loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tujiepushe na vurugu uchaguzi mkuu

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) hatimaye imetangaza kuwa Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utafanyika Oktoba 28, mwaka huu.

Pia, tume hiyo  imetangaza kuwa uteuzi wa wagombea wa kiti cha rais, ubunge na udiwani, utakuwa Agosti 25 mwaka huu na kampeni zitaanza rasmi Agosti 26 hadi Oktoba 27.

Tunaipongeza tume kwa kutoa ratiba hiyo ya uchaguzi, kwani ilikuwa inasubiriwa kwa hamu na Watanzania wengi na wadau wengine.

Lakini, ni vizuri Watanzania tukumbushane mambo kadhaa tunayotakiwa kuyazingatia katika kipindi chote hiki hadi siku ya kupiga kura na siku ya kutangaza matokeo.

Jambo kubwa ni kulinda amani na utulivu uliopo nchini; na tunampongeza Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP), Simon Sirro kwa kuzungumzia suala hilo, alipowahutubia maofisa wakuu waandamizi wa Polisi na makamanda wa mikoa na vikosi mbalimbali.

Sirro anaeleza kuwa ni wajibu wa Polisi, kuhakikisha kuna amani na utulivu nchini, kwa kuwa hatuwezi kupata viongozi wazuri na wazalendo wakati wa uchaguzi, kama kuna vurugu.

Kwamba Polisi wamejipanga kudhibiti vitendo vya uvunjifu wa amani kwenye uchaguzi wa mwaka huu; na watu wachache watakaosababisha uvunjifu wa amani wakati wa uchaguzi, watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.

Anasisitiza kuwa wameweka mikakati kabambe, kuhakikisha kuwa Jeshi la Polisi haliwi chanzo cha vurugu au ukosefu wa haki wakati wa uchaguzi.

Sirro anakumbusha kuwa Rais John Magufuli alishatoa maelekezo kwamba uchaguzi mkuu wa mwaka huu utakuwa huru na wa haki, hivyo Polisi kazi yao ni kusimamia vizuri  uchaguzi huo ili haki ionekane imefanyika.

Mbali na Polisi, makundi mengine yanayotakiwa kuhakikisha amani inalindwa ni wanasiasa na vyombo vya ulinzi na usalama. Makundi hayo mawili nayo yanatakiwa kutimiza wajibu wao, kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za nchi.

Kundi lingine ni wananchi ambao nao wanatakiwa watimize wajibu wao wakati wa kampeni, siku ya kupiga kura na wakati wa kutangaza matokeo, kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.

Kwa ujumla, makundi yote hayo, yajiepushe na vurugu na yashirikiane vizuri  na kutimiza wajibu wao kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa, ili uchaguzi uwe wa haki na huru.

KUMEKUWAPO na habari za kufurahisha kuhusu mashirika zaidi ya ndege ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi