loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Simulizi za Mkapa akiwa jeshini

RAIS mstaafu Benjamin Mkapa alijiunga na mafunzo ya kijeshi akiwa tayari ameshamaliza kusoma Chuo Kikuu Makerere, Uganda na kuajiriwa kama Mhariri Mtendaji wa gazeti lililokuwa likiitwa The Nationalist.

Mkapa alibainisha hayo katika kitabu chake cha My Life, My Purpose kinachoakisi maisha yake tangu akiwa mtoto kijijini kwao Lupaso, Mtwara hadi katika medani za siasa, kazi ya uandishi wa habari, urais wa nchi hadi kustaafu.

Anasema katika gazeti hilo alilokuwa akifanya kazi kati ya mambo aliyokuwa akifanya, ni pamoja na kutetea sera zilizotambulishwa na Rais wa Awamu ya Kwanza, Mwalimu Julius Nyerere hapa nchini kutoka katika nchi nyingine za kijamaa.

Anasema kati ya sera hizo, ilikuwa ni kuingia jeshini kwa vijana waliohitimu elimu ya juu mwaka 1964 na miaka miwili baadaye, ikawa ni lazima kwa wahitimu wa elimu hiyo kuingia mafunzo ya jeshini.

Anasema akiwa kama Mhariri Mkuu wa gazeti la Serikali, alihamasisha kwa kiasi kikubwa utekelezwaji wa sera hiyo huku akiwasihi wahitimu kujiunga na jeshi na kuelezea sifa na umuhimu mkubwa wa kujiunga nalo.

Akiwa anaendelea na harakati zake hizo, akasikia maneno kutoka kwa watu mbalimbali ambayo mengine alifikishiwa kutoka kwa watu wake wa karibu wakisema kuwa alikuwa akipigia debe vijana kuingia jeshini kwa kuwa yeye hakuwahi kuhudhuria mafunzo hayo.

Maneno hayo yalimgusa hasa ikizingatiwa kuwa hakuwahi kuingia jeshini kwa mafunzo kama hayo ambayo wahitimu wa elimu ya juu walikuwa wakihudhuria na hiyo ni kwa sababu wakati sera hiyo inatambulishwa, yeye alikuwa ameshaingia kazini.

Hivyo, aliamua kwenda kwa Mwalimu Nyerere na kumwelezea nia yake ya kuhudhuria mafunzo ya jeshi hilo ili kujionea mwenyewe kazi za jeshini humo na kuweza kuifanya kazi yake ya kulipigia debe jeshi hilo kuwa raisi zaidi.

Mafunzo hayo yalikuwa yakichukua muda wa miezi mitatu hadi minne.

Alipomwelezea nia yake hiyo, Mwalimu Nyerere alimuuliza kuwa ni nani atakayebakia kufanya kazi zake za kuhariri gazeti kama yeye akiondoka kwenda jeshini kwa muda huo wote.

Mkapa alimwelezea juu ya uwepo wa waandishi wa habari wawili ambao ni Ruhinda na Nsa Kaisi huku akiwanadi kuwa walikuwa wafanyakazi wake watiifu, wenye weledi wa hali ya juu na kuwa anaweza kuwatumia kama anavyomtumia yeye.

Anaelezea kuwa aliondoka akiwa ameruhusiwa na Mwalimu Nyerere kwenda jeshini ambapo alipoingia kambi ya jeshi, alianza kuona shughuli ilivyokuwa pevu katika kambi hiyo.

Anasema kwanza aliambiwa kwa ukali: Simama, beba hilo begi lako kichwani kisha kimbia elekea bwenini haraka sana.

Mkapa anasema kuwa wakati akiwa anapewa maelekezo hayo, ndipo alipoanza kuona maisha tofauti kutoka kuwa Mhariri Mkuu anayetuma watu kazi hadi yeye mwenyewe kukimbizwa mchakamchaka huku akikumbukia maisha yake ya shuleni Ndanda yalivyokuwa.

Anasema akiwa anaelekea bwenini akiwa na wenzake kulikuwa na mwanamke mwanajeshi akiwasindikiza ambaye mara kwa mara alikuwa akiwaambia: Mmeingia humu kambini shahada zenu mmeziacha nje hapa ni amri tu.

Mkapa anasema kuwa mwanajeshi huyo mwanamke alikuwa mzuri sana lakini alikuwa mwanamke shupavu, hana mzaha na hakukuwa na mtu ambaye angeweza hata kumwelezea mambo yoyote ya kipuuzi.

Anasema kulikuwa na watu wazima wenzake kutoka sehemu mbalimbali wakiwemo maofisa wenye shahada kama yeye, wengine wakulima na watu wengine ambapo wote walikuwa sawa wakiwa jeshini hapo.

Kati ya mambo ambayo yalimuumiza akili ni baada ya kuwa kambini hapo kwa mwezi mzima na siku moja jioni akafuatwa na mwanajeshi ambaye alimpatia jembe bila ya mpini na kisha kumtaka ifikapo asubuhi, afike kwenye paredi akiwa ana jembe lenye mpini.

Alichanganyikiwa kwa kuwa hakujua hata ni wapi pa kupata mpini huo wa kubebea jembe, akamuuliza rafiki yake mmoja ambaye alimsaidia kuchonga mpini wa jembe usiku huo na asubuhi walifika nao kwenye paredi kisha kumuonesha mwanajeshi huyo.

Anasema siku nyingine wakapewa agizo la kuandaa igizo kuhusiana na harakati za ukombozi na akajikuta akiwa amepangwa kundi moja na rafiki yake huyo aliyemsaidia kutengeneza mpini wa jembe.

Wakati huo Mkapa akamwambia rafiki yake huyo kuwa amwachie kazi ya kuandaa igizo hilo kwa kuwa Mkapa tangu amalize Shule ya Msingi Ndanda na kuingia elimu ya juu ya Sekondari Pugu alikuwa akipenda maigizo hasa ya jukwaani.

Aliandaa igizo kuhusiana na unyanyasaji uliokuwa ukifanywa na wakoloni wa Msumbiji na Angola huku akielezea unafiki uliokuwa ukifanywa na aliyekuwa Rais wa Malawi wakati huo, Kamuzu Banda, ambaye alikuwa ni kama kibaraka wa wazungu wakati akiwa Rais wa Malawi na alikuwa akiwasaidia makaburu wa Afrika Kusini kuwagandamiza Waafrika.

Mkapa anasema igizo lilikuwa zuri na wanajeshi waliuona uwezo wake mkubwa katika kuigiza hasa ikizingatiwa kuwa alipokuwa shuleni alikuwa mtu wa maigizo sana.

Walimaliza mafunzo yao ya miezi minne, Mwalimu Nyerere alikwenda kufunga mafunzo hayo, alipofika kambini hapo akaanza kukagua gwaride na wahitimu wote na akampita akiwa kwenye gwaride hilo bila ya kumtambua.

Lakini kwa kuwa Mkapa alichaguliwa kusoma risala ya shukrani ya kufunga mafunzo hayo ndipo wakati akisoma Mwalimu Nyerere alionesha kumkumbuka tena baada ya kutaja jina lake kuwa risala hiyo imesomwa na Benjamin Mkapa.

Anasema alikuwa amepungua uzito na kuwa mwembamba kitu ambacho hata mwenyewe alijiona amebadilika, kisha mafunzo yalipofungwa rasmi akarejea kazini.

Mkapa katika kitabu hicho anabainisha kuwa hata alipokuja kuwa Rais wa nchi mwaka 1995 mwaka mmoja baadaye, alipotembelea kambi ya jeshi Lugalo na kukumbana na kero nyingi zinazowakabili wanajeshi kipindi hicho, kwake alijiona ni kama sehemu ya jeshi hilo kwa kuwa alishaishi maisha jeshini na kushiriki kutatua kero hizo.

WAKATI zikiwa zimebaki siku ...

foto
Mwandishi: Evance Ng’ingo

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi