loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

‘Hizi kanuni mpya za misitu ziangaliwe upya’

WIKI iliyopita tulianza kuangalia athari za tangazo la serikali la 417 ambalo ukilisoma katikati ya mstari ni kama linaondoa mamlaka ya halmashauri za vijiji kuamua namna ya kusimamia misitu iliyo katika vijiji vyao na madaraka hayo kuyapeleka kwenye mamlaka za kiserikali, hususani Mkurugenzi wa Misitu.

Tuliona pia namna bei elekezi ya mkaa inayotokana na tangazo hilo ilivyoanza kukimbiza wafanyabiashara katika vijiji vinavyovuna mkaa kwa njia endelevu wakielekea kwenye maeneo ambayo kuna uvunaji holela au kwenye vijiji vilivyo karibu na soko lao. Halikadhalika tulisikia wadau wanavyosema kuhusu hatua hiyo ya serikali kuhusu faida na hasara wanazoziona.

Je, baadhi ya viongozi katika wilaya zenye vijiji vinavyoendesha miradi endelevu ya uvunaji wa misitu wanasemaje kuhusu hatua hiyo ya serikali? Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mwezi uliopita, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kilosa (DAS) mkoani Morogoro, Yohana Kasitila, anasema kwamba hajajua kwa nini serikali imeamua kuchukua hatua hiyo.

“Pengine wana sababu nzuri… lakini ninachojua hata serikali kuu haiwezi kusema inailinda ipasavyo misitu inayoimiliki. Na ninachojua misitu ya serikali imevamiwa sana,” anasema.

Anaendelea: “Kwa hiyo ninashindwa kuona mantiki ya kupeleka usimamizi wa serikali katika misitu ya vijiji wakati ile ya kwetu tumeshindwa kuisimamia ipasavyo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo uchache wa watendaji. Mbali na kukosekana kwa nguvu kazi ya kutosha hakuna fedha za kuweza kuhudumia misitu hii ipasavyo.

“Mimi ninachoshauri ni kwamba, kwa sababu sera yetu ya nchi ni decentralization (ugatuzi wa madaraka kwenda chini), suala lingekuwa ni kufikiria serikali za vijiji zenyewe ziweze kujitegemea, zijipangie mipango yao zenyewe na ziweze kujiendeleza zenyewe,” anasema.

Anasema la msingi ambalo serikali inapaswa kufanya ni kutoa elimu ya kutosha kama iliyotolewa kwenye vijiji vinavyoendesha Usimamizi Shirikishi wa Misitu katika wilaya ya Kilosa ili elimu hiyo ieneee nchi nzima.

“Ni vyema sana wananchi wajue athari za kuvuna misitu holela, wapate elimu na kutenga matumizi bora ya ardhi. Watenge eneo la msitu la kuvuna mkaa na mbao, eneo la mifugo na watenge maeneo kwa ajili ya makazi na kilimo,” anasema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kilosa, Asajile Mwambambale, anaanza na bei elekezi akisema kwa bahati mbaya haisimamiwi kwa sehemu zote na hivyo kufanya baadhi ya watu kuwa waathirika.

Anashauri serikali kuona umuhimu wa kuhakikisha inasimamia maeneo yote yanayovuna rasilimali za misitu ili wafanyabiashara wasiwe na maeneo ya kukimbilia kwa sababu huko kuna uvunaji holela.

“Bei elekezi imewekwa ili kusaidia uvunaji kwa sababu bei ikiwa ya chini sana inachangia watu kuvuna misitu sana… Lakini lingine linalotakiwa kufanywa ni kuwawezesha wachoma mkaa na wakata mbao kujua mahala masoko yalipo ili kuondoa mtu wa katikati ambaye anasababisha bei ya mazao ya misitu kupanda. Kwa hiyo tuvune misitu sisi wenyewe, tuhifadhi misitu sisi wenyewe halafu tukauze kwenye soko. Hii itaongeza mapato,” anasema.

“Misitu ni mali na ni hifadhi ya uhai wa mwanadamu na viumbe vingine hai. Rai yangu ni kwamba wananchi wa Kilosa waamue kuhifadhi misitu katika maeneo yao kupitia serikali za vijiji. Ni muhimu wahifadhi misitu ili igeuke kuwa chanzo cha mapato katoka maeneo yao.

“Rai yangu nyingine ni wadau wengine waje kushirikiana na sisi katika kuanzisha miradi ya Usimamizi Shirikishi wa Misitu kwa sababu wafadhili wa awali (Mashirika ya TFCG, MJUMITA na TaTEDO) wameondoka. Tunataka tutoke kwenye vijiji 20 vinavyondesha Usimamizi Shirikishi wa Misitu na kuwa mara mbili ya hivyo au vijiji vyote kama vina sifa ya kuwa na misitu. Waje watusaidie utengaji wa maeneo na watusaidie elimu ya usimamizi shirikishi wa misitu.

“Rai yangu nyingine ni kwa maeneo mengine nchi nzima ambako wamejaliwa kuwa na misitu… Kama bado hawajaanza usimamizi shirikishi wa misitu kwenye ngazi za vijiji waanze mara moja kwa sababu hifadhi ya misitu ina faida. Kuna faida za kijamii na faida za kiuchumi ikiwemo kipato na hivyo kuboresha Maisha ya wananchi,” anasema.

Kuhusu vijiji kuondolewa mamlaka ya kusimamia misitu kupitia tangalo la 417, Mwambambale anasema kwamba anavyojua kwa sheria iliyopo sasa inaruhusu vijiji kusimamia misitu inayowazunguka bila kuingiliwa. “Sheria inakipa kijiji haki ya kutenga eneo la kijiji na hata kama kuna mikakati ya kupunguza madaraka ya vijiji kusimamia misitu na kujipangia mambo yake haiondoi usimamizi shirikishi wa misitu kwa vijiji wenyewe,” anasema.

Anasema kubwa ambalo linatakiwa kufanywa na vijiji ni kuonesha uwezo wa kusimamia ipasavyo misitu hiyo. “Ni kweli, tukishindwa kuendesha vizuri ndipo mawazo yanakuja kwamba mbona wanashindwa kuendesha vizuri.

Kwa hiyo ni vyema vijiji vioneshe uwezo mzuri wa kusimamia,” anasema. Anaongeza: “Lakini ni kweli pia kwamba vijiji vikinyang’anywa mamlaka ya kusimamia misitu yao itakuwa ni sawa na kuondoa ukaribu na misitu yao. Hii misitu ambayo ni ya wananchi wenyewe inalindwa vyema zaidi na wananchi wenyewe na hasa kama kunapokuwa na miradi kama ya mkaa endelevu.

“Lakini ile ambayo iko chini ya mamlaka nyingine wananchi wanajua hii si ya kwetu na hivyo kunakuwa na uvamizi. Kwa hali hiyo, ili kulinda vyema misitu hii ni vyema ikaendelea kubaki kuwa kwenye mamlaka za serikali za vijiji, lakini kuwe na dhana nzima ya ushirikishi ili wananchi wajenge dhana kwamba hiki ni cha kwetu. Huu ni msitu wa kwetu na hivyo wataulinda,” anasema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, mkoani Lindi, Renatus Mchau, anasema kwamba kwa mtazamo wake hatua ya serikali kuja na uamuzi wa kupunguza madaraka ya vijiji kusimamia misitu na kujiamulia bei haujakaa vyema.

“Nchi yetu inatekeleza sera ya ugatuaji wa madaraka kwenda kwenye serikali za mitaa kwa maana ya kushirikisha vijiji, mitaa na halmashauri katika usimamizi wa shughuli mbalimbali. Eneo moja wapo ni hizi raslimali zilizopo,” anasema.

Anaendelea: “Sisi tungetamani kuona vijiji vyetu vinasimamia rasilimali hizi, na eneo mojawapo ambalo linazifanya hizi serikali za vijiji zipate nguvu ya kiuchumi ni rasilimali ambazo zinawezesha kupata fedha.”

Akitolea mfano wa kijiji cha Nanjirinji, Mkurugenzi huyo anasema baadhi ya misitu ambayo imekuwa ikisimamiwa na vijiji imekuwa ni misitu yenye manufaa sana kwa wananchi na kwa halmashauri kwa ujumla. “Hawa wamekuwa na miradi endelevu inayotokana na rasilimali misitu. Wanapata pesa wanazowekeza katika miradi ya maendeleo. Kwa mfano sasa (Nanjirinji) wana gesti ambayo inaleta manufaa kwa kijiji.

“Lakini pia wamekuwa wakitekeleza shughuli nyingine za maendeleo. Kwa mfano sasa hivi tunajenga kituo cha polisi katika hicho kijiji. Serikali ya kijiji nayo imetoa fedha ili kutekeleza ujenzi wa kituo. Kuna miradi mingine wanayotekeleza ikiwemo ujenzi wa shule, huduma katika vituo vya afya na yote ni kutokana na fedha zinazotokana na rasilimali misitu. Wanasaidia wajawazito, wanafunzi wanaofaulu kujiunga na sekondari na yote haya ni kutokana na fedha zinazotokana na rasilimali misitu,” anasema.

Anasema kitu kizuri zaidi ni kwamba hawavuni tu holela bali wana programu mbalimbali kwa ajili ya kulinda hiyo misitu na kufanya uvunaji kwa njia ndelevu.

“Hatua hii imekuwa inaturahisishia sisi kama halmashauri au wilaya kusimamia misitu yao kwani wanakuwa wako karibu na misitu na kwa vile wanaona manufaa yake wanaisimamia vizuri sana,” anasema.

Anasema kutokana na vijiji kadhaa wilayani Kilwa kufanya vizuri katika suala zima la usimamizi shirikishi wa misitu, wamekuwa wakitamani hali kama hiyo isambae pia katika vijiji vingine katika halmashauri hiyo. Itaendela

TAIFA la Tanzania hivi karibuni lilipita katika majonzi makubwa ya ...

foto
Mwandishi: Hamisi Kibari

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi