loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mzee Mkapa Ulimaanisha nini?

MWAKA 2018 tarehe ambayo bahati mbaya siikumbuki nilipokea simu yenye sauti nzito kutoka kwa mzungumzaji wa upande wa pili:

"Mkurugenzi hujambo?"

"Mimi ni Mzee Mkapa'" alijitambulisha kwangu Mzee Benjamin William Mkapa, Rais Mstaafu na kiongozi wetu mpendwa wa Awamu ya Tatu tuliyemzika kijijini Lupaso, Masasi, Mtwara, Jumatano ya Julai 29, 2020 na kuhitimisha mwendo wa miaka 81 alioutembea dunia hii. 

Licha ya kujitambulisha kwake, bado ilikuwa vigumu kuamini nilikuwa nimepokea simu ya Mzee Mkapa kufuatia kujitambulisha kwake kwangu kwa unyenyekevu vile tena kwa mtu mdogo kwake kiumri na kiuongozi kama mimi.

Si kwamba katika maisha yangu ya kikazi kwa sasa sipati nafasi ya kuzungumza na viongozi wakuu au mashuhuri wa aina yake, la hasha!

Au kwamba  huko nyuma kama mwanahabari sijawahi kupata fursa kufanya mahojiano na viongozi wakuu wa kitaifa wa nchi, la hasha!

Nikiwa mmoja wa wahariri vijana barobaro na mwanahabari za maisha ya viongozi mashuhuri wakati huo, nimepata kukutana na kuwahoji viongozi wakubwa katika mihimili yote ya dola na pia katika mawanda ya diplomasia duniani.

Nimepata kumhoji Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne,  Jakaya Kikwete siku Taifa Stars ilipoifunga Burkina Faso nyumbani kwao michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika.

 Pia nimepata kumhoji aliyekuwa Spika wa Bunge, Samuel Sitta wakati wa sakata la Richmond na nimepata kumhoji Jaji Mkuu, Barnabas Samatta siku alipostaafu rasmi.

Aidha, niliwahi kumhoji Jaji Mkuu, Augustino Ramadhani siku alipoanza majukumu yake rasmi na pia Mama Fatma Karume kujua kwa undani historia ya Mapinduzi ya Zanzibar na kifo cha Mzee Abeid Aman Karume n.k.

Zaidi niliwahi kuwahoji wanadiplomasia wengi akiwamo Balozi wa Marekani nchini, Balozi Mark Green alipokuwa akihitimisha safari yake ya kikazi Tanzania.

Hata hivyo, tofauti yake hapa ni kwamba, simu ya Mzee Mkapa niliyopokea siku ile ilikuwa ni ya kipekee na itabaki maalumu na wosia muhimu kwangu na nitakaowataja katika yulojia hii. 

Mosi, siku hiyo nilipokea simu na kuzungumza kwa mara ya kwanza na ya mwisho katika maisha yangu na mtu wa aina ya Mzee Mkapa, galacha katika fasihi, nguli katika fonetiki, manju wa sintaksi na simantiksi za Kiingereza tuliyekuwa tunamuona kama rejea shuleni.

Wakati akiwa kiongozi katika ngazi mbalimbali za uwaziri na baadaye urais, sisi wanafunzi wa fasihi na simantiksi kila tulipomsikiliza Mzee Mkapa, tulimtumia kama rejea kwa kufuatilia hotuba zake alizotoa ndani na nje ya nchi hasa anapochapa kimombo lakini pia hata Kiswahili. 

Alikuwa kamusi yetu ya misamiati mipya na rejea yetu katika matamshi. Kwa wanaotaka kuamini hili soma pia "My Life, My Purpose" uvune hazina ya misamiati aliyotumia Mkapa.

Kwa hivyo siku ile nilipopokea simu ya "role model" wangu katika mawanda ya fasihi katika  Kiingereza, moja ya masomo ya lugha niliyochukua katika elimu ya juu ya sekondari. Nadhani unaelewa furaha unayoweza kuwa nayo! 

Pili, ukiacha shida aliyokuwa nayo ya kuhitaji picha za kumbukumbu kutoka kwenye maktaba ya Idara ya Habari-MAELEZO niliyokuwa naiongoza wakati huo, simu ile itabaki kuwa chachu ya kuendelea kumuenzi Mzee Mkapa!

Ni katika simu ile unapata nguvu kupongezwa na mtu wa aina ya Mzee Mkapa. Siku ile nakumbuka alisema: "MAELEZO naijua sana, mmepabadilisha mno kwa sasa, endeleeni kufanya mageuzi." Kabla sijaendelea, ujumbe ule niliutoa na sasa nautoa tena "dedication" kwa TeamMAELEZO wooote popote walipo. 

Tatu. Hili pengine ndilo linalonifikirisha sana, kunitafakarisha na kunifanya nipekeche macho yangu kuzuia machozi kumkumbuka Mzee Mkapa ambaye tayari tumemlaza kwenye nyumba yake ya milele pale kijijini Lupaso.

Ni hivi: Baada ya kuwa ameniomba nimtafutie kwenye maktaba yetu picha za rafikiye, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uswisi, Olof Palme, aliyepata kuja nchini miaka ya 1970 (na kwa bahati nzuri picha zikawepo za kutosha), Mzee Mkapa akaniambia mambo mengine mawili muhimu yaliyo katika tanzia yangu hii.

Kwanza, ni katika mazungumzo haya ndipo Mzee Mkapa alinidokeza alikuwa mbioni kukamilisha kitabu kuhusu maisha yake ambapo alisema: “nitawategemea sana hapo MAELEZO kwa picha zaidi za kumbukumbu muhimu za maisha yangu hasa zile za kikazi!

Na hakika TeamMAELEZO hatukumwangusha. Nilifarijika mwaka jana aliponiletea mwaliko wa uzinduzi na baadaye nakala ya bure ya kitabu chake "My Life, My Purpose; A Tanzanian President Remembers." 

Picha kutoka maktaba ya Idara ya Habari-MAELEZO ni miongoni mwa zilizosawiri kitabu chake hicho na kila alipozitumia alinakilisha hati miliki ya picha hizo kuwa ni za MAELEZO au Tanzania Information Services.

Mzee Mkapa aliijua vyema Idara ya Habari-MAELEZO, kwani SHIHATA aliyoianzisha ilizaliwa kutoka ubavu wa MAELEZO.

 Na zaidi, miaka mingi baadaye ilipohitimisha kazi zake; majukumu, mali na wafanyakazi walirejea MAELEZO na  baadhi ya wasaidizi wake waandamizi wa habari akiwemo dada Maura Mwingira walipita/ kutoka MAELEZO. 

La Pili, tukiendelea na simu yake ya mwaka 2018: wakati tunaendelea kumshukuru kwa kitabu chake na uungwana wake wa kunakilisha hatimiliki ya picha kadhaa alizotumia kwa MAELEZO, fauka ya hayo, kama kuna kitu kinaniliza leo na nilikuwa na wakati mgumu  kijijini Lupaso nikimkumbuka Mzee Mkapa ni kile cha mwisho alichoomba katika simu ile na bahati mbaya sikupata kuzungumza naye tena:

"Nitawategemea sana MAELEZO katika machapisho yangu mengi, mna hazina kubwa ya picha. Nitaendelea kuhitaji msaada wenu."

Leo Mzee Mkapa hatunaye tena, ametangulia mbele za haki, ametenda wema amekwenda zake, kwa Mola wake, hakutazama nyuma lakini leo kuna ya kutafakari katika kauli yake hii. 

Mengi yameandikwa, yamesemwa lakini leo nikiwa nimerejea jijini Dar es Salaam jioni hii na viongozi wengine wa nch,i najiona nimebaki mpweke na nimejiuliza sana niandike? Na kama ndiyo ni kuhusu nini kumhusu Mzee Mkapa? 

Lakini roho imeniambia lazima nimuage Mzee Mkapa kwa kuandika kitu. Sasa naandika nini? Ningeweza kueleza aliyoyafanya katika sekta mbalimbali za umma, habari na michezo nchini.

 Ningeweza pia kuzungumzia mageuzi yake aliyosimamia kwa kuunda taasisi za huduma kama Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Taasisi ya Kupambana na Kudhibiti Rushwa (PCCB) na mashirika mengine mengi nchini.

Lakini haya yameandikwa na kusemwa vya kutosha. Nikiri imenichukua zaidi ya siku sita za kuamua niandike nini! Maana lazima niandike kumuaga mwandishi mahiri kwa andiko stahiki! 

Nikiwa mtu mwenye mapenzi makubwa na fasihi, nimeandika tanzia nyingi kuhusu siku na maisha ya viongozi wengi duniani lakini pia nimesoma tawasifu za viongozi wengi duniani ikiwemo ya Mzee Mkapa; nikiri kuandika maneno machache kumhusu ilikuwa ngumu.

Sikubahatika kufanya kazi kwa karibu na Mzee Mkapa akiwa madarakani, sikubahatika kufanya naye kazi kwa karibu akiwa Rais mstaafu, lakini unapomfanyia Dhukuru mtu wa aina ya Mzee Ben Mkapa unabaini, kwa minajili ya athari chanya zinazotokana na maono yake na kazi zake, amekuwa mtu adhimu na adimu, na johari yenye thamani zaidi kuliko tu kuwa naye karibu. 

Linaloniuma sana ni ahadi yake hasa siku ile aliponipigia simu aliposema: "Nitaendelea kuhitaji msaada wenu!" Kweli inafikirisha! 

Nimeeleza hapo juu, tulishamsaidia kupitia wasaidizi wake, kumpatia baadhi ya picha kwa ajili ya chapisho la rafiki yake, Olof Palme na nyingine akazitumia katika "My Life, My Purpose". Lakini alimaanisha nini kusema "nitaendelea kuhitaji msaada wenu? Hili linabaki kuwa fumbo kuu kwani ameondoka! 

Januari 31 mwaka huu, Rais Magufuli aliniteua kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na hivyo kuniondoa MAELEZO, iliyokuwa ofisi yangu kila siku. Nimehamia na "nashinda" wizarani.

Ingawa siku tatu baadaye, Februari 3, Rais John Magufuli alinirejeshea jukumu la kuendelea kuwa Msemaji Mkuu wa Serikali, kimsingi, pamoja na majukumu ya kila siku, bado "nashinda"  wizarani na si tena MAELEZO!

Alichokisema Mzee Mkapa katika ujumbe wake wa "nitaendelea kuhitaji msaada wenu" ni fumbo kuu. Sasa najaribu kuendelea kulielewa. 

Na kama ilivyoandikwa katika Biblia kuwa ni wale tu wenye uelewa ndio wataelewa maana ya unabii na kama inavyoelezwa katika Quran Tukufu kuwa "Fadhakir Inafaat Dhikira" (Kumbusha Iwapo ni Muhimu Kufanya Hivyo), basi kauli hii ya Mzee Mkapa inabaki na maana kubwa kwangu na kwa wanatasnia wenzangu. 

Na ninawakumbusha. Leo Mzee Mkapa hayupo nasi lakini nataka kuamini tunapaswa kuendelea kuwa naye kitasnia. Wenzangu pale MAELEZO na tamathali ya jumla ya Idara ya MAELEZO ikiakisi vitengo vyote vya habari serikalini alivyovianzisha mwaka 2003 na hata tasnia ya habari kwa ujumla iliyomjenga, nataka kusema nanyi hapa katika tanbihi ya dhukuru hii.

Katika tamathali ya "nitaendelea kuhitaji msaada wenu" Mzee Mkapa ana fumbo kubwa alilotuachia; naamini anataka si MAELEZO tu, bali sote wanatasnia, tuendelee kumuenzi akiwa ameshatuachia namna ya kufanya hivyo kupitia falsafa yake ya "Ora Et Labora" (Sala na Kazi).

Nayaandika haya kuwakumbusha tu wenzangu kuwa Mzee Mkapa hajakamilisha mahitaji yake kwetu na kwamba, ninavyoendelea kuuelewa unabii katika tamko lake, ni kwamba kimwili alihitaji tumsaidie siyo tu kwa picha, bali bado kiroho anatuhitaji sana na ataendelea kutuhitaji.

Juzi saa sita usiku nilipigiwa simu ikihitajika picha ya Mzee Mkapa kwa ajili ya sehemu ya maziko yake. Nilifikiria sana. Usiku wa siku moja kabla ya maziko yake, nilipata ujumbe saa 11 alfajiri kuhusu mashada ya maua ya kwenda kuwekwa kwenye kaburi lake. Kumbe, wenye kuelewa maana sasa tunapaswa kuzidi kuelewa. 

Mzee Mkapa ameendelea "kuhitaji msaada wenu" hata akiwa amelala kwenye jeneza lile. Hata sasa akiwa amelala katika nyumba yake ya milele bado anaendelea kuhitaji msaada wetu. 

Tuendelee kusali kumwombea na kuwaombea marehemu wengine wote kila tupatapo nafasi. Lakini sala haitoshi, ametuonesha shauku yake kwetu kuwa ni pamoja na kuchapa kazi! 

Nazungumza tena na watu wangu wa MAELEZO kama namna nyingine ya kuupambanua ufunuo wa Mzee Mkapa kwangu, kuwa si MAELEZO tu atakaowahitaji. Hapana.

Katika "Ora Et Labora" niwaombe Watanzania tumuenzi Mzee Mkapa kwa yote na tumsamehe alipotukosea, iwapo lipo alilotukosea au kutukwaza na wanatasnia ya habari kwa upana wake tumuenzi Mzee wetu kwa sala na maombi.

Katika "Ora Et Labora" Mzee Mkapa anatuhimiza kuchapa kazi. Niwakumbushe Watanzania, WanaMAELEZO, tasnia ya habari na maofisa habari serikalini, Mzee Mkapa aliposema atatutegemea si kwa sala tu bali KAZI.

Tuchape kazi hasa, tutimize wajibu wetu katika taaluma hasa na tusitetereke katika kulinda amani, utulivu na mshikamano na kuenzi misingi ya fani zetu aliyotuachia Mzee Mkapa.

Fumbo la ujumbe wake kuwa "nitaendelea kuhitaji msaada wenu" lilikuwa la kinabii na linalohusu maisha ya dunia na ahera pia.

Huenda hapa duniani Mzee Mkapa alihitaji picha na tulishampa katika "My Life, My Purpose" lakini katika maisha ya ahera, kauli ya Mzee Mkapa, inabaki fumbo, tuendelee kulifumbua.

Leo ametangulia mbele ya haki, Mzee Mkapa hahitaji picha, mabango tena, wala mashada. Anahitaji sala na maombi yetu. Anahitaji tuyaenzi aliyoyaamini kwa kazi kweli kweli! 

Hakika ametuachia mtihani mzito ndio maana nabaki naelewa lakini bado pia nabaki najiuliza kila mara: Mzee Mkapa kwa kauli ya "nitahitaji msaada wenu" na yaliyokufika Julai 23, 2020 alipofariki Mzee Mkapa Ulimaanisha Nini? Itakuwa Lini tena? Na wapi tutakuona tukupe ulichotamani na kuomba tuendelee tukusaidie?

Hakika Mzee Mkapa umetuachia fumbo kuu, tutaendelea kulifumbua kupitia Ora et Labora. Mola akupe pumziko la amani na la milele Mzee Mkapa,  galacha wetu wa simantiksi, sintaksi na fonetiki uliyeacha alama za kukumbukwa milele katika nchi yetu na dunia!

Mwandishi wa tanzia hii ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 

MILA na desturi zimeelezwa kuwa chanzo cha watoto kupata udumavu ...

foto
Mwandishi: Dk Hassan Abbasi

1 Comments

  • avatar
    Musa Michael Sewando
    01/08/2020

    Nakupongeza sana kwa Makala yako ya kumuelezea Mzee Benjamin William Mkapa. Ushauri wangu ni kwamba nadhani alikuwa na nia ya kuandika Kitabu kingine na machapisho mengine ndio maana alisema ataendelea kuhitaji msaada wenu. Pia nashauri ajitokeze mwandishi mzuri wa vitabu anayeweza kukusanya Hotuba zake na kuzichapisha ili ziweze kutoa dira nzuri kwa masuala ya Utawala, Uongozi, Uchumi, Afya, Elimu n.k.

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi