loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mawaziri wang’ara kura za maoni CCM

KURA za maoni kwa walioomba kuteuliwa kugombea ubunge na uwakilishi kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), zilizoanza jana zimetoa matokeo mazuri kwa mawaziri katika Serikali ya Awamu ya Tano.

Miongoni mwa mawaziri walioongoza kwenye kura hizo ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama wa Jimbo la Peramiho aliyepata kura 845, akifuatiwa na wenzake wengine ambao waliambulia kura tatu, mbili na moja.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo aliongoza kwa kupata kura 588 kati ya kura 601 zilizopigwa. Wagombea wengine wamepata kura moja hadi tatu. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alipata kura 453 akifuatiwa na wagombea wengine waliopata kura kati ya 0 hadi 16.

Katika Jimbo la Newala Mjini, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, George Mkuchika aliongoza kwa kupata kura 319, akifuatiwa na Rashidi Mtima 121 na Karimu Lichela 42.

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Angeline Mabula aliongoza Jimbo la Ilemela, Mwanza kwa kupata kura 502, kati ya kura 685 zilizopigwa na alifuatiwa na Israel Mtambalike aliyepata kura 112. Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga aliongoza kwenye matokeo hayo Jimbo la Vwawa mkoani Songwe, kwa kupata kura 552 akifuatiwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mbozi, Elick Minga aliyepata kura 129.

Jumla ya kura zilizopigwa ni 723 na wagombea walikuwa 15. Jimbo la Kasulu Mjini mkoani Kigoma, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako aliongoza kwa kupata kura 405 na kufuatiwa na aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Daniel Nsanzugwanko aliyepata kura 80. Msimamizi wa uchaguzi katika jimbo hilo, Thomas Sangai alisema mgombea mwingine, Thobias Mhanuzi alipata kura tatu, Patrick Mbasha kura tatu na Mteule Mkono kura mbili.

Waziri wa Madini, Doto Biteko aliongoza kura hizo Jimbo la Bukombe mkoani Geita kwa kupata kura 555, kati ya kura 569 zilizopigwa. Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango ameongoza kura hizo katika Jimbo la Manyovu mkoani Kigoma, kwa kupata kura 298 akifuatiwa na aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Albert Obama aliyepata kura 72.

Jimbo la Karagwe mkoani Kagera, lililokuwa na watia nia 36, Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa aliongoza kwa kupata kura 587 kati ya kura 679 zilizopigwa.

Msimamizi wa uchaguzi huo ambaye ni Katibu wa CCM Wilaya ya Karagwe, Mery Kananda alisema wagombea wengine walipata kura kati ya 46 hadi sita. Jimbo la Muhambwe mkoani Kigoma, Method Kamamba aliongoza kwa kupata kura 50 akifuatiwa na Method Msakila aliyepata kura 47 na aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, Christopher Chiza alipata kura 33.

Jimbo la Kibakwe mkoani Dodoma, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene aliongoza kwa kupata kura 667, akifuatiwa na Dk Kwame Mwaga aliyepata kura 151. Jimbo la Nyasa mkoani Ruvuma, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Stella Manyanya, alipata kura 539. Jimbo la Kigoma Mjini, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Kirumbe Ngenda aliongoza kwa kupata kura 218 dhidi ya kura 44 za Tabibu wa tiba asili, Dk Juma Mwaka.

Mwingine ni James Nyabakari aliyepata kura 37, huku mwandishi wa habari Baruani Muhuza alipata kura 10. Msimamizi wa Uchaguzi, Naftali Robert alisema Noel Severe aliongoza katika Jimbo la Arumeru Magharibi mkoani Arusha kwa kupata kura 113 akiwashinda wagombea wenzake 32, akiwemo aliyewahi kuwa mbunge wa jimbo hilo, Goodluck Ole Medeye aliyepata kura 14.

Mbunge aliyemaliza muda wake Jimbo la Kongwa mkoani Dodoma, Job Ndugai, aliongoza kwenye matokeo ya kura za maoni kwa kupata kura 850, akifuatiwa na Dk Samora Mshanga aliyepata kura 20 na Isaya Mngulumi mwenye kura 19. Katika Jimbo la Mbeya Mjini, aliyekuwa Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, Dk Tulia Ackson aliongoza kwa kupata kura 843 akifuatiwa na Dk Mahande Mabula aliyepata kura 16.

Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Gairo, Deogratius Rutha alisema mbunge aliyemaliza muda wake, Ahmed Shabiby aliongoza kwa kupata kura 532 kati ya kura 591, akifuatiwa na Dk Joel Mmasi aliyepata kura nane na Sehewa Chiduo aliyepata kura sita. Jimbo la Siha mkoani Kilimanjaro, mgombea aliyeongoza ni Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto, Dk Godwin Mollel aliyepata kura 148 akifuatiwa na Aggrey Mwanri aliyepata kura 147.

Mbunge anayemaliza muda wake Mtwara Vijijini, Hawa Ghasia alishinda kwenye kura za maoni kwa kupata kura 440 kati ya kura 847. Ghasia aliwashinda wagombea wenzake 14. Aliyemfuatia ni Seleman Mwamba aliyepata kura 191 na Olivernus kura 139.

Katika Jimbo la Morogoro Mjini, Msimamizi wa Uchaguzi, Hamza Mfaume alisema wagombea walikuwa 80 na mbunge aliyemaliza muda wake, Abdulaziz Abood aliongoza kwa kupata kura 524 kati ya kura halali 635.

Katika jimbo la Vunjo mkoani Kilimanjaro, Enock Koola aliongoza kura za maoni kwa kupata kura 187 kati ya 567 akifuatiwa na aliyewahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji Benki ya CRBD, Dk. Charles Kimei aliyepata kura 178 na Chrispine Meela aliyepata kura 47.

Mkoani Dar es Salaam, aliyekuwa mbunge wa Kigamboni, Dk Faustine Ndugulile aliongoza kwa kupata kura 190 akifuatiwa na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo, Paul Makonda aliyepata kura 122.

Katibu wa CCM Wilaya ya Kinondoni, Sure Mwasanguti alisema katika Jimbo la Kinondoni mkoani Dar es Salaam, watia nia 79 walijitokeza na Abbas Tarimba aliongoza kwa kupata kura 171 na kufuatiwa na Idd Azzan kura 77, Manyama kura 32 na Said Subert kura 28.

Kwenye Jimbo la Ilala, Katibu wa CCM wilayani humo, Idd Mkowa alisema aliyeongoza kwenye kura za maoni ni Mussa Hassan ‘Zungu’ aliyepata kura 148 na kufuatiwa na Sofia Mjema 103. Jimbo la Ubungo, aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Profesa Kitila Mkumbo aliongoza kwa kupata kura 172 akifuatiwa na Mwamtumu Mgonja aliyepata kura 73.

Mbunge aliyemaliza muda wake katika jimbo la Bumbuli mkoani Tanga, January Makamba aliongoza kwa kupata kura 680 na kufuatiwa na Abdulkadir Mghen aliyepata kura 21. Jimbo la Kondoa Mjini mkoani Dodoma aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Edwin Sanda ameanguka kwenye kura za maoni.

Ally Makoa aliongoza katika kura za maoni katika jimbo hilo kwa kupata kura 137 akifuatiwa na Omary Kimbisa aliyepata kura 71. Katika Jimbo la Chalinze mkoani Pwani, Ridhiwani Kikwete aliongoza kwa kupata kura 369, akifuatiwa na Ramadhani Maneno kura 273 na Said Zikatimu kura 223.

Katika Jimbo la Arusha Mjini, Msimamizi wa Uchaguzi, Molleit Ole Moko, alisema aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo aliongoza kwa kupata kura 333 akifuatiwa na Philemon Mollel aliyepata kura 68.

Jimbo la Kyerwa mkoani Kagera, mgombea aliyeongoza ni Innocent Bilakwate aliyepata kura 298, akifuatiwa na aliyewahi kuwa mbunge kwa tiketi ya TLP kabla ya kujiunga na CCM, Benedicto Mutungilei aliyepata kura 200.

Jimbo la Mvomero mkoani Morogoro, aliyeongoza ni Amos Makalla aliyepata kura 321 akifuatiwa na Selemani Sadiq aliyapata kura 231 na Jonas Zeland kura 112.

Matoke hayo ni kwa mujibu wa msimamizi wa uchaguzi huo, Heri Hoza.

Imeandikwa na Ikunda Erick (Dar), Veronica Mheta (Arusha), Nakajumo James (Moshi), Sijawa Omary (Mtwara), Sifa Lubasi (Dodoma), Diana Deus (Bukoba), John Nditi (Morogoro) na Muhidin Amri (Songea).

MILA na desturi zimeelezwa kuwa chanzo cha watoto kupata udumavu ...

foto
Mwandishi: Waandishi Wetu

1 Comments

  • avatar
    Martin
    22/07/2020

    Makala imeandikwa kwa umakini mkubwa. Hakuna hata kosa moja? Salute!

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi