loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Asante Mkapa kutuachia Chuo Kikuu Huria

MZEE Benjamin Mkapa (81), Rais wa Serikali ya Awamu ya Tatu alifariki dunia usiku wa kuamkia Ijumaa na leo atazikwa kijijini kwao Lupaso Wilaya ya Masasi, Mkoa wa Mtwara.

Watu wengi, Watanzania na raia wa nchi za nje na jumuiya ya kimataifa wanaendelea kumlilia Mzee Mkapa aliyefariki kwa mshtuko wa moyo wakati akitibiwa hospitalini jijini Dar es Salaam.

Msemaji wa familia, William Erio ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa NSSF alisema kuwa, Mzee Mkapa alikuwa akitibiwa malaria baada ya kupelekwa hospitali alipojisikia vibaya.

Mengi yamesemwa na watu mbalimbali kwa jinsi walivyomfahamu Rais Mkapa. Kama watu wengine nitamkumbuka kwa mambo mengi baadhi yakiwa ya kitaaluma na kikazi.

Ukiacha ukweli kuwa nimeguswa na kifo chake kwa sababu nafahamiana na Erio ambaye ni mpwa wake, namkumbuka Mzee Mkapa kama mtu aliyekuwa kiongozi wetu wakati nafanya kazi kama mwandishi wa magazeti ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Uhuru na Mzalendo.

Nilijiunga na magazeti hayo Septemba 1990, na mwaka 1995 Rais Mkapa alipogombea urais, magazeti hayo yaliandika habari za kampeni kumnadi mgombea urais huyo wa CCM.

Ulikuwa ni wakati mgumu ambao uliacha taasisi ya Uhuru na Mzalendo katika hali ngumu ya kifedha kufuatia watu kudhani mgombea wa upinzani kupitia NCCR Mageuzi, Augustine Mrema ndiye alikuwa anafaa zaidi kuwa Rais hivyo kususa kununua magazeti ya Uhuru.

Hata hivyo, Mungu si Athumani kwani Mkapa alidhihirisha umahiri na uwezo mkubwa wa uelewa katika mdahalo wa wagombea urais ulioendeshwa na luninga ya ITV, mtangazaji akiwa Josephat Warungu wa Kenya. Halikadhalika Baba wa Taifa, Julius Nyerere alimnadi kwa wananchi hivyo kushinda uchaguzi huo 1995.

Ilikuwa kama alisikia machungu tuliyopitia katika kampeni kwani alipoanza kuteua tu viongozi, alimteua aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Magazeti ya Chama (siku hizi Uhuru Publications), Mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM, Daniel Ole Njoolay kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha.

Pia alitoa kiasi cha fedha kusaidia taasisi na hata alipochaguliwa kipindi cha pili mwaka 2000, pia alisaidia kupata gari ndogo ya Suzuki na kununua mtambo wa kuchapishia magazeti.

Kwa muktadha huo, nilimwona Rais Mkapa ni mtu wa shukrani kwa watu waliomsaidia katika kazi zake lakini pia aliyeweza kuteua wasaidizi wenye uwezo kwani Njoolay aliachaalama.

Akiwa Mkuu wa mkoa wa Arusha, Njoolay alishauri mkoa huo ugawanywe na kuzaa Manyara na hata alipohamishiwa Mwanza alifanya mabadiliko mengi makubwa kiasi hadi leo anakumbukwa.

Hata Rais Mkapa alipostaafu, Njoolay chini ya Rais Kikwete alionesha uwezo mkubwa kama RC Rukwa kwa kujenga mtandao wa barabara iliyounganisha na Mbeya ukawa mwanzo wa kufunguka mkoa kabla ya Katavi kuanzishwa.

Ukiacha suala la kampeni zake, nilimfahamu Mzee Mkapa kwa kupata fursa za kumhoji akiwa Waziri wa Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia mwaka 1993 na 1994, Katibu Mkuu wake akiwa Dk Gharib Bilal aliyekuja kuwa Makamu wa Rais wa Jakaya Kikwete.

Lakini nitamkumbuka zaidi kama mtu ambaye hata akishindwa kumsaidia mtu, huchukua hoja yake na kuifanyia kazi kwa njia nyingine kupata suluhisho la tatizo aliloombwa atoe msaada.

Kwa mfano, mwaka 1994 nilipomaliza diploma ya uandishi wa habari kupitia kilichokuwa Chuo cha Uandishi wa Habari Tanzania (TSJ), nilimfuata Rais Mkapa akiwa Waziri wa Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia bungeni Karimjee na kumwomba fursa ya masomo ya shahada ya uzamili ya uandishi wa habari nchini Uingereza.

Wakati huo mfumo wa elimu nchini haukuwa na chuo kinachotoa shahada ya kwanza wala ya uzamili ya uandishi wa habari bali waandishi walikuwa wakipelekwa nchi za nje na serikali ilikuwa imepeleka waandishi wawili Uingereza, Beda Msimbe na Bujaga Kadago wa RTD. Katika hali ya utulivu, Rais Mkapa alinisikiliza na kuniomba radhi kwamba serikali ilikuwa imesitisha kupeleka waandishi nje.

Hata hivyo, Rais Mkapa aliona kiu ya waandishi kusoma zaidi. Ili kuwawezesha kusoma zaidi, Chuo cha TSJ kiliunganishwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuanza kutoa shahada ya kwanza ya uandishi wa habari na baadaye diploma ya uzamili na shahada ya uzamili ya uandishi.

Rais Mkapa aliamini katika uandishi wenye weledi na amefariki akizidi kuusisitiza kwani katika kitabu chake, My Life My Purpose, ameelezea kuudhiwa kwake na waandishi wavivu, wasiopenda kusoma, kufanya utafiti na wasio na weledi.

Kauli yake inathibitishwa na aliyewahi kuwa Mhariri Mtendaji wa magazeti ya Serikali, Dk Jim Yonazi aliyewahi kuelezea namna Rais Mkapa alivyokuwa msomaji mzuri wa magazeti ya Habari- Leo na Daily News kutokana na kupenda yanavyoandikwa kwa umahiri mkubwa zaidi. Kwamba Rais Mkapa aliguswa na waliopenda kujiendeleza kielimu ilithibitishwa na aliyewahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Dk Batilda Burian aliyeieleza TBC baada ya kuaga mwili wa Mkapa Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam kwamba Mkapa alimsaidia kusoma shahada ya uzamivu (PhD) pale alipokwama.

Dk Batilda alieleza alivyomfuata Rais Mkapa na kumwomba ufadhili akamshika mkono hadi kwa Katibu Mkuu wa wizara yake, Dk Bilal na kupelekwa Tume ya Mipango kujishikiza hadi alipopata ufadhili kumalizia masomo yake na kisha kuja kusaidia uanzishaji wa mradi wa kuondoa umaskini, Tasaf aliouasisi Rais Mkapa.

Ni wazi Rais Mkapa alikuwa kiongozi ambaye aliguswa na watu wenye kiu ya kusoma wawe na weledi. Kwa maneno ya Waziri wa Fedha wa wakati wake, Basil Mramba juzi alipoaga mwili wake pia, Rais Mkapa aliamini kuwekeza katika elimu kama njia kumkomboa mtu na umaskini.Alipobaini Watanzania wengi wanataka kusoma lakini wanakosa muda au rasilimali fedha za kutosha kujiunga na vyuo vya nje au Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Rais Mkapa aliamua kuanzisha Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) mwaka 1999 na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) inayokopesha hadi leo.

Makamu Mkuu wa zamani wa Chuo Kikuu cha Udoma, Profesa Idd Kikula alilia sana aliposikia kifo cha Mkapa akikumbuka alivyokiongoza chuo hicho kwa ustadi akiwa mkuu wa chou hicho.

Anapoondoka mwenzake Mkapa mimi na wengine tuliokosa fursa ya kusomeshwa na serikali nje tutamuenzi kwa mengi ikiwemo kuanzisha Chuo Kikuu Huria ambako nimesoma shahada yangu ya kwanza ya sheria na uzamili ya Ushirikiano wa Kimataifa na Maendeleo (ICD) kwa gharama nafuu tofauti na nje ya nchi.

Mamilioni ya wanafunzi hasa wafanyakazi wa taasisi za binafsi na umma ambao wanaendelea kusoma OUT watamkumbuka Mkapa kwa kuanzisha chuo hicho akimpa jukumu hilo Makamu wa zamani wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Geoffrey Mmari na kuwapa fursa adhimu ya kujiendeleza kadri ya muda wao kuongeza weledi uliowasaidia pia kupanda madaraja kazini kuongeza kipato na madaraka.

Nitakumbuka Mkapa kama mtu ambaye alikuwa anajali watu wenye shida nikirejea alivyoamua kumfukuza mkuu mmoja wa Itifaki akamteua Balozi Cisco Mtiro baada ya mtu huyo kudaiwa kushindwa kumsaidia mwandishi wa habari aliyepotelewa mzigo wake walipokuwa naye ziarani Ulaya hivyo kukosa nguo za kubadilisha.

Kwa mujibu wa aliyekuwa mpigapicha wake, Godfrey Baluah, Mkapa hakupenda watu ambao walikuwa kwenye msafara wake wapate shida hivyo alivyobaini mwandishi yule hakusaidiwa wakati fungu lilikuwepo, alimwondoa mhusika waliporudi nchini na kumteua Mtiro.

Na hakika alilenga kumteua mtu aliyekuwa na moyo kama wake, Mtiro ambaye mwaka 2007 tulipokuwa naye Roma, Italia kwenye msafara wa Rais Kikwete, mwandishi mwingine alipotelewa mzigo wenye nguo zake baada ya kubadili ndege Ethiopia na hivyo begi lake kupelekwa Ujerumani badala ya Roma hadi siku ya tatu uliporejeshwa Cisco akiwa tayari amemsaidia fedha za kununua nguo nyingine.

Yatasemwa mengi kuhusu Mkapa wasiomjua wakiamini hakuwa karibu na watu.

Hata hivyo, ushuhuda uliotolewa na watu wengi umewasuta kwa kumwonesha kama baba, kiongozi mwenye upendo mkubwa, aliyekuwa mnyenyekevu kwa watu wote.

Nenda Mkapa, kalale salama baba. Umati uliokusindikiza unanikumbusha umati wa waombolezaji viwanja vya Kanisa la St Peters, Vatican mwaka 2005 mazishi ya Papa Yohanne II alipofariki walipoimba kwa nguvu wakisema Santa Sobito, yaani Papa atamkwe Mtakatifu. Mambo makubwa uliyotuachia ni alama tosha. 

TAIFA la Tanzania hivi karibuni lilipita katika majonzi makubwa ya ...

foto
Mwandishi: Godfrey Lutego

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi