loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kwaheri shujaa Mkapa

BENJAMIN William Mkapa, Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu aliyefariki Julai 23 mwaka huu amepumzishwa katika nyumba yake ya milele kijijini kwake Lupaso, Masasi Mkoa wa Mtwara akiacha alama za utumishi uliotukuka.

Rais John Magufuli, Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Mzee Ali Hassan Mwinyi na Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete jana walijumuika na wananchi wa Lupaso na maeneo mengine ya jirani, Songea, Lindi na Dar es Salaam kumzika shujaa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wananchi wengine na jumuiya ya kimataifa waliungana nao katika maziko hayo kupitia luninga na matangazo mubashara ya redio na mitandao mbalimbali ya kijamii iliyorusha taarifa za maziko hayo kutoka kijijini Lupaso.

Ilikuwa ni maziko yaliyoashiria mwisho wa enzi za kuzaliwa na utumishi wa shujaa Mkapa (81) aliyefariki kwa shambulio la moyo akitibiwa hospitalini Dar es Salaam na kuacha ndugu, jamaa, marafiki na Watanzania wakihuzunika. Tunaungana na Rais Magufuli, mjane wa mzee Mkapa, Mama Anna, watoto wake na ndugu na wana Lupaso na Mtwara kuomboleza msiba huu mzito kwa taifa, Ukanda wa Afrika Mashariki (EAC), Kusini mwa Afrika (SADC), Afrika na dunia nzima kutokana na Mkapa kuacha alama akiwa Rais, mwanadiplomasia na msuluhishi nchi mbalimbali.

Wakati tukimsindikiza mzee Mkapa, ni matarajio yetu kifo chake kitawakumbusha wote, umuhimu wa kuishi maisha yampendezayo Mungu kadri ya vipawa na talanta walizojaliwa katika kuwatumikia wananchi wenzao vizuri.

Kwa mujibu wa Rais Kikwete, mtangulizi wake, Mkapa ameondoka akiwa ameacha alama kuu katika utumishi wake kwa nchi na jumuiya ya kimataifa na atakumbukwa kwa mengi ikiwemo kumfungulia njia ya urais bila hiyana akimteua Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa miaka 10 mfululizo licha ya kushindana naye kwenye urais mwaka 1995.

Ni alama hiyo ya moyo wa upendo, huba kwa kila mtu, moyo wa usuluhishi, uletaji maendeleo ya watu kwa kuondoa umaskini wao, Mkapa ameondoka akililiwa na kila mtu ndani na nje.

Ni matarajio yetu Watanzania wataungana na Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Mzee Mwinyi kumwombea kwa Mwenyezi Mungu apumzike kwa amani kwa kumsamehe kwa aliyoteleza katika utumishi wake na maisha ya kawaida.

Kuzikwa kwake kuwe mwanzo wa enzi mpya ya bila Mkapa tukiwasihi Watanzania kuendeleza mazuri aliyotuachia hasa suala la kufanya kazi kwa lengo la kujitegemea na kulinda uhuru wa nchi yetu ibaki katika amani, umoja, mshikamano na upendo.

Watanzania watumie maisha yake kama kioo kujitazama wanapoendelea na maisha mapya bila Mkapa na waliosuluhishwa naye, wazidi kuimarisha mshikamano mkubwa aliowaachia.

Ahsante shujaa Mkapa. Pumzika kwa amani.

TANZANIA itakuwa na ugeni mkubwa wa ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi