loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mwisho wa enzi

NI mazishi na maziko ya shujaa kwa takriban saa nane na robo, kukamilisha safari ya mwisho duniani ya Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, yaliyoacha waombolezaji katika Kijiji cha Lupaso mkoani Mtwara wakiwa na majonzi.

Wakati mwili wa Mkapa ukishushwa kaburini saa tisa alasiri, nchi ilikuwa kama imesimama wakati Watanzania wakishuhudia mwenzao aliyewaongoza kwa miaka 10 akizikwa, hivyo hawatamuona tena.

Mazishi ya Mzee Mkapa yalikuwa ya kidini, lakini maziko yake yalifanywa kijeshi ikiwa ni pamoja na kupigiwa mizinga baada ya waombolezaji kuweka mashada ya maua.

Maelfu ya waombolezaji wakiongozwa na viongozi wa kitaifa akiwemo Rais John Magufuli, walishuhudia mizinga 21 ikipigwa sanjari na kufanyika kwa gwaride la heshima saa 9:05 alasiri wakati mwili wa Mkapa ukishushwa kaburini. Simanzi na majonzi vilitawala jana asubuhi wakati askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), walipoutoa mwili wa Mzee Mkapa kutoka ndani ya nyumba yake na kuuweka eneo kulikofanyika ibada ya misa ya mazishi na salamu za rambirambi kutoka kwa viongozi wa ndani na nje ya nchi.

Maegesho ya magarijana hayakutosha. Mara baada ya ibada ya misa takatifu iliyoongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya, Gervas Nyaisonga, waombolezaji waliokosa nafasi ya kutoa heshima za mwisho jijini Dar es Salaam na maeneo mengine ya nchi wakiwemo wanakijiji wa Lupaso, walipata fursa hiyo.

Nyimbo za maombolezo ziliimbwa na kwaya ya shirikisho ya Jimbo la Tunduru-Masasi, iliyojumuisha wanakwaya wa Parokia za Masasi na Lupaso na bendi ya TOT.

Waombolezaji walitumia zaidi ya saa mbili, kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa mpendwa wao aliyefariki dunia jijini Dar es Salaam Julai 23 usiku wa saa 3:30 kutokana na mshtuko wa moyo.

Wakati wa kutoa heshima za mwisho, baadhi ya waombolezaji walishindwa kuvumilia na kuangua kilio walipofika na kushuhudia mwili wa mpendwa wao ukiwa kwenye jeneza.

Baadaye mwili uliondolewa katika eneo hilo kwa heshima za kijeshi na kupelekwa katika eneo la kaburi lenye makaburi mengine tisa ya familia, likiwemo la baba yake, William Matwani na mama yake, Mama Stephania.

Gwaride la ndani lililojumuisha maofisa waandamizi wa jeshi lililokuwa limeubeba mwili, liliungana na gwaride la nje ya eneo la kaburi na ibada na salamu za heshima za kijeshi zilitolewa kwa gwaride la heshima na kisha Wimbo wa Taifa ulipigwa na bendi ya JWTZ kabla ya kumruhusu Askofu wa Jimbo la Tunduru-Masasi, Filbert Mhasi, kuongoza ibada ya maziko kwa kulitakasa kaburi.

Taratibu za kanisa ziliruhusu jeshi lishushe mwili wa Mkapa kaburini. Simanzi na kimya kilitanda wakati huo uliposhushwa kaburini, jeshi lilirejesha mifuniko iliyojengwa kwa zege na kuwekewa marumaru nyeusi na kufunika kaburi hilo lenye mwili wa shujaa Mzee Mkapa.

Baada ya kaburi kufunikwa, mjane wa marehemu, Mama Anna Mkapa, watoto wake Steven na Nicolaus, wajukuu na Rais Magufuli waliweka mashada ya maua kabla ya viongozi wengine.

Viongozi wengine walioweka udongo na mashada ni Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein, viongozi wengine wa mihimili ya dola, mawaziri, mabalozi wa Tanzania nje na wa nchi nyingine nchini.

Mizinga 21 iliyopigwa ilikazia maana halisi ya Mkapa alikuwa mtu wa namna gani. Awali kiongozi wa shughuli aliwatoa wasiwasi kuwa mizinga isingekuwa na madhara, lakini aliwaomba wenye matatizo ya kiafya na wajawazito waende pembeni, kwa kuwa ilikuwa imewekwa takribani hatua 15 kutoka jukwaa kuu. Kishindo kilikuwa kikubwa na minong'ono ya hapa na pale.

Wakati ikipigwa baadhi ya watu walishtuka hadi wengine kukaa chini na ilipomalizika kupigwa, wanajeshi waliohusika na tukio hilo, walipiga kelele zilizoelezwa kuwa ni ishara ya kishujaa.

Wasifu wa marehemu uliosomwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Laurian Ndumaro, ulisheheni mema na mengi hivyo kuendelea kumuelezea Mzee Mkapa kwa dunia. Mkapa ameenda na hatorudi tena. Buriani shujaa, pumzika kwa amani.

MILA na desturi zimeelezwa kuwa chanzo cha watoto kupata udumavu ...

foto
Mwandishi: Gloria Tesha, Masasi

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi