loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Ukosefu huduma za ugani waathiri misitu

KUKOSEKANA  huduma za ugani misitu na nyuki kunafanya wadau hasa vijijini wasiweze kufanya vizuri  kupanda miti na kuitunza na kushindwa kuhifadhi misitu ya asili iliyopo.

 Hali hiyo inatokana nakutozingatia namna ya kusimamia na kutumia vizuri rasilimali misitu nchini bila kuleta madhara kwa mazingira.

 Aliyekuwa Mkurugenzi wa Misitu na Nyuki nchini, Dk Felician Kilahama alisema hayo  Dar es Salaam na kuongeza hali ya misitu vijijini na maeneo yaliyohifadhiwa hairidhishi.

Alisema ni vyema changamoto hiyo ikatafutiwa ufumbuzi haraka na wadau wake kwani elimu kwa umma, kuhusu rasilimali misitu na nyuki inatakiwa iwe endelevu. 

 Alisema mazingira yanaendelea kuharibika kwa sababu watu vijijini wanakosa maarifa, hawajui wafanye nini kuinusuru misitu na uoto wa asili visitoweke kwa kasi hadi mazingira kuhatarisha maisha ya viumbe hai.

 "Ili kurekebisha hali hiyo ni muhimu suala la huduma za ugani katika misitu na nyuki lipewe kipaumbele badala ya kuacha kama ilivyojitokeza miaka ya karibuni," alisema.

 Alisema ipo haja ya kutengwa kwa bajeti ya kutosha na kuwepo wataalamu wa kufanya kazi hiyo kwa kushirikiana na sekta nyingine kama kilimo, mifugo, uvuvi, wanyamapori, maendeleo ya jamii na halmashauri zote bila kusahau sekta binafsi na taasisi na asasi mbalimbali za ndani na kutoka nje ya nchi.

 Alisema uhifadhi mazingira kwa kushirikisha jamii na wadau siyo muhimu tu kwa nchi yetu bali pia ni agenda ya dunia nzima na mkazo unatakiwa uwekwe kurejesha uoto wa asili na kuimarisha ikolojia itokanayo na misitu asili.

Alisema  ipo haja ya kuimarisha mbinu za matumizi endelevu ya misitu na ardhi ili kuleta tija kupitia kilimo kijani katika kuelekea uchumi wa viwanda.

Alisema kufanya hivyo kutachangia kufanikisha malengo ya dunia ya milenia ya kuondoa umasikini ifikapo mwaka 2030, kwa Tanzania kuwa na uchumi endelevu mpaka kufikia taifa la kipato cha kati ifikapo 2025. 

Dk Kilahama alisema Tanzania Bara imebahatika kuwa na eneo la ardhi lenye hekta milioni  88.6  sawa na (kilometa za mraba 886,000), kati ya eneo hilo asilimia 38 imefunikwa na rasilimali misitu ambayo ni muhimu kwa utunzaji wa mazingira, ikolojia na bayoanuwai mfano, makazi ya wanyamapori ikiwemo nyuki, kuhifadhi vyanzo vya mito.

Kadhalika, alisema  misitu inasaidia  kuhifadhi na kurutubisha udongo kwa kupunguza kasi ya kumomonyoka kwa udongo ambao huishia kwenye mabonde na mito, mabwawa au ziwani na pia baharini hasa wakati wa majira ya mvua.

Pia alisema misitu ni chanzo muhimu cha bidhaa zinazotumiwa na watu na wanyama pia.

MILA na desturi zimeelezwa kuwa chanzo cha watoto kupata udumavu ...

foto
Mwandishi: Lucy Lyatuu

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi