loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tumche Mungu kumuenzi Mkapa

MENGI yamesemwa, kuandikwa na kutangazwa kuhusu Rais mstaafu Benjamin Mkapa aliyefariki dunia usiku wa Alhamisi ya Julai 23 kuamkia Ijumaa ya Julai 24 mwaka huu.

Pamoja na yote hayo mazuri yaliyosemwa, kuandikwa na kutangazwa, jambo moja kubwa lililokuwa likitajwa mara zote ni tabia yake ya ucha Mungu ambayo ilimfanya kupenda kusali daima, kuishi uadilifu, unyenyekevu na uaminifu kwa taifa lake, watu wake na imani yake.

Kwa maoni yangu, tumuenzi Mkapa kwa kuwa na tabia ya ucha Mungu kwani ndiyo kigezo cha uadilifu, utu, wema, haki, upendo na uzalendo.

Pasipo kumcha Mungu, kila kitu ni sawa kiwe kibaya au kizuri, lakini maisha ya ucha Mungu humjenga mtu kuishi katika tabia njema na mwenendo bora kwa Mungu na kwa binadamu wenzake.

Mzee Mkapa aliishi maisha hayo ya ucha Mungu ambayo yamemjengea sifa njema ndani na nje ya Tanzania. Kwa kumcha Mungu, Mkapa alipata hekima na ufahamu katika kutatua mambo magumu ya kitaifa pamoja na kusaidia kutatua migogoro ya kisiasa kwenye mataifa mengine.

Alipofika nyumbani kwa Mkapa kwa ajili ya kuwafariji wanafamilia, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan alisema Mkapa alikuwa Mlezi wa nchi kwa kuwa wakati wowote kulipotokea jambo kubwa na lenye kutatiza, alilipatia ufumbuzi kwa urahisi.

Samia pamoja na viongozi wengine wamemtaja Mkapa kusaidia kutatua mgogoro wa kisiasa nchini Kenya na Burundi, na katika hilo, Waziri Mkuu wa Burundi, Jenerali Alain Bunyoni, alikiri juzi Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam wakati wa kutoa heshima za mwisho kitaifa kwamba Mkapa alikuwa msaada mkubwa katika kutatua mgogoro waliokuwa nao nchini humo.

Kana kwamba haitoshi, wakati akihubiri kwenye misa ya mazishi ya Mkapa jana katika Kijiji cha Lupaso wilayani Masasi mkoani Mtwara, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Songea, Damian Dallu, alisema katika kila chuo au mahali ambapo Mkapa alikwenda, alijiunga na vyama vya wanafunzi Wakatoliki au kundi la waamini wenzake.

Hii ni moja ya zawadi muhimu ambazo Mzee Mkapa ametuachia Watanzania ambayo ni maisha ya ucha Mungu.

Kwa kumtanguliza Mungu na watu mbele, aliweza kutimiza wajibu wake vyema katika kila nafasi ya uongozi aliyopewa wakati wa uhai wake, ndivyo tunavyopaswa kuishi kwa kuwa maisha yetu siyo mali yetu wenyewe bali ni ya Mungu kwa ajili ya Mungu na watu wengine.

Tukiwa wacha Mungu tutachukia dhambi, uovu, wizi, chuki, uonevu, dhuluma, na badala yake tutakuwa wema, wenye upendo, waaminifu kwa Mungu na watu, na wazalendo kwa taifa letu.

WAKATI zikiwa zimebaki siku ...

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi