihukumiwa kifungo cha maisha jela katika Kisiwa cha Robben, Pwani ya Magharibi, Zindzi alikuwa na umri wa miaka mitatu.

Ushujaa wake ulianza kuonekana akiwa na umri wa miaka 12 alipoandika barua kwenda Umoja wa Mataifa akiuomba uingilie kati na umlinde mama yake, Winnie ambaye pia alikuwa mwanaharakati aliyepinga ubaguzi wa rangi.

Barua hiyo aliyoandika mwaka 1973 ilisomeka: “Naandika barua hii kwako kwa sababu kama mama yangu angeandika, msingeipata kwa sababu barua zake nyingi kwa marafiki zake haziwafikii. Familia na marafiki wa mama yangu wana hofu. Mazingira yalivyo, jambo baya linaweza kumtokea mama yangu.”

Mwaka 1977, serikali ya kibaguzi ilipomfukuza Winnie kwenda mji wa Brandfort uliopo kilometa 400 kutoka Johannesburg, Zindzi pia alikwenda na mama yake. Alipelekwa katika shule ya bweni nchini Swaziland na baadaye alihitimu Shahada ya Sheria katika Chuo Kikuu cha Cape Town.

Rais wa Afrika Kusini, Pieter Willem Botha aliamua kumwachia Mandela kwa sharti la zuio katika wilaya huru ya Transkei, ambalo lilianzishwa na utawala wa Chama cha Wazungu cha National Party kwa ajili ya wenyeji weusi, Mandela alikataa ofa hiyo.

Zindzi aliwasilisha ujumbe kwa serikali ya Botha mwaka 1985. Februari, mwaka huo, wakati wa mapambano dhidi ya upaguzi wa rangi yaliyoshika kasi Afrika Kusini, Zindzi alizungumza na mamia ya watu mjini Soweto kwa niaba ya baba yake aliyekuwa kifungoni na mama yake aliyefukuzwa.

Kipindi hicho ndipo Zindzi alianza uanaharakati kama anavyoeleza mmoja wa mawaziri, Lindiwe Sisulu ambaye ni binti wa mwanaharakati mpinga ubaguzi wa rangi, Walter Sisulu aliyefungwa pamoja na Mandela.

“Kwa haki yake mwenyewe, alikuwa mpiganaji na kama angekuwa na uwezo angeenda kwenye mafunzo ya kijeshi, lakini alikuwa na mama wa kumtunza,” Lindiwe alilieleza Shirika la Utangazaji la Afrika Kusini saa chache baada ya kifo cha Zindzi.

Zindzi alikuwa mshiriki wa kampeni iliyoshinikiza Mandela kuachiwa huru na alipewa mafunzo ya operesheni za chini kwa chini yaliyotolewa na kikundi cha mapambano kilichokuwa chini ya Chama cha African National Congress (ANC). Mtazamo wa Zindzi kupinga ubaguzi unabainishwa katika utenzi wake “Black as I Am,” uliochapishwa mwaka 1978. Vile vile katika shairi “A tree was chopped down,” uliokumbuka familia ilivyosambaratishwa.

Majanga aliyopitia Lindiwe anamwelezea Zindzi kama mdogo wake wa kike na kumtaja kwamba kwake alimuona kama sura iliyopitia majanga. Siku ambayo utawala wa kibaguzi ulitangaza kumuachia Mandela kutoka gerezani, mwaka 1990, Zindzi alifiwa na mwenza wake ambaye baba wa mmoja wa watoto wake. Mwaka 2010 alifiwa na mjukuu wa kike mwenye umri wa miaka 13, Zenani aliyekufa katika ajali ya gari baada ya kutoka kuhudhuria tamasha la FIFA World Cup.

“Miaka ya hivi karibuni hata akiwa katika nafasi yake ya kidiplomasia, Zindzi alikuwa akikosoa wazi sera za Afrika Kusini,” anasema Lindiwe.

Anakumbuka Juni mwaka jana alipoandika katika akaunti yake ya twitter akisema: “Wapendwa watetezi wa ubaguzi, muda wenu umekwisha…hamta tawala tena. Hatuwaogopi. Hatimaye ardhi ni yetu.”

Ujumbe huo aliuandika katikati ya mjadala mkubwa wa marekebisho ya masuala ya ardhi Afrika Kusini ambapo wakulima wa kizungu walikuwa wanaendelea kushikilia maeneo makubwa ya ardhi licha ya ubaguzi kukoma. Kundi la ushawishi la AfriForum linalopigania haki za wahamiaji, lilifungua malalamiko kwa Tume ya Haki za Binadamu likimtuhumu Zindzi kwa ubaguzi.

Hata hivyo mwanaharakati na mwanadiplomasia huyo hakuacha kwani baadaye aliandika ujumbe unaosema: “Siwajibiki kwa mwanaume au mwanamke mzungu yeyote ninapotoa maoni yangu binafsi.”

Aidha Februari mwaka huu alituma ujumbe kwenye akaunti yake ya twitter kueleza alivyovunjika moyo baada ya Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Frederik Willem de Klerk kuruhusiwa kuzungumza katika hafla ya kitaifa na kutoa kauli kuwa matatizo yote ya nchi hiyo hayawezi kulaumiwa kwa sababu ya ubaguzi. Zindzi alieleza kuwa amevunjika moyo kutokana na alivyotetea matendo yake. Kisha aliweka picha ya mama yake (Winnie) ya mwaka 1991 akiburutwa na maofisa polisi.

Ndoa/ familia Mwanamama huyo alifunga ndoa mara mbili kwa nyakati tofauti. Ndoa ya kwanza ni ya mwaka 1992 aliyofunga na mfanyabiashara Zwelibanzi Hlongwane. Mwaka 2013 alifunga ndoa na Molapo Motlhajwa, aliyeishi naye mpaka mauti yanamkuta.

Zindzi ameacha watoto wanne; wa kike Zoleka na wa kiume ni Zondwa, Bambatha na Zwelabo. Kifo cha Zindzi kimefanya kati ya watoto sita wa Mandela, wamebaki Zenani Dlamini ambaye ni Balozi wa Afrika Kusini nchini Korea Kusini na Pumla Makaziwe aliyezaliwa na Evelyn Mase aliyekuwa mke wa kwanza wa Mandela.

Zindzi alizikwa Ijumaa katika eneo la Fourway Memorial Park jijini Johannesburg pembeni mwa kaburi la mama yake Winnie na wajukuu zake (Zindzi) Zinawe (alifariki 2011) na Zenani (alifariki 2010) Mandela. Ingawa Rais Ramaphosa hakutaja chanzo cha kifo lakini Askofu Gary Rivas alisema Zindzi alikutwa na homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona (Covid-19) siku aliyofariki.

Pia mtoto wa kiume wa Zindzi, Zondwa alithibitisha mama yake kukutwa na ugonjwa huo ingawa hakusema kama ndiyo chanzo cha kifo chake. Maziko ya mama huyu anayetajwa kama ‘askari wa nchi kavu’ yalifanyika kukiwa na tahadhari kutokana na ugonjwa wa Covid-19 na yalihudhuriwa na wanafamilia wachache lakini pia viongozi na wanasiasa wachache sana.

Mama aliyejitoa bila woga tangu akiwa na umri mdogo kutetea haki na usawa wa Waafrika bila kuogopa vitisho vya namna yoyote. Makala haya yameandaliwa na ANGELA SEMAYA kwa msaada wa intaneti.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/6bbaa8b9009c7fb90af4669d6411e1a5.jpg

NCHINI Tanzania kuna matajiri wengi wakubwa walioanzia ngazi ...

foto
Mwandishi: JOHANNESBURG, Afrika Kusini

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi