loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kifo cha Mkapa na funzo la kuacha alama

MAELFU ya watanzania na wageni walifurika Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam kwa siku tatu zilizotolewa kwa ajili ya kutoa hesima zao za mwisho kwa mwili wa Rais Mstaafu Benjamin Mkapa aliyefariki Julai 23, mwaka huu usiku kwa maradhi ya mshtuko wa moyo na kuzikwa jana kijijini alikozaliwa, Lupaso, Masasi mkoani Mtwara.

Haikuwa jambo rahisi kusikia hotuba ya Rais John Magufuli, aliyotangaza usiku wa kifo hicho kwamba Mzee Mkapa hatunae tena.

Ilikuwa ni vilio na simanzi kwa kifo hicho ambacho watanzania wengi wanamlilia kwa sababu bado alikuwa na nguvu huku busara zake zikihitajika sana katika masuala mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.

Katika siku tatu za kuaga mwili huo uwanjani hapo iliyoanza Jumapili ya Julai 26, mwaka hu una kuhitimishwa Julai 28, maelfu ya wananchi walijihimu kufika uwanja wa Uhuru alfajiri wakiongozwa na Rais Magufuli, Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Iddi Seif Ally, Waziri wa Sera, uratibu na bunge, Jenista Mhagama, Spika Mstaafu Anne Makinda na viongozi wengine.

Saa 3:45 asubuhi jana,mwili wa Rais Mstaafu Mkapa uliingia viwanjani hapo huku helikopta ya polisi ikipita angani kwa mwendo pole kisha dakika chache helikopta ya jeshi la wananchi nayo ikapita uwanjani hapo kwa mwendo pole na kusimama kidogo kama ishara ya heshima na kuondoka.

Wakati huo matayarisho ya misa yakaanza na mwili ukaingia kwenye zulia jekundi ukibebwa kwenye jeneza na makanali wa jeshi la wananchi na kuzungukwa na mabregedia na kutembea mwendo wa pole kuelekea altareni tayari kuanza misa wakitanguliwa na mjane Mama Anna Mkapa na familia yake.

Kwa hali ya utulivu, misa ikaanza ikiongozwa na Askofu wa Jimbo Katoliki Iringa, Mhashamu Tarcisius Ngalalekumtwa ambaye katika mahubiri yaliyobeba ujumbe wa ‘Omba utakalo nikupe’ alimwelezea Mzee Mkapa kama mwanadamu aliyeishi maisha ya sala na kushiriki shughuli zote za kikanisa na jumuiya.

“Wakati wa uongozi wake wa urais, Mkapa aliishi kama kiongozi lakini alikuwa Mkristo wa kawaida aliyependa maisha ya sala na kushiriki ibada na jumuiya,”anasema Askofu Ngalalekumtwa.

Akizungumzia maisha ya Mzee Mkapa, Askofu Ngalalekumtwa alisema kitabu cha kiongozi huyo cha My life, My Purpose ni zawadi kwa watanzania kwani kinaelezea maisha yake yalivyo hapa duniani na kwamba amemaliza mwendo salama na matumaini yao makubwa ni huruma ya Mungu kumkaribisha mbinguni. Baada ya misa hiyo, ilifuatiwa na ibada ya buriani iliyongozwa na Askofu wa Jimbo Katoliki Tanga, Anthony Banzi, na katika misa na ibada hiyo ilihudhuriwa pia na Askofu Alfred Maluma wa Jimbo Katoliki Njombe na Askofu Agapitus Ndorobo wa Jimbo Katoliki Mahenge.

Katika salamu zao, Askofu Ndorobo alizungumza kwa niaba Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) alisema Rais Mkapa alikuwa baba aliyependa wote na Afrika kwa ujumla.

“Alisikiliza shida ya kila mmoja. Hiki ndicho tutakikosa tumepata pungufu, alishiriki kazi na shughuli mbalimbali za jamii, alikuwa na hekima, busara, tunamwambia Mungu asante,” alisema Askofu Ndorobo.

Wakizungumzia kifo hicho waombolezaji waliofika uwanjani hapo walimwelezea Mkapa kama kiongozi aliyeacha alama katika taifa kwa uongozi wake uliotukuka. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Willium Lukuvi ambaye ndiye waziri pekee wa sasa aliyebahatika kuwa waziri kuanzia serikali ya Mkapa hadi ya sasa ya Rais Magufuli, alimuelezea Mzee Mkapa kama baba na mwalimu wake wa siasa.

“Siwezi kueleza ikatosha, Mzee Mkapa kwangu ni baba, mwalimu na mshauri wangu.

Ndiye aliyenifundisha siasa na nilibahatika kuwa kwenye serikali yake kama waziri na hadi leo nimebahatika kuendelea kuwa waziri kwenye serikali hii. Nimebaki peke yangu kwa wadhifa huu,” anasema Lukuvi.

Nao wananchi waliozungumzia kifo hicho walisema wameumia kwa sababu Mzee Mkapa hakuugua muda mrefu.

“Nimeumia sana bora hata angeugua muda mrefu, yaani anaugua siku mbili na kufariki.

Kifo chake kimenigusa, nakumbuka alivyosaidia jamii yeye ndiye aliyekuwa na wazo la kuanzishwa kwa bima ya afya.

Wakati anaanzisha wapo waliopinga lakini leo inatusaidia sana. Kama si hii tungeweza kweli gharama za matibabu sisi wengine?” alihoji sema Mwalimu wa Shule ya Msingi Tabata, Saida Msofe.

Alisema, mbali na mamlaka mbalimbali za udhibiti (regulatory authorities) alizoanzisha, bima ya afya imekuwa kimbilio kubwa la wananchi wanyonge sambamba na maboresho ya sekta ya elimu alioyafanya akiwa madarakani.

“Siwezi nyamaza, namlilia Rais Mstaafu Mkapa, amefanya mengi mazuri kwa nchi yake, Mungu amlaze pema,” anase Msofe.

Foibe Jacob anasema Mzee Mkapa ni kiongozi aliyeacha alama zisizosahaulika kamwe katika maisha ya watu kwani alirejesha tumaini pale wananchi walipokata tamaa hasa kwa kuanzisha mashirika na mifuko mbalimbali ya kijamii ambayo imekuwa mkombozi wa wengi.

 

TAIFA la Tanzania hivi karibuni lilipita katika majonzi makubwa ya ...

foto
Mwandishi: Ikunda Erick

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi