loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

‘Tumieni kitabu cha Mkapa kujitathimini’

VIONGOZI mbalimbali wakiwamo wa kisiasa wametakiwa kusoma na kutumia maarifa yaliyomo kwenye kitabu cha My Life, My Purpose cha Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa  kujitathimini utendaji wao wa kazi unavyohakikishia wananchi ubora wa maisha. 

Rais mstaafu Mkapa ambaye alizikwa kijijini kwake Lupaso wilayani Masasi katika Mkoa wa Mtwara, alifariki dunia Julai 23, mwaka huu, jijini Dar es Salaam baada ya moyo kusimama kwa mshtuko ulioambatana na homa ya malaria.

Miongoni mwa watu waliozungumza na gazeti hili, wamesema kutokana na mafanikio, msingi wa maendeleo na uchumi uliojengwa na Mkapa, viongozi hawana budi kufuata nyayo zake hususani kuhakikisha wananchi wanakuwa na maisha bora.

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Wilaya ya Morogoro mjini, Abeid Mlapakolo alisema miongoni mwa vitu vya kujivunia alivyoacha Mkapa, ni kupigania nchi yake kwa maslahi ya wananchi. Alisema viongozi na wananchi kwa jumla, wanayo fursa ya kusoma kitabu chake waweze kujitathimini na kujikosoa wakiwa hai. 

“Hiki kitabu kikisomwa na viongozi, wataweza kujitathimini na kujikosoa wao wenyewe…kikubwa,  wafanye kazi kwa maslahi ya taifa lakini pia waishi wakijua kuwa ipo siku watakuwa hawapo kwenye vyeo wanavyoshikilia,”alisema. 

Kiongozi huyo wa CUF alipongeza namna wananchi walijitokeza kuaga mwili wa Mkapa na kusema kitendo hicho kimeonesha umoja walionao Watanzania bila kujali tofauti za kiitikadi.

Wengine waliozungumza na gazeti hili, walihimiza umuhimu wa viongozi kufuata nyayo ya kujenga Tanzania yenye demokrasia ya kweli inayoweka misingi ya haki na usawa mbele, kama alivyofanya Mkapa wakati wa uongozi wake.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ruaha mkoani Iringa (RUCO), Profesa Gaudence Mpangala alisema Mkapa alikuwa na mchango mkubwa kama kiongozi katika maendeleo ya Tanzania.

“Viongozi wengine hawana budi kufuata nyayo zake kama ambavyo Moi alifuata nyayo za Kenyatta hadi akaitwa mzee wa nyayo. Waangalie yale mazuri aliyoyafanya ambayo ni mengi na mafanikio yake yanaonekana,”alisema Profesa Mpangala.

Akieleza kuhusu uchumi na huduma wakati wa utawala wa Mkapa, alisema alijenga misingi mizuri iliyolenga kuondoa umasikini miongoni mwa Watanzania.

“Sasa hili ndio liwe lengo kuu la maendeleo, viongozi, serikali na mfumo wa siasa ilibebe kuhakikisha maisha ya wananchi yanakuwa bora kwa maana ya makazi bora, majisafi, elimu, usafiri na afya bora,”alisisitiza.

Alisema mzee Mkapa aliendeleza kwa kiasi chake aliyoachiwa na waliomtangulia katika eneo hilo la uchumi na kuondoa umasikini na waliomfuata wameendeleza hadi nchi ilipofikia.

Kwa upande wa siasa, mhadhiri huyo alisema Rais Mkapa ndiye rais wa kwanza kuingia madarakani kupitia uchaguzi uliohusisha vyama vingi na alijitahidi kujenga misingi ya demokrasia jambo ambalo viongozi waliopo na wanaokuja wanatakiwa kuliendeleza. 

Alisema mwaka 1962, Mwalimu Julius Nyerere alipohutubia Bunge la kwanza la Jamhuri ya Tanganyika alisema Tanganyika itajengwa kwa kulinda haki za binadamu, jambo ambalo pia Mkapa aliliendeleza na kwenye kitabu chake alilizungumzia. 

Tangu kifo cha Mkapa kilichotoka mwishoni mwa wiki iliyopita, viongozi mbalimbali na wananchi wamezungumzia mchango wake kwa taifa la Watanzania, ikiwemo jitihada zake za kujenga uchumi imara wa Tanzania kwa kufanya mageuzi mbalimbali ndani na nje ya serikali yake.

MILA na desturi zimeelezwa kuwa chanzo cha watoto kupata udumavu ...

foto
Mwandishi: Halima Mlacha

1 Comments

  • avatar
    Musa Michael Sewando
    01/08/2020

    Nashauri Vyombo vya Habari kutengeneza Vipindi vya Radio na Television ambavyo vitakuwa vinaangazia Mambo na Hotuba zake alizokuwa anazitoa kabla ya Utawala wake wa Urais, wakati wa Utawala wake wa Urais na baada ya Utawala wake wa Urais. Hii itasaidia kuwakumbusha viongozi wajibu wao kwa Wananchi na kuongeza uzalendo kwa Vizazi vijavyo.

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi