loader
Dstv Habarileo  Mobile
TPA
Picha

Shein aanza kuaga

RAIS wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein ameaga katika Braza la Idd el Hajj na kutaka vyama vya siasa katika uchaguzi mkuu mwaka huu kufanya kampeni za kuhubiri amani na mshikamano.

Akihutubia Baraza la Iddi el Hajj, Bumbwini katika Wilaya Kaskazini B Unguja, alisema matarajio yake makubwa ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28 mwaka huu ni kuwa huru na wa haki kutokana na kukamilika kwa maandalizi mengi mapema. 

Dk Shein ambaye alisisitiza kuwa muda wake wa kuondoka madarakani unakaribia na hataongeza dakika yoyote, alisema uchaguzi huru na haki utatokana na wanasiasa wenyewe kujiepusha na kauli zenye lengo la kupandikiza chuki na uhasama.

“Sote tunafahamu kwamba baada ya kufanyika uchaguzi mkuu wa mwaka huu wa 2020, na kupatikana Rais mwingine wa Zanzibar kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya 1984, ndio itakuwa mwisho wa uongozi wangu,” alisema Dk Shein. 

Aliendelea kusema, “kwa hivyo hapana shaka kwamba, shughuli hii ya Baraza la Idd el Hajj tunayofanya leo, Mwenyezi Mungu akipenda itakuwa ni ya mwisho kwangu kuhudhuria na kutoa hotuba nikiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi”.

Aliwashukuru wananchi wote wa Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jumla kwa mapenzi makubwa waliyomuonesha kwake na kwa kuunga mkono serikali katika kutekeleza majukumu kwa vipindi vyote viwili vya SMZ awamu ya saba. 

“Huu ni mwaka wa uchaguzi, ifikapo Oktoba 28...matarajio yangu makubwa kwamba vyama vya siasa kupitia wagombea wao watajinadi kwa wapiga kura kwa kutangaza ilani na sera huku msisitizo mkubwa ni kuhubiri amani na utulivu,” alisema.

Aliwataka viongozi wa vyama vya siasa kutekeleza majukumu yao ya kufanya kampeni katika kipindi chote kwa kuzingatia sheria na kanuni za uchaguzi ziliopo kupitia Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

“Uchaguzi unaongozwa na sheria na kanuni ambazo viongozi wa vyama vya siasa vyote mnazijua kwa sababu mmefikia makubaliano na kusaini matamko hayo…nataka myazingatie kwa makini sana,”alisema.

Alisema kipindi cha harakati za kampeni za uchaguzi mkuu kitumiwe kama kipimo cha kutafuta viongozi na siyo kusababisha  mifarakano na kupandikiza chuki za kisiasa.

Dk Shein alitumia nafasi hiyo kukumbusha Waislamu pamoja na waumini wengine kwa ujumla kwamba kitabu kitakatifu cha Kurani suratil Al Imran, Mwenyezi Mungu amewataka waja wake na kuwaambia 'shikamaneni kwa kamba ya (dini) wala msifarikiyane’.

Dk Shein alitumia nafasi hiyo kuwaaga Waislamu waliohudhuria sherehe za Baraza la Idd el Hajj na kusema ni za mwisho akiwa Rais kwani baada ya uchaguzi, atakuwa amemaliza muda wake wa kuwapo madarakani kwa miaka 10. 

Alisema sherehe hizo zimekuwa zikifanyika katika sehemu mbali mbali Unguja na Pemba zikitoa nafasi na fursa kwa Waislamu kujumuika pamoja na viongozi wao katika kufanya ibada.

“Sherehe hizi za baraza la Idd el Hajj ndiyo za mwisho kwangu kufuatia kumaliza muda wangu wa kuwepo madarakani katika kipindi cha miaka kumi...ni utaratibu mzuri ambao umetuwezesha sisi Waislamu kujumuika pamoja na kubadilisha mawazo kwa ajili ya kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazotukabili,” alisema. 

Rais alitumia nafasi hiyo kuwapa pole Waislamu nchini ambao walikuwa katika matayarisho ya kuhudhuria ibada ya hijja Makka na kushindwa kutekeleza dhamira zao kutokana na janga la corona linazozikabili nchi mbali mbali duniani.

Alizitaka taasisi zinazoshughulikia safari ya ibada ya hijja kufanya maandalizi ya mapema kwa mahujaji walioshindwa kufanya safari hiyo waweze kutekeleza ibada hiyo kipindi kingine. 

Aidha aliwajulisha wananchi kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kupambana na ugonjwa wa Covid 19 unaosababishwa na virusi vya corona akisema kwa sasa umetokomezwa ikiwa hakuna mgonjwa yeyote katika vituo vilivyotengwa kulaza wagonjwa hao.

Hata hivyo aliwataka wananchi kuchukua tahadhari zaidi kwa sababu ugonjwa upo katika baadhi ya nchi jirani ambazo baadhi ya shughuli muhimu zimesitishwa kutokana na tishio lake.

“Nataka niwaaambie wananchi kwamba Serikali yenu imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kupambana na ugonjwa wa corona ambao kwa sasa umedhibitiwa na kutokomezwa...lakini tuchukue tahadhari zaidi kwa sababu ugonjwa upo katika baadhi ya nchi jirani,” alisema.

Aliwataka Waislamu kuwa na subra na uvumilivu akisema hiyo ndiyo mitihani ya Mwenyezi Mungu ambayo waja wake lazima wakabiliane nayo. 

Awali, Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Kabi alimpongeza Dk Shein kwa uongozi bora katika kipindi cha miaka 10 akisema mfano wa kuigwa.

“Sisi Waislamu tunakutakia kila la kheri katika safari ya mapumziko yako baada ya kumaliza muda wa uongozi huku tukiamini kwamba tutakuwa tukishirikiana na wewe katika shughuli mbali mbali za kijamii na ibada,”alisema.

Waislamu duniani husherehekea sikukuu ya Iddi el Hajj kutokana na kumalizika kwa ibada ya hijja Makka, Sauda Arabia ambayo ni miongoni mwa nguzo tano za dini ya Kiislamu ambayo muumini hutakiwa kuitekeleza mara moja katika maisha yake.

Katika sherehe hizo zilihudhuriwa na viongozi mbali mbali akiwamo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Samia Suluhu Hassan pamoja na mgombea wa urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Dk Hussein Mwinyi na mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Muungano.  

MELI kubwa ya mizigo yenye tani 55,000 imetia ...

foto
Mwandishi: Khatib Suleiman, Zanzibar

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi